Binti yako kama hana elimu asikanyage Daslama

Muktasari:

  • Kupitia yeye ungeweza kuamini hili, kwamba hata majina yetu wazazi walitupatia kutokana na mazingira ya eneo husika. Na mazingira tunayoishi baadaye yanaanza kutulazimisha tujibatize upya majina na kuyatupa kapuni ya awali. Mabinti wanaongoza kwenye jambo hili. Betina ni mmojawapo.

Dar es Salaam. Ngozi halisi ikaanza kuonekana. Kumbe hakuwa mweusi tii bali ni rangi ya chokoleti. Maji ya chumvi, vipodozi, misosi flani, sabuni na mafuta anayopaka. Kombinesheni yote hii ilizalisha kiumbe tofauti na kile kilichokulia Itigi. Alikuwa na haki ya kuanza kujiita Tyner badala ya Betina.

Kupitia yeye ungeweza kuamini hili, kwamba hata majina yetu wazazi walitupatia kutokana na mazingira ya eneo husika. Na mazingira tunayoishi baadaye yanaanza kutulazimisha tujibatize upya majina na kuyatupa kapuni ya awali. Mabinti wanaongoza kwenye jambo hili. Betina ni mmojawapo.

Hakurudi Singida, akafuate nini? Mwili wake ulikuwa na thamani ya shoo kadhaa za Konde Boy. Sura yake ingewalazimu ‘panya rodi’ waokoke papohapo bila kusubiri neno la Mwakasege wala Kimaro wa Kijitonyama. Mzuri mpaka uzuri wenyewe uliona wivu juu ya uzuri wake. Kisu kwelikweli.

Anarudije Manyoni? Akafanye nini na punda za Itigi? Amwachie nani bata za viwanja vya Daslama mjini? Ndio kwanza alianza kuonja ladha ya utamu wa jiji hili. Rafikie aliyeishi Sinza, aliyeanza kujitegemea baada ya kupita njia alizopitia yeye. Akampokea, akamhifadhi, wakaishi.

Geto lenye kila kitu ndani kinachotakiwa kwa mtoto wa kike wa mjini. Maana kuna mtoto wa kike na mtoto wa kike wa mjini. Kilivutia kuliko sura na shepu za mastaa wengi wa Bongo Movie. Kuna vyumba vya watoto wa kike vina urembo kuliko warembo wenyewe. Ndo hiki alichohifadhiwa.

Kila kitu cha thamani ndani. Kuanzia runinga, ‘wolipepa’ (ukutani), kitanda, sofa, redio, kapeti, kabati la nguo, ‘dressing tebo’, jiko la pleti nne. Ungeenda bafuni ungekutana na sabuni za kweli, vibikini na vibraa vitamu vikiwa vimetundikwa na kuleta mvuto wa kipekee wenye upekee.

Ndo yale mageto ya watoto wa kike, ambayo mwanaume unajikuta bwege tu. Utampa nini sasa labda figo. Na hiyo figo uwe nayo sasa, figo za masela wengi zimechakaa kama ardhi ya pale Jangwani wakati wa masika. Imechakazwa kwa sumu zote unazojua wewe hapa duniani.

Haya yote yanakuja baada ya Tyner, kufukuzwa nyumbani kwa dada yake, (siyo tumbo moja ila wanatoka sehemu moja Singida). Ambaye alimleta Daslama kumsaidia shughuli zake za saluni. Haukupita mwaka kabla ya kuanza kuraruana kwa sababu za kipuuzi, ‘Mabwana’.

Aliingia Dar kama msichana wa kawaida sana. Mitoko na pamba alizoiga kutoka kwa wateja wa saluni ya dada, ghafla akawa kiumbe pendwa. Wateja wa saluni wakageuka mawakala wa mwili wake, aliuzwa kama mwanasoka na huduma yake ilikuwa siyo ya nchi hii. Kila pedeshee akataka kummiliki.

Akaanza kutishia himaya ya mwenyeji wake (dada mtu). Hakujiona tena kama mfanyakazi wa saluni. Kwani usiku mmoja aliingiza pesa nyingi kuliko faida ya saluni ya dada kwa wiki nzima. Ilikuwa rahisi Konde Boy kurudi WCB kuliko Tyner kuendelea kuishi kwa dada. Ndipo akatimuliwa usiku usiku.

Mwanamke aliyempokea Sinza ni miongoni mwa wateja wa saluni ya dada yake, ambaye pia alishiriki sana kumnadi Tyner kwa wanaume. Mrembo ni rahisi kumjua mrembo mwenzake. Akampokea kwa bashasha la kike akijua sasa atavuna pesa za ukuwadi kwa uhuru zaidi.

Ungewatembelea mchana muda wote wamelala, sura zimekunjamana kwa ukosefu wa usingizi. Nyakati za jioni wakijipara, ukiwaona utashangaa na matajiri wote hapa mjini wamekosaje kuolewa? Okay sawa waoaji hawapo na ‘mabarazameni’ wanaozalisha kina Tanasha hawawaoni kina Tyner?

Mwaka mmoja baada ya Tyner kulainika zaidi ngozi na kuongeza vifurushi vya bando kwenye umbile. Sasa alikuwa Tyner hasa, mashosti walimchukia kwa wivu. Hakujali, kwani alikuwa na marafiki wengi wa kiume kuliko wa kike na hao ndio aliowahitaji. Utamueleza nini?

Alizidi kuvutia zaidi, Sinza nako hakudumu baada ya kukosana na mwenyeji kwa sababu zilezile. Wivu juu yake. Daslama ilijenga undugu na mwili wake haikutaka aondoke. Rafiki yake mmoja wa Mbezi, akijua umbo la Tyner lingempa bata zaidi, alimkaribisha kwake haraka sana.

Mabwana walikuwa wengi kuliko nywele zake, wa kila rika, rangi na utaifa. Hakujua kumkataa mtu mwenye kipaji na nyota ya pesa. Ni miongoni mwa wasichana wa mjini waanzilishi wa msemo wa “Kudanga”. Alikuwa anadanga mpaka shetani mwenyewe anaogopa na kumkana waziwazi.

Kiwanja gani Tyner ungemkosa? Anakunywa ‘pii tuu’ kila siku kama karogwa. Ni dhahiri kwamba Tyner siyo mtumiaji wa zana. Mtoto mzuri, mbichi, laini laini anahusudu ‘drai chama kituo’, yaani ganda la ndizi ‘pyuuu mpaka maka’. Ndo maisha yake kwa miaka mingi sasa.

Rafiki yake wa Mbezi naye walizinguana akasepa. Sasa hivi maisha yake ni kambi popote. Anaishi kwenye nyumba za wageni ‘gesti’, anazolipa kila siku kwa kutegemea pesa za udangaji. Kuanzia Sinza mpaka Kisenvule, hakuna ‘gesti’ asiyoijua.

Ni zaidi ya kudanga. Kila siku anaamka giza likiingia na kuanza kukusanya hesabu zake kama bodaboda, mwanga ukichomoza asubuhi yeye ndipo analala. Kihalisia Tyner anaishi kwa ratiba ya Marekani akiwa mitaa hii hii ya Jiji la Chalamila. Watu tunalala yeye anaamka, tukiamka yeye analala.

Anaishi maisha ya ajabu sana. Utu umemtoka moyoni, hana staha ya kike wala adabu ya mama yake. Anakula baa, anashinda baa hana hata ujuzi wa kuchemsha chai. Siyo ‘waifu matirio’ tena bali ni ‘waifu masalia’. Maisha yake yameharibika.

Mzazi wa mikoani usiruhusu mtoto wako asiyekuwa na mbele wala nyuma kielimu akaja Daslama mjini. Asilimia kubwa ya mabinti zetu wamegeuka kuwa watumwa wa biashara haramu ya ngono. Wanatumikishwa kama taksi za mitandaoni. Watu ‘wanarikwesti’ tu inauma sana.