RIPOTI MAALUMU: Mbumbumbu waongezeka nchini

Ripoti ya utafiti wa ufuatiliaji wa kaya (NPS) ya mwaka 2020/2021 inaonyesha kuwa asilimia 76.0 ya Watanzania wote kwa ujumla ndiyo wanaojua kusoma na kuandika.

Takwimu hizi zinatoa tafsiri kuwa asilimia 24 iliyosalia ya Watanzania wote hawajui kusoma na kuandika.

Idadi hii ni ishara hasi katika kufikia malengo ya maendeleo kwa kuwa ili Taifa liendelee, ni muhimu liwe na watu wengi walioelimika na wenye stadi muhimu maishani zikiwamo za kusoma, kuandika na kuhesabu.

Ripoti hiyo inafafanua zaidi kuwa kati ya hao wasiojua kusoma na kuandika, wengi ni wanawake (wakiwa asilimia.. na wanapatikana hasa vijijini na maeneo ya pembezoni ya miji. Hili linatokana na ukweli kwamba watu waishio miji mikubwa kwa kawaida wapo karibu na huduma za elimu, hivyo ni rahisi kwao kuzifikia kuliko ilivyo kwa waliopo vijijini.

Wakati tathmini hiyo inafanyika wakazi wa Dar es Salaam walikuwa na viwango vya juu vya kusoma na kuandika, ambapo takriban asilimia 94 walikuwa na uwezo wa kusoma na kuandika, wakati wale wa Vijijini walikuwa na viwango vya chini zaidi (asilimia 69.7).

Kwa kulinganisha viwango vya kujua kusoma na kuandika kati ya ripoti za NPS za 2014/15 na 2020/21, idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika iliongezeka kwa kiasi kikubwa katika maeneo yote ya kijiografia kwa wanaume na wanawake ikilinganishwa na miaka sita iliyopita ambapo asilimia 30.2 ya watu wote walikuwa hawajui kusoma na kuandika.

Ripoti inaonyesha kiwango cha kusoma na kuandika kati ya miaka hiyo 6-12 ni asilimia 68.0, wakati kiwango cha kusoma na kuandika kwa watoto wa miaka 7-13 ni asilimia 77.2.

Hii ina maanisha kwamba idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika kwa walio na umri wa miaka saba hadi 13 ni kubwa kuliko ile ya watu wote (asilimia 76.0).


Hali ilivyo kwa vijana

Kwa upande wa vijana takwimu kiwango cha wanaojua kujua kusoma na kuandika ni asilimia 87.3, wanaume ikiwa asilimia 88.6 na wanawake asilimia 84.5.

Ingawa viwango vya watu wazima kusoma na kuandika pia ni chini mno kuliko viwango vya kusoma na kuandika kwa vijana, viwango vya kusoma na kuandika kwa wanaume watu wazima bado viko juu zaidi kuliko vile vya wanawake watu wazima.

Licha ya tofauti za jinsia, matokeo yanaonyesha kuwa kiwango cha kujua kusoma na kuandika kwa vijana wa kiume na wa kike kiliongezeka kati ya NPS 2014/15 na NPS 2020/21, pamoja na watu wazima wa kiume na wa kike.

Viwango vya kujua kusoma na kuandika kwa vijana vilikaribia asilimia 100 katika Jiji la Dar es Salaam mwaka 2020/21 kutoka asilimia 96 mwaka 2014/15), huku idadi ya vijana wanaojua kusoma na kuandika katika maeneo ya Vijijini Tanzania Bara, watu wasiojua kusoma na kuandika – iliongezeka kutoka asilimia 78.8 hadi asilimia 83.7.

Hii ina maana kwamba kuna asilimia 16.3 ya vijana waishio vijini na maeneo ya pembezoni hawajui kusoma wala kuandika.

Takwimu hizi zinatuonyesha katika karne hii ya 21 bado kuna Watanzania hawajafikiwa na huduma za elimu au wanakwepa au wapo katika mazingira yanayowafanya wasione umuhimu wa elimu

Dk Faraja Kristomus

Wasemavyo wachambuzi

Kutokana na takwimu hizi, baadhi ya wachambuzi wanasema bado kazi kubwa inatakiwa kufanyika ili kukidhi viwango vya taifa linaloendelea.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Faraja Kristomus anasema kipimo cha taifa linaloendelea ni kuwa na watu wenye uwezo wa kusoma na kuandika ili washiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo.

Anasema endapo kiwango cha ujinga kitakuwa kwa kiasi kikubwa, ni ishara kwamba watu wachache watashiriki kwenye shughuli za maendeleo na ukuzaji wa uchumi.

“Takwimu hizi zinatuonyesha kwamba katika karne hii ya 21 bado kuna Watanzania hawajafikiwa na huduma za elimu au wanakwepa au wapo katika mazingira yanayowafanya wasione umuhimu wa elimu na kujikita kwenye shughuli nyingine.

“Kuna yale maeneo ya wafugaji, migodi, uvuvi bado kuna watu hawaendi shule, wamekuwa wakiamini katika shughuli hizo kuliko elimu na hata wanapopelekwa kwa lazima, wanaacha sasa hawa ni vigumu kuwatoa kwenye ujinga,”anasema.

Hata hivyo, mhadhiri huyo anasema hali inaweza kuwa nafuu zaidi baada ya Serikali kuanza utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo inayowafanya wazazi wengi kuhamasika kupeleka watoto shuleni.

Anasema upo uwezekano idadi kubwa ya wasiojua kusoma na kuandika, ni zao la kabla ya utekelezaji wa sera hiyo ambapo wengi walikosa elimu kwa kushindwa kumudu gharama za ada, kutoona umuhimu wa elimu na sababu nyingine nyingi.

“Wanawake wanaonekana waathirika wakubwa katika hili kutokana na maeneo; kuna tamaduni ambazo ziliamini kwamba mtoto wa kike hakustahili elimu. Zipo jamii ambazo mtoto wa kike anapozaliwa tayari anaandaliwa kuwa mke na mama wa familia na hawa watu tunao kwenye jamii, ndiyo sababu nasema inaweza kuwa pia ni zao la kabla ya kuwepo kwa hamasa kwenye suala zima la elimu,”.

Kwa upande wake, mwalimu na mtunzi wa vitabu, Richard Mabala anasema hilo linachangiwa na hali ilivyo kwenye shule nyingi za msingi ambapo kuna idadi kubwa ya wanafunzi kwenye darasa moja, jambo linaloleta ugumu kwa mwalimu kuwafikia wote.

Anasema: “Darasa likiwa na wanafunzi wengi ni vigumu mwalimu kuwafikia wote, hapa sasa upo uwezekano mkubwa wengine wakawa hawajui kusoma wala kuandika. Halafu kwenye ufundishaji kuna wale wanafunzi wanaoelewa kwa haraka na wale wazito sasa hawa wanahitaji ufuatiliaji wa karibu na hili haliwezi kufanyika kama mwalimu ana wanafunzi wengi.

Katika dunia ya leo mtu asiyejua kusoma na kuandika lazima atakwama, hivyo mfumo wetu wa elimu unapaswa kutambua watu hawa wako wapi na kuweka mkakati maalum wa kuwanasua kwenye changamoto hiyo,”anaeleza.

Akizungumzia athari za taifa kuwa na idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma na kuandika mkurugenzi mstaafu wa shirika la Uwezo Tanzania na mdau wa elimu, Zaida Mgala anasema ni kikwazo katika mapambano ya kukuza uchumi na kuishi kwenye dunia ya utandawazi.

Anasema kusoma na kuandika ni stadi ya msingi katika maendeleo ya watu na nchi hivyo hakuna shughuli inayoweza kufanyika kwa ufanisi bila kujua kusoma na kuandika.

“Kama tuna watu wengi wa aina hii ni kwamba nchi haifikii malengo yake kwenye elimu kama ilivyojiwekea. Maana hapa kuna ambao hawajawahi kabisa kwenda shule na kuna walioenda wakakatiza masomo au kumaliza wakiwa hawajui kusoma wala kuandika,’’ anasema.

Anaongeza: “Kwa dunia ya sasa hata kilimo kinahitaji uwe unajua kusoma na kuandika, maana kuna pembejeo sasa utazitumiaje kama hujui kusoma , hufuatilii taarifa, haya tuje kwenye afya kama mtu hajui kusoma anaweza kutumia vibaya dawa. Ameenda hospitali ameandikiwa dawa kwa ajili yake au mtoto kwa sababu hajui kusoma anaweza kutumia tofauti na ikaleta madhara.

“Harakati za nchi kuleta maendeleo kupitia viwanda ni lazima watu wajue kusoma, maana huko viwandani kuna mashine, mitambo, kemikali kama hujui kusoma unaweza kujikuta unapata madhila. Kujua kusoma kunamfanya mtu kupata taarifa.’


Tufanyeje?

Mdau wa elimu Dk Avemaria Semakafu anasema ili kupunguza au kumaliza idadi ya watu wasiojua kusoma, tayari Serikali imeshaonyesha njia kinachotakiwa ni usimamizi na kila mmoja kutimiza wajibu wake.

“Hivi karibuni imefanyika sensa na wamefikiwa watu wa makundi yote, kama ambavyo imewezekana kuwafuata huko na taarifa zilichukuliwa, basi ihakikishwe kwamba wote ambao hawajui kusoma wanaunganishwa kwenye programu zitakazowasaidia.

“Sera na sheria ya sasa hapa Tanzania inataka kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule awe shuleni kinyume na hapo hatua za kisheria zichukuliwe kwa mzazi wa mtoto ambaye yupo nje ya mfumo elimu,” anasema Dk Aveline na kuongeza:

“Hili suala la anuani za makazi nalo litarahisisha kuwafikia watu wa kundi hili, kwahiyo ninavyoona njia tayari ipo na hatua tayari zimechuliwa na Serikali kinachotakiwa sasa ni kila mmoja kutimiza wajibu wake.’’

Naye mwalimu mstaafu, Bakari Kheri anasema kama iliwezekana kuwa na mkakati miaka ya nyuma, hakuna kinachoshindikana sasa kubuni mkakati wa kukuza usomaji.


Mbumbumbu sekondari

Mwaka 2012, iliyokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ilibaini kuwapo kwa wanafunzi 5,200 walioingia sekondari wakiwa hawajui kusoma na kuandika.

Uzoefu unaonyesha kuwa wanafunzi wengi wanakosa msingi wa masomo hayo tangu wakiwa elimu ya awali na madarasa ya mwanzo ya elimu ya msingi (darasa la kwanza hadi la tatu).

Kwa uzoefu huu na kinachotokea sasa shule za msingi kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya elimu, ni dhahiri kuwa kama uchunguzi wa kina utafanyika, upo uwezekano mkubwa wa shule za sekondari kuwa na wanafunzi wasio na uwezo wa kusoma wala kuandika.