Dk Kashenge : Mtafiti aliyezalisha mbegu bora ya mpunga
Dk Sophia Kashenge-Killenga
Muktasari:
- Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Chollima Kilichoko, Dakawa, Morogoro kimeleta mafanikio kupitia utafiti uliofanywa na Mkuu wa Kituo hicho, Dk Sophia Kashenge-Killenga ambaye anaongoza jopo la watafiti wa mbegu bora za mpunga.
- Mtaalamu huyo aliyefanikisha kituo hicho kuzalisha mbegu bora zinazoweza kukabiliana na uharibifu wa udongo katika mashamba ya umwagiliaji ya mpunga yanayokabiliwa na ongezeko la chumvi.
Unamfahamu mtafiti mwanamke aliyewezesha nchi kupata mbegu bora za mpunga ili kukabiliana na uharibifu wa udongo?
Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Chollima Kilichoko, Dakawa, Morogoro kimeleta mafanikio kupitia utafiti uliofanywa na Mkuu wa Kituo hicho, Dk Sophia Kashenge-Killenga ambaye anaongoza jopo la watafiti wa mbegu bora za mpunga.
Mtaalamu huyo aliyefanikisha kituo hicho kuzalisha mbegu bora zinazoweza kukabiliana na uharibifu wa udongo katika mashamba ya umwagiliaji ya mpunga yanayokabiliwa na ongezeko la chumvi.
Mbegu za mpunga tatu ambazo mtafiti huyo amezalisha ni SATO1, SATO6 na SATO9 ambazo ni bora zaidi kukabiliana na ongezeko la chumvi katika mashamba ya umwagiliaji mpunga.
“Mbegu moja kati ya hizo tatu, SATO1 iliidhinishwa na kamati maalumu ya mbegu iliyoko wizarani Machi 18 mwaka huu,” anasema Dk Sophia.
Anasema utafiti wake ambao ulianza mwaka 2010 chini ya mradi wa kuzalisha mbegu wa Agra-PASS aliuanzisha kwa dhana ya kitafiti kuwa: “Kila mbegu ina uwezo wake wa kukua kulingana na aina ya udongo”.
Anaendelea kueleza kuwa ili kuboresha utafiti huo, mwaka 2013 alianzisha mradi nwingine wa utafiti chini ya mpango wa Shirika la Misaada la Maendeleo la Kimataifa Marekani (Usaid) –iAGRI kwa ajili ya kutafiti njia bora ya kubadili mfumo wa ardhi katika mashamba ya umwagiliaji mpunga ya Ndungu ya wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro.
Katika maboresho hayo ya utafiti, alisema watafiti walibaini matumizi ya madini ya Gypsum, mboji na taka zitokanazo na mabaki ya mbao zikiwekwa ardhini zinasaidia kurutubisha na kuwezesha mbegu hizo mpya kuleta mavuno zaidi kuliko katika ardhi isiyorutubishwa.
“Matokeo haya ya utafiti wa muda mrefu ni muhimu sana kwa kuwa ongezeko la chumvi ni chachu inayoua udongo taratibu. Kupatikana kwa tiba hii kutasaidia sana kuongeza mapato ya wakulima wa mpunga kwani chumvi imekuwa ikisababisha kupungua kwa mapato,” anasema.
Matokeo ya utafiti huu pia yatasaidia wakulima wadogo wengi wa mpunga ambao wanakabiliana na umaskini. Matokeo haya ya utafiti ni ufumbuzi wa kuongeza mapato katika uchumi wa familia na taifa kwa ujumla kwani usalama wa chakula pia utaimarika.
Kuhusu Dk Sophia
Ni mtafiti mwajiriwa wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi ni Ofisa Mfawidhi katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Chollima Iliyopo Dakawa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
Ana shahada ya uzamivu katika taaluma ya uzalishaji wa mbegu bora Tanzania hasa katika zao la mpunga.
Alihitimu shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha KwaZulu Natal Afrika Kusini. Alisoma shahada ya kwanza na ya pili katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua), kilichopo mkoani Morogoro.
Amefanya tafiti mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, anaamini kilimo hasa cha kisasa ni mkombozi kwa wakulima iwapo watafuata taratibu na kanuni bora za uzalishaji na hasa matumizi ya mbegu bora na mbolea.
Ndoto yake ni kumsaidia mkulima wa kawaida kujikomboa na kubadilika kupitia tafiti.