Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii ndiyo zawadi wanayostahiki kina baba

Muktasari:

  • Siku moja baada ya kutoka shule, mtoto mmoja wa miaka 12 jijini Dar es Salaam aliulizwa ni zawadi gani kubwa angependa kumpa baba yake. Badala ya kutaja simu mpya, fedha au nguo, alijibu kwa utulivu: “Ningependa tu akae nami kwa saa moja tuongee.”

Dar es Salaam. Katika mijadala ya malezi ya kisasa, baba mara nyingi huonekana kama mtoaji mkuu wa mahitaji ya familia akiwa na jukumu la kuhakikisha chakula kiko mezani, ada zinalipwa na maisha yanaendelea.

Hata hivyo, nyuma ya picha hiyo ya “nguzo ya familia” kuna swali linalojitokeza: kinababa wanapata nini kama zawadi ya kweli kutoka kwa familia zao hasa siku kama ya leo ambapo dunia inaadhimisha Siku ya Baba?

Siku moja baada ya kutoka shule, mtoto mmoja wa miaka 12 jijini Dar es Salaam aliulizwa ni zawadi gani kubwa angependa kumpa baba yake. Badala ya kutaja simu mpya, fedha au nguo, alijibu kwa utulivu: “Ningependa tu akae nami kwa saa moja tuongee.”

Jibu hilo dogo linaibua mjadala mkubwa: labda kile baba wanachostahili zaidi si vitu, bali uwepo, upendo na muda wa kweli na familia zao.


Baba nguzo ya familia

Kwa miaka mingi katika jamii nyingi za Tanzania, baba amepewa jukumu la kuwa nguzo kuu ya uchumi wa familia. Ni yeye anayetarajiwa kuamka mapema, kufanya kazi kwa muda mrefu, na kuhakikisha mahitaji yote ya nyumbani yanapatikana.

Kwa sababu hiyo, baba wengi huondoka nyumbani mapema na kurejea usiku wakiwa wamechoka, mara nyingine bila nguvu za kuzungumza na watoto wao.

Ingawa mchango huo wa kifedha ni muhimu na hauwezi kupuuzwa, wataalamu wanasema hauwezi kuchukua nafasi ya uwepo wa baba katika malezi ya kila siku.

 Mwanasaikolojia wa familia, Neema Mwakalonge, anasema utafiti wa kitabia unaonesha watoto wanaokua karibu na baba zao huwa na uwezekano mkubwa wa kujiamini, kufanya vizuri shuleni na kuwa na uwezo wa kukabiliana na msongo wa mawazo.

“Mtoto anahitaji kujua kuwa baba yake anamsikiliza na kumjali. Hata kama baba hana uwezo mkubwa wa kifedha, uwepo wake katika maisha ya mtoto unaweza kuwa na thamani kubwa kuliko vitu vingi vya kimwili,” anasema Neema.

Anaongeza kuwa watoto wengi wanaokabiliwa na changamoto za kihisia, uoga au kutojiamini, mara nyingi hukosa sio tu rasilimali bali ukaribu wa kihisia na wazazi wao, hususan baba.


Hadithi za ndani ya familia

 Mtazamo huo unaungwa mkono na mzazi wa watoto watatu, Juma Ngonyani, ambaye anasema aligundua umuhimu wa kushiriki malezi baada ya kuona watoto wake wakianza kuwa karibu zaidi na mama yao kuliko yeye.

“Nilikua nafikiri kazi yangu ni kutafuta fedha tu. Lakini siku moja mtoto wangu alipoanza kuniogopa badala ya kuniamini, nilitambua kuna kitu nilikuwa nakikosa. Sasa kila wiki natenga muda wa kuzungumza nao na kufuatilia masomo yao,” anasema.

Anasema mabadiliko hayo madogo yamebadilisha uhusiano wake na watoto wake, ambao sasa wanamueleza mambo yao kwa uwazi zaidi kuliko hapo awali.

Kwa upande wake, baba mwingine wa Dar es Salaam, Salum Abdallah, anasema malezi hayapaswi kuachwa kwa mama pekee hata kama baba ana majukumu mazito ya kiuchumi.

“Ukweli ni kwamba watoto hawahitaji fedha tu. Wanahitaji kuona baba yupo, anasikiliza na anajali. Nimejifunza kupanga muda wa jioni kukaa na watoto hata kama nimechoka,” anasema Abdallah.

Anasema muda huo mfupi wa kuwa pamoja na watoto wake umesaidia kuboresha mawasiliano na kupunguza migogoro ya kifamilia nyumbani kwake.

Baba mwingine, ambaye ni mfanyabiashara wa Kariakoo, Hassan Mbaraka, anasema awali aliamini mafanikio ya kifedha yanatosha kuwa zawadi kwa familia, lakini baadaye alibaini hilo halitoshi.

“Ningefikiria nikileta pesa nyumbani basi kila kitu kiko sawa. Lakini niligundua watoto walikuwa wanahitaji zaidi mazungumzo yangu na uwepo wangu. Sasa hata nikiwa bize kazini napata muda wa kupiga simu nyumbani,” anasema Mbaraka.

Dereva wa bodaboda jijini Dar es Salaam, Ally Ramadhan ambaye pia ni baba anasema kazi yake ya kila siku haijamzuia kuwa karibu na watoto wake, licha ya uchovu wa kazi.

“Mimi napanda pikipiki mchana kutwa, narudi nyumbani nimechoka sana. Lakini nimejifunza kuwa hata dakika 20 za kucheza au kuzungumza na watoto zinabadilisha hali ya nyumba. Wanakuwa na furaha na hata mimi napata amani,” anasema Ramadhan.

Kwa upande mwingine, changamoto za kiuchumi zimeendelea kuwafanya baadhi ya baba kushindwa kuwa karibu na familia zao. Wapo wanaofanya kazi mikoa tofauti na walipo watoto wao, huku wengine wakitumia muda mwingi kutafuta kipato.

Hata hivyo, wataalamu wanaeleza kuwa hata katika mazingira hayo, mawasiliano ya mara kwa mara kupitia simu, ujumbe au video yanaweza kusaidia kuimarisha uhusiano kati ya baba na watoto.

 

Kumbukumbu za mtoto na thamani ya uwepo

Akizungumza na Mwananchi, mtoto wa miaka 15 ambaye hakutaka jina lake litajwe, anasema kitu anachokikumbuka zaidi kuhusu baba yake ambaye kwa sasa ni marehemu si zawadi alizowahi kumpa, bali ushauri na muda aliokuwa akimpatia.

“Baba alikuwa ananiuliza kila siku shule imekuwaje. Hata nilipokosea alikuwa hanipigii kelele sana, alikaa na kunieleza. Hilo ndilo ninalolikumbuka hadi leo,” anasema.

Kauli hii inaonesha kuwa mara nyingi watoto hawakumbuki thamani ya vitu walivyopewa, bali namna walivyohisi walipokuwa pamoja na wazazi wao.

Mtaalamu wa malezi, Asha Mnyamwezi, anasema ujumbe mkubwa unaojitokeza katika maadhimisho ya Siku ya Baba ni kwamba watoto wanahitaji zaidi ya fedha za matumizi.

Anasema wanahitaji baba wanaowasikiliza, wanaowashauri, wanaowafariji wanaposhindwa na wanaosherehekea nao wanapofanikiwa.

“Baba si ATM ya familia wala mtoa mahitaji pekee, bali ni mlezi, mshauri, mwalimu na rafiki wa watoto wake,” anasema.


Mabadiliko ya kijamii na changamoto mpya

Asha anaeleza kuwa katika dunia inayobadilika kwa kasi, mzigo wa kazi na maisha ya mijini umeongeza pengo kati ya baba na watoto.

Wazazi wengi hutumia muda mrefu kazini, kwenye biashara au kwenye usafiri, hali inayopunguza muda wa familia.

Anasisitiza kuwa zawadi kubwa zaidi ambayo baba anaweza kumpa mtoto wake si kiasi cha fedha alichoweka benki, bali muda anaoutumia kujenga kumbukumbu na uhusiano wa kudumu.

Tofauti na miaka ya nyuma ambapo malezi yalionekana zaidi kuwa jukumu la mama, sasa wataalamu wanasema mazingira ya sasa yanahitaji ushirikiano wa wazazi wote wawili kwa kiwango sawa.

Mama wa watoto wawili, Rehema Hamisi wa Dar es Salaam, anasema watoto wake huwa na furaha zaidi wanapopata nafasi ya kuwa karibu na baba yao.

“Wakati mwingine wanaweza kukaa sebuleni wakiongea au wakitazama mpira pamoja. Unaona kabisa watoto wanavyofurahi. Huo muda una mchango mkubwa kuliko hata vitu vya gharama,” anasema.


Watoto kukua bila baba na athari za kihisia

Pamoja na umuhimu wa baba, Tanzania bado inakabiliwa na changamoto ya baadhi ya watoto kukua bila uwepo wa karibu wa baba zao kutokana na migogoro ya kifamilia, talaka, kutengana au kutowajibika kwa baadhi ya wanaume.

Mwanasaikolojia Asha Mbwana anasema hali hiyo inaweza kuathiri ukuaji wa mtoto endapo hakutakuwa na mfumo mbadala wa msaada wa kihisia.

“Baba ni sehemu muhimu ya ukuaji wa mtoto. Hata hivyo, pale ambapo hayupo, ni muhimu familia na jamii kuhakikisha mtoto anapata mwongozo kutoka kwa watu wengine wenye ushawishi chanya,” anasema.

Anasema maadhimisho ya Siku ya Baba yanapaswa kuwa fursa ya kutafakari, si kusherehekea tu. “Kizazi cha sasa kinahitaji baba wanaoshiriki zaidi katika maisha ya watoto wao kuliko ilivyokuwa zamani,” anaongeza.


Athari za migogoro ya ndoa

Kwa upande wake, Leonida Mollel, mtaalamu wa saikolojia, anasema migogoro ya ndoa ikiwemo talaka ina athari kubwa kwa uhusiano kati ya mtoto na baba.

Anasema watoto wengi huathirika kihisia pale wanapokosa ukaribu na wazazi wote wawili baada ya kutengana.

“Katika mazingira ya talaka, migogoro ya muda mrefu huathiri mawasiliano. Wakati mwingine mtoto anajikuta amekosa kabisa mawasiliano na baba, jambo linaloathiri maendeleo yake ya kihisia,” anasema.

Anaeleza kuwa mtoto anapokosa mawasiliano ya mara kwa mara na baba yake, huweza kukua akiwa na hisia za kukataliwa au kutojithamini. Hali hii inaweza kuathiri namna anavyojenga uhusiano wake wa baadaye.

Anasisitiza kuwa changamoto kubwa si talaka yenyewe, bali namna wazazi wanavyoshughulikia malezi baada ya kutengana.

“Mtoto hawezi kubeba makosa ya wazazi wake. Ni muhimu kuhakikisha uhusiano wake na baba na mama unabaki salama,” anasema.


Wito kwa jamii na wazazi

Wataalamu wanasisitiza kuwa jamii inapaswa kubadili mtazamo wa kumchukulia baba kama mtoa fedha pekee, na badala yake kumwona kama mshirika kamili wa malezi.

Shule, taasisi za kidini na jamii kwa ujumla zina nafasi ya kuelimisha wazazi kuhusu umuhimu wa uwepo wa kihisia katika maisha ya watoto.

Pia, baba wanahimizwa kupanga muda maalum wa kuwa na watoto wao, hata kama ni dakika chache kila siku, kwa kuzungumza, kusikiliza au kufanya shughuli za pamoja.