Teknolojia na changamoto za utoaji wa elimu vyuoni
Dar es Salaam. Tanzania inahitaji kutafakari upya nafasi na mfumo wa elimu ya vyuo vikuu, ikiwa inataka kuwapatia vijana ujuzi unaohitajika katika uchumi wa dunia unaobadilika kwa kasi.
Hiyo ni kauli aliyoitoa hivi karibuni, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) nchini Tanzania, Shigeki Komatsubara.
Akizungumza wakati wa warsha kuhusu mifumo ya umahiri na maendeleo ya mitalaa inayozingatia umahiri iliyofanyika katika Taasisi ya Tekolojia Dar es Salaam (DIT), alisema mifumo ya jadi ya elimu ya vyuo vikuu haina nafasi tena katika kipindi ambacho dunia inapitia mabadiliko makubwa ya kiteknolojia na kiuchumi.
Alisema kuibuka kwa bunifu za kiteknolojia kama Akili Unde, (AI), uchumi wa kidijitali pamoja na teknolojia za kijani kunabadilisha kwa kiasi kikubwa aina ya ajira duniani, hali inayozilazimisha taasisi za elimu kuondoka katika mfumo wa kufundisha nadharia pekee na kuelekeza nguvu zaidi katika utoaji wa ujuzi wa vitendo.
“Angalieni dunia ambayo vijana wanaingia. Akili Unde, uchumi wa kidijitali na teknolojia za kijani zinabadilisha hali ya mambo kwa kasi kubwa,” alisema.
Alieleza kuwa kazi nyingi ambazo wanafunzi wa leo watazifanya katika miaka ijayo huenda zisiwepo jambo linalofanya uwezo wa kuendana na mabadiliko, ubunifu pamoja na utatuzi wa changamoto kuwa muhimu zaidi.
“Hii ndiyo sababu tunapaswa kutafakari upya namna elimu ya vyuo vikuu inavyofanya kazi ili kuenzi maono ya kujitegemea katika karne ya 21,” alisema.
Wajibu wa vyuo vikuu
Komatsubara alisema vyuo vikuu havipaswi kuendelea kuzalisha wahitimu wenye vyeti vya kitaaluma pekee, bali pia watu wenye uwezo wa kuunda fursa, kuongoza jamii na kushughulikia changamoto tata za kijamii na kiuchumi.
“Tunahitaji mfumo wa elimu unaojenga wabunifu, watatuzi wa matatizo na watu wenye fikra pevu,” alisema.
Alihusisha mjadala huo na falsafa ya Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, akisema kuwa dhana ya Elimu ya Kujitegemea bado ina umuhimu mkubwa hata katika mazingira ya sasa ya dunia.
Akinukuu falsafa hiyo ya Nyerere, alisema elimu inapaswa kuwasaidia vijana kufikiri kwa kujitegemea, kufanya uamuzi na kuutekeleza kwa ufanisi.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa katika dunia ya sasa utekelezaji wa uamuzi huo, unahitaji umahiri wa kisasa pamoja na maarifa ya vitendo yanayokwenda sambamba na mahitaji ya soko la ajira.
Komatsubara pia aliipongeza DIT kwa kushiriki katika mpango wa kuendeleza mitalaa inayozingatia umahiri, akiitaja taasisi hiyo kuwa miongoni mwa vinara wa mageuzi ambayo yanaweza kuwa mfano kwa vyuo vingine nchini.
“Huu si waraka mwingine tu wa sera. Huu ni mwongozo wa namna taasisi zinaweza kuwaandaa vizuri zaidi wanafunzi kwa ajili ya siku zijazo,” alibainisha.
Akizungumza katika warsha hiyo, Naibu Mkuu wa DIT anayeshughulikia taaluma, utafiti na ushauri wa kitaalamu, Profesa Ezekiel Amri, alisema vyuo vikuu vinapaswa kuendelea kupitia mitalaa yake mara kwa mara, ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Alisema kuzalisha wahitimu wenye umahiri unaoendana na mahitaji ya ajira, si muhimu kwa taasisi za elimu pekee, bali pia kwa maendeleo mapana ya uchumi wa Taifa.
“Hatuwezi kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi bila kuendelea kuboresha mafunzo na umahiri,” alisema.
Kwa mujibu wa Profesa Amri, DIT imekuwa ikishirikisha wadau pamoja na waajiri katika mapitio ya mitalaa, ili kuhakikisha programu zinazotolewa zinaakisi hali halisi ya soko la ajira na matarajio ya sekta mbalimbali.
Alisema mafunzo yanayozingatia umahiri, husaidia taasisi kuwaandaa wahitimu wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya sehemu za kazi mara tu baada ya kuhitimu.
“Suala la kuwa na ujuzi sahihi si changamoto ya DIT pekee, bali ni ya Tanzania kwa ujumla,” alisema.