Sababu, athari kupotea kwa uandishi wa barua

Mmoja ya watumiaji wa huduma za posta akitoa barua katika sanduku lake. Picha na Maktaba

Mwaka jana, rafiki yangu Hanifa Kafashe alipata msiba wa mtoto wake aliyefariki kwa ajali ya gari.

Ndugu, jamaa na marafiki tulimiminika nyumbani kwake kumhani na kumfariji kwa nasaha na dua.

Mmoja kati ya marafiki waliosafiri hadi msibani ni Nalozi Chipeta (maarufu Chichi), aliyetumia siku nzima kuzungumza na mfiwa pamoja na kumliwaza.

Siku iliyofuata, wakati akiondoka msibani na kurejea nyumbani kwake, Nalozi alimkabidhi mfiwa barua ya pole na faraja aliyomwandikia kwa mkono.

Kama unajiuliza, ni kwa nini aliamua kumwandikia barua na ilhali amefika msibani na kuzungumza naye ana kwa ana, yumkini nawe ni miongoni mwa maelfu ya watu wasiojua. Kipi hicho?

 Ni “uchawi wa barua” katika kuwafariji wenye huzuni, kuwaliwaza wenye simanzi, na hata kulainisha nyoyo za tuliowakosea.

Katika kadhia hii, unadhani mfiwa atamkumbuka nani zaidi baina ya wale waliomwandikia arafa (ujumbe) kwenye simu na huyu aliyemwandikia barua kwa mkono? Jibu unalo!


Kwa nini barua?

Uandishi wa barua ni moja kati ya njia bora zaidi za kuwasilisha fikra na hisia kwa mlengwa.

Hii ni kwa sababu, unapoandika barua unapata wasaa wa kutosha kutafakari kwa hisia na kukumbuka kwa kituo kila ulichokusudia kukitia kwenye maandishi.

Hilo la kwanza. La pili, anayepokea barua si tu anapata wasaa wa kuusoma ujumbe uliomkusudia, bali pia anapata kuzihisi na kuzitafakari hisia za aliyemwandikia.

Tukio hilo la Nalozi kwa Hanifa, likanikumbusha siku moja nilipokuwa mdogo kiumri, tuliletewa taarifa nyumbani na jirani yetu aliyekuwa akimiliki simu ya mezani, kuwa mjomba wangu, Rashid Kassa aliyekuwa kwenye mafunzo ya uaskari huko Kiwira, Mbeya, amepiga simu akitaka kuzungumza nasi.

Wakati huo hapakuwa na simu za mkononi. Pasi na kufanya ajizi, mama yangu mzazi pamoja na mama yangu mdogo, walitoka ili kuwahi simu hiyo. Nami nikawafuata. Haikuchukua muda tangu tulipofika nyumbani kwa jirani, simu ikaita mezani.

Mama zangu wakawa wanapokezana mkonga wa simu kwa raha zao, wakipiga “stori” na mdogo wao. Nami pia nilipewa kuzungumza naye.

Ilikuwa ni simu kwa ajili ya kujuliana hali na kujuzana habari. Baada ya kuhitimisha mazungumzo kwa soga na michapo ya hapa na pale, mjomba Kassa akatujulisha kuwa siku hiyo atatuandikia barua na kuituma kwa njia ya posta. Mama zangu walionekana kufurahia zaidi kupokea barua, tofauti kabisa na mimi ambaye nilitamani kudadisi hiyo barua ni ya kazi gani ilhali tumekwisha kuzungumza naye kwa simu?

Kwa wakati ule sikuwa na maarifa ya kutosha kutambua kuwa, uandishi wa barua ni zaidi ya mawasiliano ya simu. Umri wangu ulikuwa mdogo kutambua kuwa barua ni zaidi ya mazungumzo ya ana kwa ana.

 Ni sanaa ambayo ikitumika vema hubeba hisia halisia, kwani anayeandika husukumwa na mguso wa ndani zaidi kutegemea na jambo analoandika na mtu anayemwandikia.

Hiyo ni kwa sababu anayeandika hupata muda wa kutosha kutafakari kabla ya kuandika kitu ambacho hakipatikani katika ujumbe wa simu.

Siku barua ya Kassa ilipowasili, nakumbuka familia nzima tulijumuika barazani ambapo bibi aliidhinisha bahasha ichanwe rasmi na barua isomwe.

 Huu ulikuwa ni utamaduni wa familia yetu kila tulipopokea barua ya kifamilia. Kimya kilitanda kadri barua ilivyokuwa ikisomwa kwa sauti.

 Hisia za mwandishi zilizobebwa na maneno aliyotumia, zilituchota sote kiasi kwamba tukajihisi tu-pamoja naye huko kambini.

Alituelezea hali ya baridi hapo kambini mpaka nilijihisi vinyweleo vikinitutumka. Alituelezea kuhusu mazoezi ya kukimbia na mabegi mazito mgongoni mpaka nilijihisi kifua kimenijaa upepo. Ilikuwa ni furaha kuliko mazungumzo tuliyofanya naye kwa simu.

Utamaduni huu ulitujenga hata sisi watoto kupenda kusoma na kuandika barua. Shuleni pia tulifunzwa namna ya kuandika barua mbalimbali kwa utaratibu na mtiririko rasmi.

Ilifikia hatua tukishindana kubuni maneno ya namna ya “kuanzia” au “kumalizia” barua.

Wakati huo kulikuwa na maneno fulani yaliyofanana karibu kwenye kila barua, kutegemea na aina ya barua.

Mathalani, kwenye barua za mapenzi, kulikuwa na maneno kama: “Kwako mpenzi.... Utakapo kujua hali yangu, mimi ni mzima bukheri wa afya. Hofu na mashaka ni juu yako wewe uliye mbali na upeo wa macho yangu.”

Aidha, katika umaliziaji wa barua hizo, kulikuwako maneno mashuhuri kama:

“Wasalam fulani bin fulani,” au “Ndimi fulani bin fulani,” au “Wakatabahu.”

Nakumbuka miaka hiyo kulikuwa na zile kalamu ambazo wino wake ukinukia marashi. Unayemwandikia barua akifungua bahasha anakumbana na harufu maridhawa. Pia, kulikuwa na kalamu za wino wa rangi mbalimbali. Tuliweza kuandika barua moja kwa rangi tofauti tofauti. Na kila rangi ilibeba ujumbe mahususi.

Hata barua zilizoandikwa kwa maadui zilikuwa na raha yake kiuandishi. Mfano, badala ya kuandika: “Ni matarajio yangu barua hii itakufikia ukiwa salama,” iliandikwa, “Ni matarajio yangu barua hii itakufikia kabla sijakufikia.”

Hata namna barua hizi zilivyohitimishwa zilijaa jeuri na vitisho. Kwa mfano, badala ya kumalizia kwa maneno kama: “Usisite kuwasiliana nami kama utahitaji ufafanuzi zaidi,” iliandikwa, “Nakutakia siku ngumu ya kujitafakari kabla ya ajali. Ni busara kwako kama utasita kuwasiliana nami kwa ajili ya ufafanuzi zaidi ya huu niliokutumia.”

Tofauti na simu au ujumbe wake, barua huandikwa kwa utulivu pasi na kuingiliwa kimawazo na yule unayemwandikia. Kitu ambacho humfanya anayeandika kutafakari kabla ya kuandika.

Hilo humfanya aliyeandikiwa naye kusoma mpaka mwisho bila kujibu. Ni kwa utulivu huo, ndiyo maana barua nyingi zilikuwa ni fupi na zenye kueleweka.

Kwa sababu ni katika kutafakari kwa kina ndipo mtu huweza kuchagua maneno machache na bado yakabeba masimulizi yenye ubora na msisimko maridhawa.

Mwanafalsafa Blaise Pascal aliwahi kuomba msamaha kwa kumwandikia rafiki yake barua ndefu sana, akisema, “Sikuwa na muda wa kuandika barua fupi.”


Athari ya teknolojia

Tangu kuenea kwa mawasiliano ya barua-pepe, ujumbe mfupi na hata simu za video, sanaa ya uandishi wa barua imekuwa ikiyeyuka mithili ya theluji juani. Cha ajabu, huko “duniani” ambako ukuaji wa teknolojia ni wa kasi zaidi kuliko huku kwetu, wao wanaendeleza sanaa hii pamoja na kubuni mbinu za kurithishana vizazi hadi vizazi.

Wenzetu wanatambua kuwa ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano haukuja ili kuutelekeza utamaduni huu wa kuandikiana barua.

Nchini Uingereza, imeasisiwa jumuiya ya kuthamini barua zilizoandikwa kwa mkono (The Handwritten Letter Appreciation), yenye makao makuu yake eneo la Swanage, Dorset.

Kama haitoshi, Septemba Mosi ya kila mwaka, huadhimishwa Siku ya Uandishi wa Barua Duniani, kwa minajili ya kuhanikiza watu kutenga muda wa kuandika barua.

Kwa hapa Tanzania, nalipa shumbe na kongole, Shirika la Posta Tanzania kwa kuendesha mashindano ya uandishi wa barua kwa watoto ili kutia msukumo wa kuhuisha sanaa hii inayopotea.

Shime kwenu wazazi popote mlipo, wajengeeni watoto ari ya kuandika barua. Itawasaidia kuboresha ujuzi wa uandishi na umahiri katika uchaguzi na mpangilio wa maneno.

 Itawasaidia kuboresha miandiko yao na kuwajengea hali ya kujiamini. Itawasaidia kuboresha uwezo wa ubongo katika kutafakari.

 Itawajengea mahaba baina yao na jamaa na marafiki kwa kuandikiana barua zitakazobeba kumbukumbu zenye hisia za ndani.

Hisia ambazo ni muhali kuzivumbua kwa kuandikiana ‘meseji’ za kawaida kwenye simu za mkononi. Kwa hakika ni raha sana kuandika barua, na ni furaha kuzisoma pia.

Maundu Mwingizi ni mwandishi wa riwaya na hadithi fupi kutoka Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (Uwaridi). Anapatikana katika mtandao wa X kwa @maundumwingizi