Faida, hasara za kukacha kidato cha tano

Unaweza kusema ni mtazamo upya uliowakumba baadhi ya wazazi na wanafunzi. Hata hivyo, hali hiyo unaweza kuliita kama wimbi linalotishia mfumo wa elimu nchini.

Ni wimbi la wanafunzi kukacha masomo ya kidato cha tano na sita na kukimbilia vyuoni kusoma elimu ya ngazi ya diploma. Wimbi hilo linaonekana kuwasomba wanafunzi wengi wakiwamo wanaofanya vizuri na wenye sifa ya kusoma kidato cha tano.

Hata hivyo ni wimbi lililowagawa wadau wa elimu hasa kwa kuzingatia faida na hasara za kusoma ngazi hizo za elimu.

 Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema wanafunzi wengi wanaochagua utaratibu wa kukacha kidato cha tano, wanatafuta njia za mkato kufikia katika fani wanazozitaka, huku wengine wakisema ni hofu ya kufeli kutokana na masomo ya kidato cha tano na sita kuonekana kuwa magumu kuliko ya vyuoni.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema sababu kubwa ya wazazi kuamua mwanafunzi aende chuoni badala ya kidato cha tano, ni ugumu wa ajira uliopo nchini.

Anasema mtu anaenda kusoma miaka miwili kidato cha tano na sita halafu miaka mitano shahada halafu anakosa ajira. Anaona afadhali aende chuoni.

“Sasa hivi hakuna ajira kwa fani zote, hakuna uhakika kwamba akimaliza masomo yake ataajiriwa. Mtu anaona anapoteza muda baadaye hakuna ajira. Anaona bora aende chuoni, kwani kuna uwezekano wa kupata ajira ama kujiajiri mwenyewe kwa sababu tayari anakuwa amepata ujuzi,”anasema.

Dk Loisulie anasema vyuo vya kati vinalenga kumuandaa mtu kujiajiri ama kuajiriwa, kwa sababu vinafundisha kivitendo zaidi tofauti na vyuo vikuu ambavyo vinaandaa watu kuwa maofisa.

Anasema kijana anapokuwa amesoma hadi ngazi ya diploma, suala la ajira sio gumu sana kama wale wenye shahada. Anasema mwenye diploma anaweza kufanya kazi hata ndogo kama vile kwenye hoteli.

Pia anasema wanafunzi hivi sasa wanamaliza wakiwa wadogo, hivyo wanapokwenda chuo kikuu, wanashindwa kuhimili vishindo vyake kwa sababu ya uhuru wanaoupata.

Hata hivyo anasema anasema kama mitalaa mipya iliyotungwa itasimamiwa vilivyo, inaweza kuwapatia ujuzi wanafunzi wakiwa sekondari hivyo wasilazimike kukimbilia vyuoni kama ilivyo sasa.

Kwa upande wake, mwalimu na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Jiji la Dodoma, Samson Mkotya anaunga mkono utaratibu wa Serikali kutaka watoto wanaofanya vizuri kwenda katika masomo ya kidato cha tano, kwa sababu elimu yake inamuuandaa mtoto na masomo ya shahada ya kwanza katika fani anazotaka.

“Sifahamu kwa nini baadhi ya wazazi wanapenda mtoto aende chuoni baada ya kutoka kidato cha nne, wanafikiria zaidi taaluma wala hawakosei lakini kwa msimamo wangu naunga mkono utaratibu wa Serikali kuwa mtoto mwenye sifa za kwenda kidato cha sita aende,”anasema.

Mwalimu wa sekondari jijini Dodoma, Betha Msihi anasema miongoni mwa faida ambazo anazipita mwanafunzi anayetoka kidato cha nne na kwenda chuo cha kada ya kati ni kupata taaluma na kuingia kazini mapema.

Anasema wengi hasa waliosomea masomo ya sayansi wanapenda kukimbilia vyuoni kutokana na ugumu wa masomo hayo na kuhofia kufeli katika mitihani ya kidato cha sita.

“Hii ni njia ya mkato kuliko aende miaka miwili kidato cha tano na sita, anautumia muda huo kwenda chuo kusoma diploma. Lakini pia anaweza kusomea ualimu katika baadhi ya vyuo,’’ anasema na kuongeza:

‘’Huwa mwaka mmoja mwanafunzi anasoma masomo ya kidato cha tano na sita na miwili inayofuata anasoma ualimu, hivyo anapata faida ya kusoma vyote kwa muda mfupi.’’

Hata hivyo, anasema kwa maoni yake ni vyema mwanafunzi aliyepata ufaulu mzuri kwenda katika mfumo uliowekwa na Serikali, kwa sababu siku za usoni kutakuwa na tofauti kati ya mwanafunzi aliyekwenda moja kwa moja chuoni na yule aliyepitia kidato cha tano na sita.

Anasema mwanafunzi aliyemaliza kidato cha sita angalau anakuwa amekua na hivyo anaweza kujisimamia akipewa fedha za matumizi na maisha kwa ujumla akiwa chuoni kuliko yule aliyemaliza kidato cha nne na kukimbilia chuo akiwa na umri mdogo.

Betha anasema hata kwenye wasifu kuna maeneo mengine waajiri wanauliza kuhusu cheti cha kidato cha sita, hivyo hali hiyo inaweza kumkwamisha anapofika wakati wa kutafuta kazi.

Mdau mwingine wa elimu, Dk Nderakindo Kessy anasema ukimaliza kidato cha sita bila ya kufanya vizuri kwenye mitihani ni sawa na kumaliza kidato cha nne kwa sababu itakulazimu kwenda katika vyuo vya fani mbalimbali.

Anasema mwanafunzi anapokwenda moja kwa moja chuoni akitokea kidato cha nne, anakuwa amemtangulia aliyekwenda kidato cha tano na kufeli kwa miaka miwili.

Anasema zipo sababu nyingi za wanafunzi kuchagua kwenda vyuoni badala ya masomo ya kidato cha tano na cha sita, ikiwamo mchepuo aliopangiwa na mazingira ya shule aliyopangiwa kwenda kusoma.

“Akiangalia mazingira ya shule aliyopangiwa kwenda kidato cha tano, anajiuliza ni kweli anaweza kusoma vizuri na kupata ufaulu utakaomwezesha kwenda chuoni?”anasema.

Dk Kessy anasema pia mzazi anafikiri mtoto wake akienda chuoni atamaliza baada ya miaka mitatu na kupata taaluma yake, lakini huyu anayeenda kidato cha tano akimaliza atahitajika kutafuta fedha za kumlipia chuo kikuu.

Anazitaja faida za kwenda chuoni mara baada ya kumaliza kidato cha nne ni kuingia katika fani mapema, ataanza kufanya kazi na hata kama kwa kujitolea anaweza kufanya kwa mshahara mdogo tofauti na yule aliyesoma kidato cha tano na sita kwanza.

‘’Pia akiamua kwenda chuo kikuu kuchukua masomo ya shahada, aliyemaliza kidato cha nne na kwenda chuo anakuwa na elimu zaidi ya fani anayokwenda kusoma kuliko yule aliyekwenda chuo kikuu kutokea kidato cha sita,’’ anaeleza.

Hata hivyo, anasema hasara za kwenda chuo kwa aliyemaliza kidato cha nne , inaweza kuwa mwanafunzi alifanya uchaguzi wa haraka pasipo kuzingatia kama fani hiyo ndiyo anayoitaka maishani mwake.

Anasema hasara nyingine ni ngumu kwenda kusoma shahada ya pili kwa yule aliyemaliza kidato cha nne, kwa sababu historia yake ya masomo inakuwa dhaifu, ukilinganisha na yule aliyetoka kidato cha sita.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John cha jijini Dodoma, Dk Shadidu Ndossa, anasema wanafunzi wengi humaliza masomo ya kidato cha nne wakiwa wadogo hivyo kwenda kidato cha tano na cha sita, kunawapa nafasi ya kukua.

“Sekondari bado kuna uangalizi zaidi wa walimu na wazazi, kwa hiyo kuna faida kubwa ya mwanafunzi anayeenda kidato cha tano kukua zaidi,”anasema.

Anatoa mfano wa mtoto aliyeanza shule ya msingi akiwa na miaka mitano akimaliza masomo ya kidato cha nne atakuwa na miaka 17 tofauti na yule anayemaliza kidato cha sita atakuwa na miaka 19.

Anasema mwanafunzi aliye na umri wa 19, ni rahisi kumudu changamoto za chuoni za kujisimamia mwenyewe kimasomo na kimalezi tofauti na yule wa miaka 17.

“Kama kuna vishawishi chuoni mwanafunzi wa miaka 19 kidogo ana akili ya kuamua achague kipi kwa sababu anajua faida na hasara ya maamuzi yake tofauti na huyu mdogo sana,”anasema.

Kwa upande wa faida za kitaaluma, Dk Ndossa anasema mwanafunzi aliyemaliza kidato cha sita, anakuwa amekua kitaaluma na hivyo inampa uwezo wa kujiangalia mwenyewe kimasomo na iwapo amefaulu vizuri anakuwa na wigo mpana wa kuchagua fani anayotaka kwenda kusomea.

Dk Ndossa anashauri wanafunzi wamalize masomo ya kidato cha sita halafu waende vyuoni.