Profesa Anangisye: UDSM hatutoi digrii kama njugu

Watu wa Tanganyika ndiyo wenye kiu na njaa ya elimu. Elimu ni ufunguo wa maendeleo ya maisha ya watu katika nchi hii. Kwa maendeleo ya Taifa lazima watu wawe na elimu, ujuzi na maarifa.”

Kauli hii ilitolewa mwaka 1958 na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha Tanu, Amos Kasenge wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho ambapo kati ya mengi yaliyojadiliwa suala elimu lilichukua nafasi kubwa.

Hapa ndipo lilipoanzia wazo la kuwa na chuo kikuu cha Tanganyika na kwa pamoja kwenye mkutano huo, wajumbe walikubaliana kuwa chuo hicho kisihusishe siasa, hivyo kila mmoja achangie kufanikisha lengo hilo.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tanu, Julius Nyerere naye akafanya kazi kubwa ya kuhamasisha watu wachangie jitihada za kuanzishwa kwa chuo hicho, ili kuepuka kutegemea vyuo vya nje.

Kazi ya kukusanya fedha ilifanyika na mwaka 1961 wazo hilo likatekelezwa kwa vitendo hatimaye chuo kikuu cha kwanza nchini kilianzishwa Oktoba 25.

Imepita miaka 61 sasa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho ambacho sasa kinafahamika kama chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kikiwa miongoni mwa taasisi za elimu ya juu ambazo zimetengeneza na zinaendelea kutengeneza wataalamu waliobeba katika nyanya mbalimbali.

Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Anangisye anayeeleza mambo mbalimbali kuhusu taasisi hiyo kongwe ya elimu ya juu nchini, mchango wake kwa Taifa katika kuzalisha wataalamu na mtazamo wake kuhusu elimu ya juu kwa ujumla.

Swali: Miaka 61 ya uhai wa chuo kikuu nini mnajivunia?

Jibu: Tangu mwaka 1961 hadi sasa ni mengi ambayo chuo hiki tunaweza kujivunia; kwanza chuo kilianzishwa kwa ajili ya kuwapa elimu watoto wa Tanganyika jambo ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Kupitia chuo hiki wametengenezwa watalaamu na wanataaluma ambao wamewezesha kuanzishwa kwa vyuo vingine na kutoa huduma katika nyanja mbalimbali.

Swali: Upi mchango wa UDSM katika maendeleo ya nchi?

Jibu: Mchango wa chuo hiki si haba, kwanza kimehusika kutoa vijana wa Kitanzania ambao wameenda kuwa viongozi katika ngazi mbalimbali na kutoa mchango kwa Taifa. Viongozi wengi wa kitaifa wamesoma katika chuo hiki na wote tunajua mchango wa viongozi wakuu katika nchi.

Mbali na hao, vijana waliopita hapa wamewezesha utekelezaji wa miradi mikubwa na hadi sasa wengine wapo huko wanaendelea kulitumikia Taifa.

Chuo pia kimekuwa kikifanya tafiti ambazo zinatatua matatizo yanayoikabili jamii ya Kitanzania. Wanazuoni wetu wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanasaidia jamii kupitia tafiti za kitaaluma wanazofanya.

Pia unapozungumzia sera za uchumi katika Taifa, kwa kiasi kikubwa vijana wetu kutoka shule kuu ya uchumi wamekuwa na mchango mkubwa katika eneo hilo.

Swali: Zamani UDSM ilisifika kwa midahalo na mijadala ya wazi, kuna mpango wa kurudisha mijadala hiyo?

Jibu: Midahalo na mijadala ndiyo uhai wa chuo kikuu chochote, kwa hapa UDSM hakuna mwaka unapita bila kuwa na mdahalo. Huu ndiyo uhai wa taasisi yoyote inayoitwa chuo kikuu na tumekuwa tukihamasisha iwepo, lakini kitaalamu huwezi kufanya mdahalo kama hujafanya utafiti. Katika hili tumejipanga kwa kuongeza bajeti katika tafiti na ubunifu ikiwa ni pamoja na kuwajengea walimu wetu uwezo wa kufanya tafiti ambazo zitawezesha kuwa na mijadala yenye afya.

Hata hivyo, midahalo haijasimama bado ipo kwenye ndaki na idara inafanyika na chuo kimekuwa kikitengeneza mazingira mazuri ya kuifanya.

Swali: Kuna changamoto ya upungufu wahadhiri katika vyuo vikuu, hali ikoje UDSM?

Jibu: Ni kweli changamoto hii ipo, lakini sio kiasi cha kushindwa mambo kwenda. Hii taasisi ipo chini ya Serikali na haiwezi kukaa kimya kuona kuna kitu kinaathiri mchakato wa kuelimisha Taifa. Uongozi uliopo madarakani unajitahidi kuhakikisha changamoto zinazokwamisha taasisi hii ya elimu zinatatuliwa.

Pale tunapoona kuna upungufu tunatumia part time lecturers (wahadhiri wa muda) wenye sifa, lakini Serikali iko mstari wa mbele kuhakikisha tunapata walimu. Hivi karibuni walitupa watu 220 katika vitengo mbalimbali.

Changamoto nyingine ni kwamba mwanataaluma hadi abobee ni muda mrefu na kisera, digrii ya falsafa ndiyo ngazi ya chini ya kufundisha ingawa huwa tunawatumia pia wenye shahada ya pili.

Swali: Nini mtazamo wako kuhusu mwenendo wa sasa wa vyuo vikuu kufungua matawi, je hilo lina afya kitaaluma?

Jibu: Tunafungua matawi kwa sababu ya uhitaji, Tanzania ina watu wengi na vyuo vipo vichache ndiyo maana inatumika hii njia ya kufungua matawi nikitolea mfano UDSM ndiyo chuo kikubwa. Ukilinganisha na nchi jirani watu waliopo kwenye vyuo vikuu hapa nchini bado idadi yao ni ndogo, hivyo kuna uhitaji mkubwa wa kuwa na vyuo zaidi. Tunaanzisha matawi kwa lengo la kuwafikia watu huko waliko, mfano kwa sasa tuna mpango wa kuanzisha tawi Lindi litakalohusika na kilimo na usalama wa chakula. Elimu ni haki ya kila mtu, hivyo hakuna tatizo kwa vyuo kuanzisha matawi kuwafuata watu huko waliko.

Swali: Kuna madai ya baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu ukanda wa Afrika Mashariki kutokidhi mahitaji ya soko la ajira kutokana na kukosa ujuzi na maarifa, unazungumziaje hili hasa kwa wahitimu wa chuo chako?

Jibu: Siwezi kuzungumzia vyuo vingine ila ninachoweza kusema sisi tunajitahidi kuhakikisha kwamba wahitimu wetu ni wa viwango vinavyokidhi soko la Tanzania, Afrika Mashariki, Afrika na dunia. Hata hivyo inawezekana unapowaandaa vijana si wote wanaweza kuiva sawa, ila tunajitahidi kutoa wahitimu ambao wanakidhi viwango vya soko lakini hatupuuzii maoni ya watu.

Kila baada ya miaka mitano tunafanya mapitio ya mitalaa yetu kwa kwenda kwa wadau kupata maoni yao kujua ni ujuzi gani unahitajika hasa kwenye soko la ajira.

Hata hivyo, hatufikirii ajira pekee tunawaandaa wahitimu wetu waweze kujiajiri na wao kutoa ajira. Sisi hatupo kutoa digrii kama njugu ila tuna walimu waliobobea wanaoweza kutengeneza vijana walioiva kwenye ujuzi; tunasimamia viwango kuhakikisha vijana wanaotoka hapa wanakidhi vigezo vya soko.

Swali: Kumekuwapo na mjadala kuhusu lugha ya Kiswahili kutumika kama lugha ya kufundishia, kwa hoja kwamba wanafunzi wafundishwe kwa lugha wanayoielewa. Nini maoni yako katika hilo?

Jibu: Lugha ni kitu muhimu, wanaweza kuwepo wenye changamoto hiyo lakini hata hao waliofanikiwa si wamepita kwenye mfumo huo. Ninachoona labda Serikali iweke msingi mzuri kwenye lugha zote na hili lianzie ngazi ya chini kabisa. Tutengeneze mazingira ambayo yatafanya watoto wa Kitanzania wabobee kwenye lugha zote, lugha ni kitu muhimu na maoni yangu tuwekeze kwenye lugha zote.

Swali: Changamoto zipi zinakikabili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam?

Jibu: Sisi ni chuo kikongwe hatuwezi kukaa chini kuzungumzia changamoto inapotokea kuna changamoto kwetu tunaichukulia kama fursa na kwa watu tulionao na uzoefu wao bila kusahau ubobezi wao kitaaluma, tunazipatia ufumbuzi. Ufumbuzi huo unaweza kuwa na manufaa sio kwa chuo chetu hata taasisi nyingine zinaweza kutumia.