Mipango ya elimu bila kumkumbuka mwalimu sawa na kutwanga maji kinuni

Mwalimu akifundisha darasani. Je mipango ya Serikali inaikumbuka kada hii muhimu kwenye elimu?

Muktasari:

Katika siku za karibuni, mojawapo ya mipango iliyoanzishwa na Serikali ni mabadiliko ya mitalaa.Ni kwa kiwango gani walimu walishirikishwa na hata kuwezeshwa?

Dar es Salaam. Mwalimu ni rasilimali muhimu katika uboreshaji wa elimu nchini.

Hata hivyo, mchango wake katika kusukuma gurudumu la elimu mbele haujatiliwa maanani inavyostahili,

Kinyume chake siasa inaonekana kushika kasi katika utetezi wa mdomoni, pasipo mipango thabiti ya kuboresha maslahi ya watendaji hawa muhimu.

Kama ambavyo mwenye nyumba hupaswa kumjali na kumpa stahiki zake fundi mwashi ili jengo lake lipendeze, ndivyo inavyopaswa Serikali iwekeze kwa walimu.

Ukiwekeza kwa walimu, hata mipango ya elimu kama mtalaa mpya, tahasusi mpya na mifumo mipya ya utathmini, itatekelezwa ipasavyo.

Bila kumjali mwalimu, elimu inaelekea kutengeneza migomo baridi kwa watoa huduma hawa. Ni bora mgomo ulio wazi kuliko ule wa kufanya kazi bora liende.

Walimu wanaweza kuwa na maandalio ya somo, shajara, zana za kufundishia na vitendea kazi vyote vinavyokaguliwa na wathibiti ubora, lakini bado wasifundishe ipasavyo kwa sababu ya kukosa ari.

Hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Charles Msonde, alikiri wazi jinsi ambavyo maslahi ya walimu yanachezewa kwenye kila halmashauri.

Akizungumza na watendaji wa elimu katika kikao kazi wilayani Karagwe na Misenye, mkoani Kagera, Dk Msonde alisema mara nyingi fedha za likizo za walimu hutengwa Aprili kwa wanaoomba likizo Juni na Oktoba kwa wanaoomba likizo Desemba.

Hata hivyo, walimu wanakwenda likizo bila kulipwa stahiki zao kwa mujibu wa taratibu. Alibainisha kuwa fedha za likizo zinapocheleweshwa, kuna mchezo unaofanywa na watendaji kuhamisha fedha kwa kufanya kazi nyingine.

Kilio cha walimu

Hii inaonesha kwamba hali si shwari katika kutimiza matakwa ya walimu. Walimu wamekuwa na malalamiko mengi, huku wakidharauliwa kwa kulipwa mishahara kiduchu, ilhali Serikali ikikanusha kauli hii kwa kusema ni idara inayolipwa mishahara mikubwa.

Kanusho la Serikali ni kejeli kwa sababu kila mtu anafahamu mazingira ya kazi ya walimu nchini. Walimu wametuhumiwa mara kadhaa kuingia kwenye mikopo umiza, wana madeni lukuki, hawapati posho za kazi ya ziada, na wanalala kwenye mabweni kama wanafunzi pindi wanaposhiriki usahihishaji wa mitihani ya kitaifa.

Dk Msonde, kama mwalimu mbobevu, amefanya kazi hii kwa miaka mingi na anajua udhaifu katika kada hii.

Ndio maana alibainisha kwenye kikao kazi kuwa walimu wanapaswa kufuata ngazi stahiki wanapodai haki zao, huku akiwashangaa walimu kwa nini hawawezi kuhakikisha wanafunzi wa kidato cha kwanza kwenye shule za umma wanalimudu somo la Kiingereza

“Naomba walimu ‘wenzangu’ mfuate taratibu. Kama hoja yako haijatatuliwa na mkuu wa shule, ipeleke kwa mratibu elimu kata ambaye ataiwasilisha kwa afisa elimu wa wilaya. Si busara kupiga simu na kutuma barua pepe moja kwa moja kwa katibu mkuu,” alisema Dk Msonde.

Kauli ya Dk. Msonde inaweza kutafsiriwa kama 'mikwara' ya kuwataka walimu wawe wanyonge wanapodai haki zao.

Badala ya kuwakatisha tamaa, angewatumia walimu hao wenye malalamiko kama intelijensia imara ya kusambaza taarifa za uozo unaofanywa ngazi za chini.

Walimu wanalalamikia kutopandishwa madaraja kwa uwiano sawia. Walimu walimwambia Dk Msonde kuwa wanaweza kuwa wamemaliza chuo na kuanza kazi kwa mwaka mmoja wakiwa watendaji mahiri wenye ngazi sawa ya elimu, mmoja akapande cheo na mwingine akazidi kugugumia maumivu kwa miaka kadhaa bila kutambuliwa.

Walimu wa Kagera walisema vigezo vya kupanda madaraja haviko bayana kulingana na elimu ya mwalimu, huku wanaojiendeleza wakilalamika kwa kutobadilishiwa muundo baada ya kujiongezea elimu, tena kwa gharama zao.

“Nilipandishwa daraja mwaka juzi lakini mshahara bado nalipwa wa zamani. Nina cheo lakini hakiakisi maslahi ninayopewa na Serikali. Naambiwa nidai kila siku nipo kiguu na njia halmashauri na barua zangu nyingi zipo kwa katibu mkuu,” alisema mwalimu mmoja kwa masharti ya kutotajwa jina lake.

Mwaka 2019, Serikali ya Tanzania ilikiri kuwa walimu walikuwa wanadai zaidi ya Sh43 bilioni yakiwamo malimbikizo ya mishahara na likizo.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara, alisema kuwa Serikali ina nia nzuri kuhakikisha inalipa walimu kwa wakati.

Hata hivyo, wapo walimu 86,000 ambao wanaidai Serikali zaidi ya Sh43 bilioni.Wakati hali ikiwa tete, aliyekuwa Waziri wa Tamisemi, Angellah Kairuki, aliwaonya viongozi wanaoomba fedha walimu ili washughulikie madai yao.

Kwa muktadha huu, hatuwezi kupiga hatua kama Taifa tukiimba nyimbo za kuboresha elimu kwa kuanzisha mitalaa mipya, huku mafundi wetu ambao ni walimu wakipigwa danadana na mikwara mizito. Tunapaswa kuimarisha mfumo mzima wa elimu kwa kuhakikisha walimu wanapewa stahiki zao na kuheshimiwa ili waweze kutoa huduma bora kwa vizazi vijavyo.

Tuige wengine

Nchi zilizoendelea kama Finland, Ujerumani, Australia, na Japani zinatilia maanani sana walimu wao, jambo ambalo limechangia sana mafanikio yao katika sekta ya elimu.

Katika nchi hizi, walimu wanaheshimiwa na kuthaminiwa kama sehemu muhimu ya jamii, hali ambayo imejenga mazingira bora ya kazi na motisha kwa walimu kutoa elimu bora.

Finland, kwa mfano, ina mfumo wa elimu unaotambulika kimataifa kwa ubora wake. Walimu nchini humo hupitia mafunzo ya kiwango cha juu na wanapewa uhuru mkubwa katika kufundisha.

Hii inasaidia kuendeleza ubunifu na ubora katika ufundishaji. Ujerumani nayo inawekeza sana katika mafunzo na maendeleo ya kitaaluma ya walimu, ikihakikisha kuwa wana vifaa na rasilimali zote muhimu zinazowawezesha kufanya kazi yao kwa ufanisi.

Kwa Tanzania, ni muhimu kuiga mifano hii kwa kuhakikisha walimu wanapewa heshima na stahiki zao kama inavyostahili. Tanzania inapaswa kuwekeza katika mafunzo ya kitaaluma ya walimu, kuboresha mazingira yao ya kazi, na kutoa motisha zinazohitajika.