Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dawa la anguko ufaulu wa hisabati

Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania (Chahita), Betinasia Manyama.

Katika kila wanafunzi 10 wa sekondari waliofanya mtihani wa hesabu kwa kipindi cha miaka mitano, ni wawili pekee ndiyo waliofaulu.

Hii ni sawa na kusema ni asilimia 20 pekee ya wanafunzi wa sekondari wanaofanya mtihani wa hesabu wanafaulu, huku asilimia 80 wakifeli.

Kwa mujibu wa Chama cha Hisabati Tanzania (Chahita), mrundikano wa vipindi bila walimu wa kutosha wa hesabu na adhabu kali kutoka kwa baadhi ya walimu wa masomo hayo, ni miongoni mwa sababu za ufaulu duni.

Lakini, ufaulu duni wa somo la hisabati ni kitendawili cha muda mrefu kilichokosa jawabu, huku kila siku zikiibuka sababu mpya za hali hiyo.

Anguko la ufaulu katika somo hilo, ndiyo sababu ya kuonekana haja ya kuundwa kwa Chahita mwaka 1966, kikilenga kujua mzizi wa changamoto hiyo.

Katika mahojiano yake na gazeti hili, Mwenyekiti wa Chahita, Betinasia Manyama anasema mrundikano wa wanafunzi darasani na unaosababisha mzigo kwa walimu wa somo hilo, ni miongoni mwa mzizi wa tatizo.

“Idadi ya vipindi inakuwa kubwa zaidi na mwalimu anashindwa kumudu kuwafundisha wanafunzi wote somo la hisabati kwa makini zaidi,” alisema.

Uchache wa walimu ni changamoto nyingine iliyotajwa na Betinasia kuwa sababu ya ufaulu duni wa wanafunzi, akifafanua wengi wamestaafu na waliopo aghalabu huhamishwa vituo vya kazi.

"Tunaomba Serikali ituangalie kwa jicho la pekee, tupo wachache na tunaelemewa tunaomba tuongezewe walimu. Imekuwa changamoto na tunashindwa kutoa hata motisha kwa wanafunzi kutokana na uchache uliopo," anasema.

Ombi lake hilo, aliliambatanisha na haja ya kutolewa motisha kwa walimu wa hisabati ikiwemo kuongezewa posho na mishahara ili kuwapa hamasa.

“Unakuta mwalimu mmoja ana vipindi 30 huku kwa walimu wa masomo mengine wana vipindi hadi nane,” anasema.

Anguko la wanafunzi katika somo hilo, wakati mwingine Betinasia anasema linachagizwa na ukali wa baadhi ya walimu wa hisabati, ambao aghalabu huingia darasani na rundo la viboko.

"Tunaomba walimu wa somo la hisabati wapunguze tabia ya ukali na kuingia na viboko darasani. Hii inawachanganya wanafunzi tujitahidi kuongeza bidii na mbinu katika ufundishaji,” anasema.

Kwa mujibu wa Betinasia, wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha kuwawezesha walimu kutembelea shule mbalimbali kuwahamasisha wanafunzi kupenda somo hilo.

Lakini, hata yakiandaliwa mafunzo na Chahita, anasema walimu wanaohudhuria ni wachache.

Baada ya chama hicho kuanzishwa, anasema mikakati iliwekwa ikiwemo kuanzisha semina kwa walimu inayofanyika mara moja kila mwaka ili kuwapa mbinu bora za ufundishaji.

Pamoja na mbinu bora za kufundishia, uwezo wa kufanya utafiti ni jambo lingine alilosema linafanywa katika semina hizo kwa walimu.

"Kupitia semina hizo tumekuwa tukiwandaa walimu katika kufanya tafiti mbalimbali darasani pamoja na kuziandika ili somo la hesabu liendelee,” anasema.

Katika utekelezaji wa majukumu yake, anasema chama hicho kwa sasa kimeshatembelea shule zaidi ya 20 ili kuhamasisha wanafunzi kupenda somo hilo.

"Walimu wanajitolea kwa nauli zao kwenda kuhamasisha katika baadhi ya shule kuhusu somo la hisabati na tayari tuna shule zaidi ya 20 tumeshazitembelea,” alisema.
Ushirikiano na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kufanya tafiti za kubaini changamoto ni miongoni mwa mafanikio ya chama hicho.

Katika maelezo yake hayo, Betinasia anasema kuna umuhimu wa mwanafunzi kujua hesabu kwa kuwa ndiyo msingi bora wa maisha, akisistiza kwenye kila eneo inatumika.
 

Maboresho ya mitalaa

Kuhusu maboresho ya sera na mitalaa yanayoendelea, anaeleza kukoshwa na mwendelezo wa kulifanya somo la hesabu kuwa la lazima.

"Mitalaa inayoandaliwa ni mizuri hivyo tunaomba wanaosimamia waweke mikakati mizuri. Pia wazingatie uwepo wa vifaa vya kutosha katika kufundishia hususani vitendea kazi kwa ujumla,” anasema.
Anasisitiza uwiano wa walimu wa hesabu na wanafunzi uzingatiwe ili kupunguza mzigo kwa wataalamu hao.

"Unakuta kwenye shule za halmashauri nyingi walimu ni wachache, lakini wanafunzi ni wengi sana. Kwa mfano, unakuta mwalimu wa Kiswahili ana vipindi nane tu huku wa hesabu akiwa na vipindi 30.

“Ni vigumu sana kwa mwalimu huyu kumudu hilo, tunaomba Serikali iongeze miundombinu rafiki kwa walimu wa somo la hisabati ili wafanye vizuri zaidi," anasema.
 

Wasemavyo wadau

Kuimarishwa kwa klabu za hisabati ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa kuleta ahueni ya changamoto kama inavyoelezwa na Ofisa elimu sekondari mkoa wa Arusha, Abel Ntupwa.

Pamoja na uimarishwaji wa klabu hizo, Ntupwa anawataka walimu hao kuacha kujilimbikizia mikopo kutoka taasisi mbalimbali, kwa kuwa inawasababishia msongo wa mawazo na kupunguza maarifa.

“Mikopo hii inapunguza maarifa, kwa sababu mnaingia darasani mkiwa na mawazo, hii inawasababisha mshindwe kushirikiana vema na wanafunzi,” anasema.
Mabadiliko ya mtazamo wa walimu kutoka kufundisha kwa mazoea hadi kubuni mbinu mpya, anayataja kuwa mwarobaini mwingine utakaoongeza ufaulu wa somo hilo.

"Nawaombeni sana muwe na ujasiri na kuthubutu, tumieni ndoto mlizonazo ili tuwe msaada kwa jamii, familia na nchi kwa ujumla na tuhakikishe tunaacha tabia za kufedhehesha somo la hisabati, bali tutafute namna ya kutoka ili chama hiki kiwe mfano wa kuigwa," anasema.

Katika maelezo yake, anairejea hoja ya Betinasia ya kuongeza fedha kwa ajili ya walimu wa somo la hisabati, kwa kuwa wanafanya kazi inayohitaji motisha ili kuwaongezea ari.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dk Cairo Mwaitete anasema fani ya hesabu ni muhimu kwenye kila idara kwani inatumika kila mahali.

Anasema hata wahasibu hutumia hesabu katika shughuli zao, hivyo ni muhimu kutoa motisha kwa wanafunzi kulipenda somo hilo kwa kuwa lina soko pana la ajira.
"Sisi chuo cha uhasibu fani zetu tunazingatia mahesabu zaidi, ni vizuri tukatambua kuwa hesabu ni msingi wa maendeleo kwa faida ya nchi yetu na ni somo linalopaswa kuzingatiwa kuanzia shule za msingi hadi vyuoni," anasema.