Mbinu za kukabiliana na kigezo cha uzoefu kazini kwa waombaji wa ajira

Muktasari:

  • Jambo hili limesababisha vijana wengi kuona kama si jambo jema na limekaa kibaguzi huku wengine wakihoji, “nimemaliza chuo mwaka huu, huo uzoefu nautoa wapi?”

Moja ya changamoto kubwa wanayokumbana nayo watafuta ajira hasa wahitimu wa taasisi za elimu ya juu ni kigezo cha uzoefu. Waajiri wengi huweka kigezo cha uzoefu kama moja ya sifa muhimu za kuajiri.

Jambo hili limesababisha vijana wengi kuona kama si jambo jema na limekaa kibaguzi huku wengine wakihoji, “nimemaliza chuo mwaka huu, huo uzoefu nautoa wapi?”

Waajiri nao wamekuwa wakijitetea kuwa elimu ya darasani pekee haitoshi kumfanya muhitimu awe na sifa stahiki za kuajiriwa na kwa kuzingatia kuwa biashara zinahusisha uwekezaji mkubwa, waajiri wanaona kumwajiri mtu asiye na uzoefu ni kama kupima maji kwa mguu.

Kwa kuzingatia kuwa mwajiri ana haki ya kumchagua mtu yeyote anayetaka kukidhi mahitaji yake njia bora ya kutatua tatizo hili si kulaumu, lakini ni kutafuta suluhisho la kukabiliana na hiki kigezo cha uzoefu. Ziko mbinu kadhaa ambazo watafuta ajira wanaweza kuzitumia ili kuhakikisha wanafanikisha malengo yao ya kupata ajira.

Kujitolea

Ukweli ni kwamba, hauwezi kupata uzoefu bila kufanya kazi, inakulazimu kufanya kazi ili kuweza kupata huo uzoefu. Kupata kazi ya kuajiriwa kwa mkataba wa malipo ni changamoto, hivyo kujitolea kunaweza kuwa njia mbadala ya kupata uzoefu.

Wengi wa vijana niliowashauri kuhusu suala la kujitolea wamekuwa wakijitetea kwamba siku hizi hata nafasi za kujitolea zimekuwa changamoto kuzipata.

Utetezi huu una ukweli usio na shaka, lakini hauwezi kwenda kufanya kazi hata kama ni ya kujitolea kama hakuna uhitaji.

Vijana wengi hujikuta wakiwa kwenye changamoto ya kukosa hata nafasi ya kujitolea kwa sababu ya shauku ya kufanya kazi kwenye taasisi au kampuni kubwa zinazovutia.

Kwa bahati mbaya, taasisi hizi mara nyingi huwa zimejitosheleza. Ni vyema kuanza kwa kutafuta nafasi za kujitolea kwenye taasisi changa au zile zenye uhitaji, lakini zina changamoto ya kuajiri kwa sababu ya ufinyu wa bajeti.

Taasisi hizi ndogondogo ni mwanzo mzuri kwa vijana kupata uzoefu, lakini pia kutengeneza mtandao unaoweza kuwapa fursa ya kuajiriwa baadaye.

Mara nyingi wanaopata kazi ni wale wenye kazi tayari, hivyo kuwa kwenye taasisi ni sehemu nzuri ya kuonyesha uwezo wao na kukutana na wadau wanaoweza kuwaajiri au kuona uwezo wao na kumuunganisha na waajiri wengine.

Tafuta fursa za kujitolea kwenye asasi ndogondogo za kiraia au kifedha, kwenye shule na sehemu nyingine ambazo hazina ushindani.

Wapo watakao sema pia kujitolea kuna hitaji nauli kwenda kazini na chakula wakati mwingine ambavyo ni gharama na siyo wote wanaoweza kuvimudu.

Tafuta taasisi ya karibu na unapoishi lakini pia si lazima kujitolea kwa mahudhurio ya kila siku; unaweza kuomba kuhudhuria mara mbili tu kwa wiki na kwa saa chache kama inawezekana.

Tafuta suluhu ya matatizo ya kitaasisi

John ni muhitimu wa Shahada ya Technolojia ya Mawasiliano (IT), baada ya kuona kigezo cha uzoefu kimekuwa kikwazo kwake kupata ajira, anaamua kufanya utafiti mdogo kujua matatizo ambayo taasisi anazozifahamu zinapitia, lakini zinaweza kutatuliwa na ujuzi wa IT alioanao.

Moja ya mambo anayongua ni changamoto ambayo wazazi wanapata katika kufuatilia maendeleo ya kitaaluma ya watoto wao wanapokuwa shuleni kwa sababu kuu mbili.

Moja, umbali hasa kwa wazazi wenye watoto wanaosoma shule za bweni na pili, wanafunzi kutokuwa waaminifu hasa wale wenye maaendeleo yasiyo ya kuridhisha darasani.

John anaamua kutengeneza tovuti ya mfano na kuweka mfumo wa taarifa ambao kila mwanafunzi anaweza kusajiliwa na hivyo mzazi wa mtoto husika kupewa nywila ambayo itamuwezesha kuona maendeleo ya kitaluma ya mtoto wake.

Kupitia mfumo huo kila matokeo ya mwanafunzi yanapopakiwa, mzazi anaweza kuyaona matokeo kupitia kompyuta, simu au kifaa wezeshi chochote cha kielektroniki.

Baada ya kufanya hivyo, anapita kwenye uongozi wa shule mbali mbali kuliuza wazo lake.

Kwa kufanya hivi, John anakuwa na fursa ya kuuza huo mfumo kwa shule mbalimbali lakini pia kuuza uwezo wake ambao utafifisha umuhimu wa kigezo cha uzoefu wa kufanya kazi na taasisi nyingine.

Hii ni njia inayoweza kutumiwa na vijana wenye kujiamini na uwezo wa kufanya jambo ambalo linaweza kutatua changamoto mbalimbali za taasisi na kuongeza ufanisi au utendaji wa taasisi husika.

Hii itathibitisha kuwa unauwezo wa kutatua changamoto za taasisi na kufanya kazi na taasisi husika bila kigezo cha umeshafanya kazi na nani kabla.

Jenga mtandao wa kiajira

Njia ya kusubiri matangazo ya kazi ili uombe kazi imeshapitwa na wakati. Matangazo hayatoki kila siku, lakini watu wanaajiriwa kila siku.

Unadhani hawa wanaajiriwa vipi bila kazi kutangazwa? Kwa kifupi ni kuwa, kazi hutolewa kwa kujuana na hili si jambo la ajabu kwani watu hutoa ajira kwa wale wanaofahamu uwezo wao na kuwaamini.

Usikae ndani na vyeti na wasifu wako ukisubiri kazi itangazwe. Toka nje jenga urafiki na watu wenye ushawishi kwenye kutoa ajira, lakini pia wenye taarifa sahihi za masuala ya ajira na kazi.

Ukikutana na watu wa aina hii jitambulishe, chukua mawasiliano yao na hakikisha wanajua sifa zako na uhitaji wa ajira.

Watu wa namna hii wapo sehemu nyingi sana. Kanisani au msikitini kwako, kuna mkurugenzi wa kampuni fulani, kwenye vyombo vya usafiri unakutana na mameneja wa kampuni na wamiliki wa biashara mbalimbali, hizo ni fursa za kuwaunganisha kwenye mtandao wako wa kiajira.

Jenga mazoea nao ya kiuweledi na hakikisha unawatafuta mara kwa mara na hata kuomba kuwatembelea kwenye sehemu zao za kazi au biashara kama inawezekana.

Watu wenye uthubutu ndiyo wenye uwezo wa kutumia fursa mbalimbali, kuwa mthubutu mwenye ujasiri wa kufungua milango ya fursa na siyo kulalamika.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe anapatikana kwa 0659 08 18 38, [email protected], www.kelvinmwita.com