Mwanamke wa Kitanzania anaolewa na nani?

Mwanamke wa Tanzania anaolewa na nani? Linaweza kuwa swali lenye jawabu rahisi, kwa kuwa kila mmoja anafahamu ndoa inahusisha mwanamke na mwanamume, lakini uhalisia ni kinyume chake kwa familia nyingi nchini.

Licha ya ndoa kufungwa na mume na mke, mwenendo wa maisha ndani yake hutekelezwa na mwanamke kwa miongozo na usimamizi wa familia ya mume.

Kwa sababu ya utaratibu huo, mke analazimika kuishi kwa miongozo ya wakwe zake, lakini anawajibika kwa familia ya mumewe, jambo linalojenga swali kwamba mke wa Tanzania anaolewa na nani? Mume au familia ya mumewe.

Jawabu la swali hilo ni kile kinachofanywa na jamii mbalimbali nchini, likiwamo kabila la Wagogo kama inavyoelezwa na Chifu wa Wanyanzaga (Wagogo), Lazaro Chihoma.

Anasema mwanamke anayeolewa na mkubwa wa familia huwa na jukumu la kuihudumia yote, wakiwamo wadogo wa mumewe na ana nafasi finyu ya wao kuwajibika kwake.

Anasema ili kupima uwezo wa mwanamke kutunza familia na tabia ya uchoyo, hupewa mtoto wa kumlea.

“Siku anakabidhiwa jiko ilikuwa lazima na hata sasa unapewa mtoto wa kumlea ili familia ya mume wakuangalie kama una asili ya uchoyo au upendo, hicho ni kipimo kikubwa kumjua anaweza kutunza familia ya mume,” anasema Chifu Chihoma.

Ni aibu ya ukoo iwapo mwanamke anayeolewa na Wagogo akakosa mtoto, anafafanua zaidi hilo haijalishi mke au mume ndiye mwenye tatizo.

“Inakuwaje mume awe na tatizo la kukosa mtoto, wanaume hawakosagi watoto, ila huwa ni kwa mwanamke na huyo hatakuwa na sifa nzuri kwa ukoo alikoolewa, lakini aibu kwao,” anasema Elizabeth Nghungo (89), Mzee wa Kimila.

Anasema inapobainika mwanamume ndiye mwenye tatizo, unatengenezwa utaratibu wa siri wa kuruhusu mmoja wa ndugu wa mume kulala na shemeji yake, hilo hufanyika kwa ushirikiano wa wakwe.

Iwapo tatizo ni mke, Elizabeth anasema ukoo wake unalazimika kutoa binti mwingine, atakayelipiwa nusu mahari ya mke wa kwanza ili aolewe na mume huyo kuendeleza ukoo.

Anasema mbali na kutunza mashemeji wadogo na wakwe, mke huyo ataangaliwa kwa ukarimu wa wageni wanaofika kwao na kabla ya kupata watoto wa kuwazaa hawaruhusiwi kuishi mbali na wazazi.

Pia, anasema watoto wa kiume ni turufu katika jamii hiyo, ataheshimika zaidi mwanamke atakayezaa watoto wa jinsi hiyo ukilinganisha na nyingine.

Hata hivyo, mwanamke wa kabila hilo huwa hana haki ya kuchagua mumewe, bali ukoo wenye nguvu ya kulima na uwezo wa chakula ndiyo hupendekezwa zaidi.

Si Wagogo pekee, wenyeji wa Kilimanjaro wanazo taratibu zao pia. Mwenyekiti wa Machifu Wilaya ya Same, Ruben Mnyuku anasema mzigo wa lawama utamshukia mwanamke iwapo atachelewa kupata mtoto.

“Inapotokea mwanamke amechelewa kupata mtoto, lawama nyingi hurudi kwa mwanamke na vijijini hakuna mwamko wa kwenda hospitali kubaini mwenye tatizo, baadhi ya wanawake hunyanyasika na mume ataoa mke wa pili kwa lengo la kupata watoto,” anasema Mnyuku.

Chifu wa Wazanaki, Japhet Wanzagi anasema mwanamke ndiye mwenye jukumu la kuhudumia watoto, mume, ndugu, jamaa na hata wageni wanaotembelea familia.

“Kuunganisha familia kwa kuwajali, kuwalinda na kuwahudumia watu wote kuanzia wazazi na ndugu wa mume, majirani na wote wanaohusiana na familia aliyoolewa.

“Kwa kifupi mwanamke akiolewa anakuwa mke wa jamii kwa maana kuwa ustawi au kusinyaa kwa familia na jamii katika nyanja zote iko mikononi mwake, akishindwa kutekeleza wajibu huo ni mgogoro unaoweza kusababisha hata ndoa kuvunjika,” anasema kiongozi huyo wa kimila.

Chifu wa Wasukuma kutoka Koo ya Bahindi, Aron Mikomangwa anasema pamoja na kuzaa, kulea watoto na kuendeleza familia, mwanamke wa jamii hiyo ana wajibu wa kuhakikisha familia inakuwa na chakula cha kutosha.

“Japo wanawake wanashiriki katika suala la kilimo, lakini jukumu kubwa la kilimo liko kwa wanaume wanaotakiwa kulima na kuvuna mazao ya kutosha mahitaji ya familia, huku mwanamke akisaliwa na kazi ya kupika chakula cha kutosha,” anasema.

Mzee Zakaria Chibuga kutoka Jamii ya Wakara wanaopatikana Kisiwa cha Ukara, Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, anasema wajibu wa mwanamke katika jamii hiyo ni kuzaa, kulea watoto, kutunza na kuendeleza familia, ukoo na jamii.

“Wanawake pia wanao wajibu wa kusimamia shughuli zote za uzalishaji katika jamii, kuunganisha familia na jamii, kupokea na kuhudumia wageni pamoja na kulisha familia kwa kupika chakula cha kutosha,” anasema Chibuga.

Majukumu ya mwanamke katika Jamii ya Waluo wanaopatikana Wilaya ya Rorya mkoani Mara hayatofautiani na wenzao wa makabila mengine ya kanda ya ziwa kama anavyosema Stephen Omolo.

Anasema kuzaa, kulea na kuendeleza familia ni moja ya majukumu ya msingi kwa mwanamke aliyeolewa.

“Kazi ya kupika chakula, kutunza wageni, kuunganisha familia, ukoo na jamii ni majukumu mengine muhimu ya mwanamke katika jamii yetu,” anasema mzee Omolo.


Viongozi wa dini

Askofu Mstaafu wa Kanisa la TAG, Glorious Shoo anasema katika maisha ya ndoa, mke anapaswa kumhudumia mumewe na watoto, huku mume akihakikisha ustawi wao.

“Lakini ndoa inapofungwa, matokeo ya kwanza yanayotarajiwa ni mama kupata mtoto, lakini ukweli kutopata mtoto kunaweza kusababishwa na mambo mengi na sababu zinaweza kusababishwa na mke au mume, hivyo si vizuri watu wakakubali kupata presha au kugombana, wanapaswa kuwa wamoja na kwa sasa wanaweza kuasili mtoto na kuwalea na kuwafanya wakwao,” anasema.

Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga anasema ndoa ni ya watu wawili, yaani mke na mume.

Anasema katika ndoa haina maana anayeolewa au kuoa anakwenda kuwa mtumwa wa familia ya mwenza wake, badala yake wawili hao ndiyo wanaohusika.

“Kijana anapooa haimaanishi wazazi wameletewa mtumwa nyumbani na hata aliyeoa hakuoa mtumwa wa familia, amemchukua mwenzake ili waongeze kizazi,” anasema Askofu Munga.

Askofu Munga anasema changamoto inayozikabili tamaduni nyingi nchini ni kutokubali ndoa ya watu wawili pekee, akisisitiza iwapo kutatokea haja ya kutoa msaada kwa familia itafanyika hivyo kwa makubaliano ya pamoja.

Anasema kwa upande mwingine ndoa inaunganisha ndugu kati ya familia moja na nyingine, huku akisisitiza kuwa hicho kisiwe kigezo cha mmojawapo kutumika kama mtumwa.


Wanasaikolojia, haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Chama cha Wanasaikolojia Tanzania (Tapa), Magolanga Shagembe anasema ndoa ni jambo la wawili waliokubaliana kuishi pamoja kwa vigezo walivyopimana navyo.

Anasema ili kuwe na ustawi wa ndoa kunahitajika wawili hao ndio wawe mstari wa mbele kushughulikia na kusimamia mambo yao.

“Ikitokea mtu wa tatu ana nguvu zaidi kuliko wawili hao, kuna hatari ya ndoa hiyo kuingia kwenye migogoro ya mara kwa mara au kuvunjika,” anasema Shagembe, ambaye pia ni Mhadhiri wa Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Anasema wawili wanapofunga ndoa hujipima kwa vigezo vyao, mtu wa tatu hushauri nje ya vigezo hivyo.

Kinachosababisha familia ya mume kuwa na nguvu katika ndoa, anataja ni kukumbatiwa kwa mila na desturi za kale.

“Wakati huo mke alikuwa anajadiliwa na familia nzima ndiyo apitishwe hadi kuolewa, lakini sasa vijana wanakutana kwenye utafutaji wanapendana wanafunga ndoa, ukiruhusu mtu wa familia ashauri ilhali hajui vigezo mlivyopendeana atavuruga,” anasema Shagembe.


Watoa ushuhuda

Margareth Haule, mama wa watoto wawili, anasema kuwa aliachika kwa sababu ya ndugu wa mumewe.

“Tulikutana chuoni Iringa, mimi nikitoka Songea na yeye akitokea Mwanza, kama utani tulianzisha urafiki na baadaye akanipelekwa kwao, pamoja na vipingamizi vya hapa na pale tulifunga ndoa,” anasema Margareth, aliyedumu kwenye ndoa kwa miaka mitatu.

“Kosa la kwanza nilitangulia kupata kazi, tena Shinyanga wakati huo tukiwa tunaishi Mwanza tukifanya biashara baada ya kumaliza chuo, huku kila mmoja akiwa ameomba kazi sehemu mbalimbali.

“Maneno yalianza kuwa mke hawezi kukaa mbali na mume na sina nidhamu, mama mkwe akaumwa akaletwa kwangu nikatakiwa niache kazi nimuuguze kwa sababu ni jukumu langu la msingi.”

Margareth anasema alichukua likizo ya siku 28 na kumuuguza mkwe, hata alipopata nafuu hakutakiwa kuondoka akae ili amfunze adabu. “Hapo tulikuwa na kibanda cha kuishi tayari na mtoto mmoja, mume wangu hakuwa na sauti ya kutetea kibarua changu, bahati nzuri na yeye akapata kazi Dar es Salaam, alipoondoka mama akarudi Mwanza, lakini tayari sikuwa na sifa ya kuwa mke.

“Nikiwa kazini akaja shemeji yangu mkubwa kuliko mimi, eti amekuja kuishi na mimi na nimtafutie kitu cha kufanya, hapo nina mimba ya mtoto wa pili, nilipokataa kwa sababu sikuona umuhimu wa kufanya hivyo, mume wangu naye alikasirika na hatukuelewana hadi tukaachana.”

Naye Suzan Mwasha anasema kuwa watu wanashindwa kutofautisha maisha ya zamani na vijana wa sasa.

Anasema akiwa kazini alikutana na kijana kutoka mkoani Singida, walipendana na wakati wa likizo akampeleka kwao kwa lengo la kumtambulisha.

“Ukumbuke nimesoma shula ya bweni, sijawahi kupika ugali hata wa watu watano, kwetu tulikuwa wachache na kulikuwa na vitu vingi vya kurahisisha kazi (mashine), kipimo cha kwanza nilitakiwa kupika ugali wa watu wasiopungua 12,” anasema Mwasha.

“Nilikataa, nikasema bora lawama kuliko fedheha, kwa sababu usingeiva na nisingeweza kukaa kwenye kibanda na kilichojaa moshi nikipika, naamini ningekulia kule na mimi ningezoea kama wao, lakini sijawahi hata siku moja, nilijilaumu na kulaumu wazazi wangu kwa nini hawakunifundisha ila kila nikiangalia pale nyumbani kile kibanda kingekaa wapi, sioni.

“Nahisi mpenzi wangu alisemwa na wao kwao, kwani waliponipa jukumu la kusaga karanga kwa mkono kwenye jiwe pia nilishindwa, walichoka hawakunisema vibaya, ila tuliporudi kazini sikuona tena zile mishemishe za kuoana na mimi nikaelewa kuwa sitowezana naye kutokana na taratibu zao kwao, niliumia ila nilisonga mbele,” anasema Suzan, mwenyeji wa Kilimanjaro.

Anasema haamini katika mwanamke kutotimiza majukumu yake, lakini maisha ya siku hizi yana tofauti sana, wazee, wazazi, walezi wanapaswa waliangalie hilo na wasikatishe safari salama za vijana wao kwa vigezo vya maisha ya zamani.

“Mimi nililetewa mgonjwa wa kuuguza, sikuwa na kazi na mume wangu alikuwa na pesa, hivyo haikuwa shida ila sikuwa na utaalamu wa kujikinga, nikamwita mtaalamu ili atupe elimu wachache pale nyumbani tunaomuuguza mgonjwa wa namna sahihi ya kumkinga na kujikinga.

“Kosa kubwa nililofanya ni kumwita mtaalamu na kuvaa soksi za mikono ninapomuogesha mgonjwa, nikaambiwa ninamnyanyapaa, suala lilikuwa kubwa kiasi cha mgonjwa kujaribu kujiua kwa maelezo ninamnyanyapaa haoni sababu ya kuishi, mambo yalikuwa mengi hadi tukatengana,” anasema Ruwahida Makame.

Akilizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga anautaja mfumo dume kuwa mzizi wa tatizo hilo.

Anasema mfumo huo unaufanya upande wa mwanamume kuonekana na nguvu zaidi ya mwanamke, hivyo anapoolewa anaishi kwa miongozo yao.

“Hata akizaliwa mtoto mwenye akili wanasema amefanana na baba yake, akiwa na uwezo wa kawaida wanasema amefanana na mjomba wake ambaye ni ndugu wa mama wa mke, kuna mfumo dume ndani ya haya yote,” anasema Henga.

Anavitaja vitendo hivyo kuwa ukandamizaji wa haki za kijinsia na suluhu yake ni kubadili mitazamo.


Imeandikwa na Juma Issihaka, Habel Chidawali na Florah Temba