Elimu ndiyo kila kitu, tusiogope kurudi shule
Helga Mayala akiwa katika kazi zake za kila siku. Picha na Maimuna kubegeya.PICHA|MAKTABA
Muktasari:
“Muda wangu wa biashara hasa ya batiki ulikuwa ni baada ya saa kazi, lakini kila siku nilikuwa nikija na mzigo wangu kazini. Hivyo baada ya kumaliza kazi, moja kwa moja nilikuwa nikienda kwa wateja wangu kupeleka oda zao, hasa wenye maduka,” anasema Helga.
Ujasiriamali ni sifa ya asili aliyonayo kila mwanamke duniani. Lakini ili kuwa na tija hata ufanisi zaidi katika kazi hiyo, elimu ya darasani inahitajika.
Hii ndiyo sababu kubwa ya Helga Mayala (47), kuamua kurudi darasani ili kupata weledi zaidi hasa katika ujasiriamali.
Helga ni mwalimu mstaafu, anayemiliki Kampuni ya Hilglobe Success Enterprises ya jijini Dar es Salaam inayojishughulisha na utengenezaji na usambazaji wa bidhaa mbalimbali za usindikaji ikiwamo sabuni na batiki.
“Huwezi kuamini pamoja na kuwa na kazi hizi, biashara yangu ya msingi ilikuwa ni utengenezaji wa ‘ice cream’, niliyoifanya kwa zaidi ya miaka kumi,” anasema mwalimu Mayala ambaye pia ni mama wa watoto wanne akiwa mke wa Peter Mayala.
Baada ya kupata uzoefu wa kutosha katika kazi yake ya ualimu mama huyu mwenyeji wa mkoani Mwanza, aliamua kutumia muda wake wa mapumziko kujihusisha na biashara ya uuzaji wa vitambaa na mikoba aliyokuwa akiifuata visiwani Unguja.
“Baada ya kumaliza elimu yangu ya sekondari katika Shule ya Ashira, Moshi mkoani Kilimanjaro mwaka 1985, nilichaguliwa kujiunga na Chuo cha Ualimu Butimba kilichopo Mwanza, hapo nilisoma kwa miaka miwili kuanzia 1987/89, ” anasema.
Kwa kuwa kwa wakati ule ilikuwa ni lazima kufanya mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa, alilazimika kujiunga na mafunzo hayo katika kambi ya Mgulani mwaka 1990.
Kituo chake cha kwanza kikazi kilikuwa ni Shule ya Buyora iliyoko Mwanza, ambako alifanya kazi muda mfupi, kabla ya kuhamishiwa Dar es Salaam akimfuata mume wake.
“Nilipofika Dar es Salaam, shule yangu ya kwanza ilikuwa ni Kigogo, nilifundisha hapo kwa muda wa miaka mitatu na baadaye kuhamishiwa Tabata kabla ya Kijitonyama,” anasema.
Alianza na biashara ya Ice cream tangu akifundisha katika shule ya Kigogo hivyo katika kila shule aliyokuwa akihamia, aliendelea na biashara yake.
“Kuna wakati nililazimika kuajiri vijana ambao walinisaidia kufunga na hata kuuza biashara hiyo jambo lililochangia kuongeza tija zaidi,” anasema.
Helga anasimulia kuwa mwanzoni mwa mwka 2000 alihamishiwa katika Shule ya Msingi Makumbusho pia jijini humo na hapo aliamua kujiunga na kozi ya utengenezaji wa batiki iliyokuwa ikitolewa katika Chuo Cha Ufundi (VETA),Sinza.
“Ilikuwa ni kozi ya miezi mitatu, lakini baada ya kutoka hapo nilikuwa mahiri katika utengenezaji wa batiki ,” anasema.
Awali, Helga alikuwa akitengeneza batiki hizo na kuzisambaza katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, lakini mtaji ulipokuwa zaidi, alimudu pia kutoka nje ya jiji hilo na kwenda katika mikoa tofauti.
“Muda wangu wa biashara hasa ya batiki ulikuwa ni baada ya saa kazi, lakini kila siku nilikuwa nikija na mzigo wangu kazini. Hivyo baada ya kumaliza kazi, moja kwa moja nilikuwa nikienda kwa wateja wangu kupeleka oda zao, hasa wenye maduka,” anasema Helga.
Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko ndipo kilikuwa kituo chake cha mwisho cha kazi ya ualimu, kabla ya kuamua kuendelea na shughuli za ujasiriamali. “Biashara nyingine niliyojihusisha nayo ilikuwa ni uanzishaji wa mpango wa kuweka na kukopa. Baada ya kujishughulisha na biashara hiyo kwa muda mrefu, kukawa na usumbufu kwa baadhi ya wateja wangu, baadhi yao walikuwa hawalipi kwa wakati,”anasema Helga akiongeza:
“Kwa kuwa mume wangu ndiyo mshauri wangu mkuu, sikusita kumshirikisha pale nilipohitaji msaada hasa unaolenga kuendeleza kazi yangu ya ujasiriamali na baada ya kupata wasaa na kuongea naye, alinishauri nirudi shule, nikajifunze zaidi kuhusu biashara kwa jumla.”
Anasimulia kuwa alikubaliana na mumewe kurudi shule kutokana na ukweli usiopingika kwamba alikuwa na kipaji cha asili katika ujasiriamali, lakini hakuwa na utaalamu wa mambo ya biashara jambo lililochangia kumkwamisha katika baadhi ya maeneo.
Anabainisha kuwa aliamua kujiunga na kozi ya biashara katika Chuo cha Biashara( CBE) cha jijini Dar es Salaam na kuhitimu ngazi ya cheti.
Baadaye aliendelea kusoma chuoni hapo, lakini mara hii alijiunga na kozi ya uhasibu ngazi ya diploma. Kozi hiyo ilimchukua miaka miwili kuikamilisha kabla ya kujiunga na kozi nyingine ya usimamizi wa biashara na ujasiriamali cheti cha juu, iliyokuwa ikitolewa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhitimu mwaka 2010.
“Bado nina kiu ya kuendelea kusoma na kuwa mtaalamu zaidi katika masuala ya biashara, baada ya kuwa na elimu hiyo sasa namudu kuendesha kampuni yangu na sasa nimeajiri vijana wachache wanaonisaidia kutengeneza bidhaa zangu,” anasema.
Helga Kwa sasa amejikita zaidi katika utengenezaji wa sabuni mbalimbali pamoja na batiki akisafirisha bidhaa zake kwenda mikoa ya Arusha, Dodoma na Mwanza. “Mipango yangu ya baadaye ni kufungua shule ya ujasiriamali, itakayoanzia na shule ya awali hadi chuo,” anasema akihitimisha:
“Wito wangu kwa wanawake wote, wasiogope kurudi shule kwani elimu ndiyo msingi wa maisha.”