Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Verone Mankou: Mwafrika wa kwanza kubuni simu

kijana kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Verone  Mankou aliyetengeneza Simu na kulipa bara la Afrika heshima

Muktasari:

Mbio za ubunifu wake zilianza mwaka 2006. Akaanza na simu jamii ya android akaiita ‘Elikia’ baadaye akabuni kompyuta ndogo aliyoiita Way-C

Kila siku programu mbalimbali za simu za mkononi na kompyuta zimekuwa zikibuniwa. Kikubwa wabunifu hao wamekuwa wakitoka nchi zilizo nje ya bara la Afrika.

Lakini kijana kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Verone  Mankou (27), amelipa bara la Afrika sura mpya katika ulimwengu wa teknolojia za simu na kompyuta.

Naye amegundua programu zake za simu mithili ya ‘smartphone’ na kompyuta ndogo maarufu kwa jina la ‘tablet’Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa hivi karibuni na  BBC, vifaa hivyo vinaendeshwa kwa teknolojia ya Android ya Googles, na  vinazalishwa chini ya kampuni yake iitwayo  VMK.

Akizungumza katika mkutano wa teknolojia uliofanyika Afrika Kusini  (Tech4Africa), Mankou alisema ubunifu huo ni wa Waafrika kwani ndio wanaofahamu mahitaji ya bara lao.

"Apple ni kampuni kubwa Marekani, Samsung ni barani Asia,  na tunataka VMK kuwa kampuni kubwa barani Afrika,"alisema.

Simu hiyo aliyoibuni  ina kamera na skrini ya ukubwa wa inchi 3.5 sawa na sentimita 8.9. Anasema kuna mipango ya kuziuza simu hizo katika nchi kumi za Afrika Magharibi,  pamoja na Ubelgiji, Ufaransa na India.

Aidha, anasema anatarajia kuzindua uuzaji wa kompyuta za bei nafuu zaidi kwa wanafunzi mwaka ujao.

Kampuni ya VMK imesema kinyume na bidhaa nyingine za awali za simu na kompyuta zilizosemekana kuwa za Afrika, bidhaa za VMK hazifanani na bidhaa zozote za aina hiyo katika nchi nyingine.

Anasema kikubwa kilichomsukuma katika ubunifu huo ni kutaka kuona watu wengi wanapata huduma za intaneti, hivyo ilihitajika kupata kifaa kizuri kitakachopatikana kwa bei nzuri.

Mbio za kijana huyu zilianza mwaka 2006 ambapo alikuwa akitoa huduma za intaneti, mwaka mmoja baada ya  Steve Jobs kutoa simu yake ya muundo wa  iPhone, Mankou akaja na wazo la kubuni alichokiita Big iPhone, akimaanisha kuja na bidhaa zake zenye ubora kama Iphone).

Katika kufikia ndoto yake hiyo, alianza kwa kuunda simu ya kisasa (Android)  iliyokuwa inaitwa  Elikia neno lenye maana ya matumaini katika lugha ya Kilingala.

Aliendeleza mbio hizo mpaka Januari 2012  alipokuja na aina ndogo ya kompyuta (tablet)  aliyoiita   Way-C .

Wataalamu wa teknolojia wanasema kuwa, ingawa kifaa hicho kimebuniwa DRC na uzalishaji wake kufanyika China, hakufanyi bidhaa hiyo kutokuwa ya Kiafrika.

Wanasema lengo la kuzalisha bidhaa hiyo China ni kupunguza gharama na pia kunatokana na ukweli kuwa DRC haina viwanda vinavyoweza kufanya uzalishaji huo.

Wanasema  kampuni nyingi kama   Blackberry na  iPad ambazo ni za Marekani, bidhaa zake zinazalishwa China kutokana na urahisi wa rasilimaliwatu na wingi wa viwanda.

Mwanzoni kijana huyu alikuwa na wazo tu, lakini ili aweze kuzalisha vifaa hivyo nchini China,  zilihitajika dola za Marekani 375,000.

“Hii ilikuwa sehemu ngumu sana, nilitumia zaidi ya miaka miwili kukusanya fedha na kuliboresha wazo hili,” anasema Mankou.

Kutokana na uzuri wa wazo hilo Serikali ya DRC iliwekeza asilimia 50 ya fedha hizo, fedha nyingine alizipata kutoka kwa watu binafsi na wadau wengine.

“Siku zote naamini kuwa Afrika hakutakuwa wanunuaji milele, inatakiwa na sisi tuwe wauzaji, hii ndiyo imani iliyokuwa ikiniongoza tangu mwanzo.

Vijana inatakiwa wajue ugumu wa kufanya kazi, kupata fedha za mradi, kitu cha muhimu ni kuamini wazo lako na kupiga hatua ya kwanza kutoka ulipo,” anaeleza.

Mtaalamu wa Sayansi ya  Kompyuta na Mhadhiri wa Chuo cha Uongozi wa  Fedha Zanzibar, Mohamed Zahraan, anasema  teknolojia  inaweza kutokea popote duniani.

Hata hivyo,  anasema ili jambo kama hilo liweze kufanyika kwenye nchi kama Tanzania, lazima watunga sera wakubali kuangalia upya mitalaa ya elimu pamoja na kuweka mazingira ya kuwasaidia wanasayansi.

Anasema kuwa, kwa sasa kuna vyuo vingi vinavyofundisha mambo ya sayansi ya kompyuta,  lakini vijana wanatoka hapo bila kuiva.

“Lazima tuwajengee mazingira ya kuweza kutoa kile walichojifunza darasani mpaka kwenda kukifanyia kazi,” anasema.

Msemaji wa Tume ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH) Theophil Laurian anasema kuwa, tume hiyo kwa upande wake inajitahidi kuwapa vijana motisha ili waweze kufikia mafanikio kama ya kijana huyu.

“Hatujaweza kuwa na mafanikio kama ya kijana huyo wa Congo,  kwa sababu vijana wetu wengi bado hawajaona kuwa masomo ya sayansi yataweza kutatua matatizo yetu, wanaona ni kama masomo ya kawaida tu,” anasema.

Anasema  bajeti ya Wizara ya Mawasiliano sayansi na Teknolojia ya mwaka 2012/13,  ilitoa Sh80,000,000 kwa ajili ya shughuli za atamizi ya Tehama.

“Atamizi hiyo imeweza kuhudumia wajasiriamali ambao wameweza kuendeleza juhudi zao za ujasiriamali katika nyanja za Tehama,  ikiwa ni pamoja na kupatia ufumbuzi wa masuala ya ununuzi wa bidhaa kwa mtandao,” anasema.

Anasema pia kuwa Sh34,894,950 zimetumika kwa ajili ya kuwahudumia wagunduzi na wabunifu kwa kuwapatia tuzo na vitendea kazi ili kuboresha shughuli zao.
Historia ya ugunduzi wa simu za mkononi

Ni mawazo ya Samwel Morse, mawazo na ndoto zake zimekuwa ni nguzo kwenye mawasiliano ya simu.

Utakubaliana na mimi kwamba teknolojia inayoongoza kuliko zote kwenye upande wa mawasiliano ya kielektroniki,  ni teknolojia ya  simu za mkononi, pamoja na huduma nyingine zinazoitegemea.

Kwa hivyo utashangaa ni vipi tumetoka kwa Samwel Morse hadi hapa tulipo leo na tunapokwenda kesho.

Samwel Morse aliwekeza kwenye Telegraph, lakini historia yoyote ya simu za mkononi lazima ianzie  kwake.

Morse alivumbua  telegraph ya sumaku mwaka 1832,  na kuitengeneza kwa ajili ya mazoezi na majaribio mwaka 1835.

Mnamo Oktoba 18 mwaka 1842, Morse alitandaza waya umbali wa karibu maili mbili hivi.

Sehemu ya waya huo ilipita chini ya maji, kwa kuwa alitaka kuonyesha kuwa hata chini ya maji waya unaweza kusafirisha ishara (signals) , lakini kwa bahati mbaya kabla hajakamilisha zoezi lake meli ilipita    na kukata nyaya zake, na huo ukawa kama ni mwisho wa jaribio hilo.

Baada ya hapo kukatokea wazo la kutuma ujumbe na uwezekano wa kufanya hivyo ulianza kuonekana. Sasa ikajulikana kuwa maji yanaweza kuchukua umeme na kupeleka ujumbe, hivyo njia nyingine zikaanza kufikiriwa.

Mwaka 1843, mtaalamu na mchambuzi wa Kemia, Michael Faraday aliendesha utafiti wa kutaka kufahamu  kama uwazi  ungeweza kusafirisha umeme, kwa kutumia kanuni ambazo tayari ziliwekwa kwa ajili ya kuanzisha telegraph.

Mwaka 1864 James Clerk Maxwell alitoa makala yake "Dynamic Theory of Electromagnetic Fields" ambayo ilihitimisha kuwa mwanga, umeme, na usumaku vyote vina uhusiano,  vyote vinafanya kazi bega kwa bega, na "ellectromagnetic Phenomena" na zinasafiri kwa mawimbi.

Halafu mnamo mwaka 1865, Dk Mahlon Loonis wa Virginia, daktari wa meno, inasemekana alikuwa mtu wa kwanza kutumia wireless kwa mawasiliano kwenye anga.

Kati ya mwaka 1866 na 1873 alifanikiwa kutumia telegraph kwa umbali wa maili 18 kutoka Cohoction hadi Beorse Deer    Mountains huko Virginia.

Alianzisha njia ya kusafirisha na kupokea ujumbe kwa kutumia anga (Earth's Atmosphere ) kama Conductor. Miaka 30 iliyofuata, wawekezaji na wataalamu walitengeneza telegraph iliyounganishwa kwa waya.

Majaribio yaliendelea kwa mfumo wa kujaribu na kukosea pasipo kufanikiwa.

Kuzaliwa kwa simu ya mkononi
Akatokea jamaa mwingine kwa jina aliitwa Martin Cooper, maarufu kama ‘baba wa simu za mkononi’. 

Aliajiriwa na kampuni ya Motorola mwaka 1954, Bw. Cooper alifanya shughuli ya kubuni bidhaa rahisi,  ikiwa ni pamoja na redio ndogo ya mkononi ya polisi kwa ajili ya idara ya Polisi ya Chicago  mwaka 1967, na tena akaongoza utafiti wa simu za mkononi wa Motorola.

Mnamo Aprili 3 mwaka 1973,  Martin Cooper alipiga simu kwa kutumia simu ya mkononi kwa mara ya kwanza mbele ya umati, ikiwa kama maonyesho ya ugunduzi wa simu ya mkononi.