JOKATE:Afikiria kubadili fani akiacha urembo
Muktasari:
Mrembo huyo pia ni mcheza filamu, mwanakwaya na mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha Channel ‘O’ nchini Afrika Kusini.
JOKETI Mwegelo ni jina lililovuma muda mrefu katika masikio ya watu wengi hasa wapenda burudani, mitindo na masuala ya urembo kwa jumla.
Uwezo wake wa kufanya vitu vingi na kwa ufanisi ndio chachu ya kufahamika kwake zaidi.
Nyota yake ilianza kung’ara baada ya kuibuka mshindi wa pili katika Shindano la Miss Tanzania mwaka 2006 na kuwa balozi wa kinywaji cha Redds.
Hadi sasa Joketi anafahamika kama mrembo na mjasiriamali anayemiliki Lebo ya Kidoti Fashion, inayojishughulisha na uuzaji wa nywele na mavazi akiwa na mpango pia wa kuongeza uuzaji wa manukato.
Mrembo huyo pia ni mcheza filamu, mwanakwaya na mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha Channel ‘O’ nchini Afrika Kusini.
Katika mahojiano na Mwananchi Jumapili, pamoja na mambo mengine Jokate, anataja watu watatu wanaomvutia katika ulingo wa siasa na maisha ya kawaida.
Mwananchi Jumapili: Kwa hapa nchini wanasiasa gani wanaokuvutia?
Joketi: Januari Makamba ninapenda anavyofanya mambo yake kwa mipango, Zitto Kabwe kwa ile hali yake ya kupenda siasa, lakini pia kuna John Mnyika, ambaye pamoja na kuwa mbunge, anaishi maisha ya kawaida kabisa.
Mwananchi Jumapili: Tukiachana na siasa, wewe ni mrembo, nje ya urembo wako unadhani ni sifa gani zitashawishi uonekane mke anayefaa?
Joketi: Kwanza najituma, nimeelimika, nashirikiana vizuri na jamii, nahisi kama sina makuu, hivyo nadhani sifa hizo zinashawishi.
Mwananchi Jumapili: Ni mwanaume gani anaweza kuwa mume bora kwako?
Joketi: Yeyote yule, haijalishi maarufu au asiye maarufu. Mimi nikikupenda, nikavutiwa na wewe basi inatosha, lakini sitegemei kupata mwanaume asiye na malengo.
Mrembo huyo pia anaweka wazi nia yake ni kutaka kuingia kwenye siasa na hata kugombea ubunge katika moja ya majimbo ya uchanguzi mkoani Ruvuma.
Mwananchi Jumapili: Wapenzi wa burudani na mashabiki wangependa kujua ukweli kuhusu tetesi kwamba wewe unataka kuingia kwenye siasa. Jambo gani limekushawishi uingie kwenye siasa?
Joketi: Kuwa kiongozi ni ‘talent’ (kipaji), ambayo ninayo, lakini pia nina azma hiyo tangu nilipokuwa kidato cha tano mwaka 2005.
Nilikuwa nikijiita JK, kwa sababu nilimpenda sana Rais Jakaya Kikwete, pia niliwahi kuwa Dada Mkuu shuleni na chuoni nilishauriwa sana kuingia kwenye siasa.
Mwananchi Jumapili: Una mkakati gani, unaodhani itakuwa silaha ya kufanikiwa kwa harakati zako katika siasa?
Joketi: Kuna vijana wengi wana vipaji, lakini hawana msaada wa kuendelezwa na zaidi kuna uhitaji mkubwa wa kuwekeza katika elimu kwani wanafunzi wana mwitikio wa elimu, lakini katika mazingira duni, kuwekeza kwenye elimu na vipaji ndiyo siri kubwa kwangu.
Mwananchi Jumapili: Kila jambo lazima liwe na masilahi, wewe unafuata masilahi gani kwenye siasa?
Joketi: Masilahi niliyotazamia kwangu ni kufanya mapinduzi ya elimu na vipaji katika jimbo langu, kama ni masilahi ya kiuchumi au kujenga jina nadhani kazi zangu zinanitosha sana.
Mwananchi Jumapili: Vipi kuhusu chama?
Joketi: Bado sijafanya uamuzi ya kuingia kwenye chama.
Mwananchi Jumapili: Je, msaada wa kufanikisha harakati hizo unategemea kuupata wapi?
Joketi: Kuna kampuni na wadau mbalimbali nitakaowashirikisha pamoja na familia yangu.