Mapishi ya kuku wa kupaka
KUNA aina mbalimbali za mapishi ya kuku ikiwamo kukaanga, mchuzi, mchemsho au supu. Lakini leo katika safu hii, tutaangalia namna ya kuandaa kuku wa kupaka.
Mahitaji
- Kuku mmoja
- Kitunguu saum kimoja
- Tangawizi moja
- Pilipili hoho mbili
- pilipili mbuzi mbili
- Ndimu mbili au limao
- Manjano nusu kijiko
- Tui la nazi
- Vitunguu maji viwili
- Chumvi vijiko viwili
- Nyanya nne
- Karoti moja
Namna ya kuandaa
Katakata kuku katika vipade vya wastani kulinganana na walaji, kisha msafishe katika maji safi hadi uchafu wote uishe na umweke pembeni.
Twanga vitunguu saum na tangawizi ili kupata mchanganyiko utakaotumia kuweka katika vipande vya kuku ulivyokatakata.
Weka pia ndimu au limao, chumvi kiasi, pilipili na mafuta kijiko kimoja, kisha acha kwa muda wa nusu saa ili viungo vichanganyike na kukolea vizuri katika nyama.
Bandika sufuria nyingine jikoni, kisha kaanga vitunguu maji mpaka vibadilike rangi, tia pilipili hoho, karoti na nyanya ukiendelea kukaanga mpaka viive kabisa.
Baada ya kuhakikisha nyanya zimeiva, mimina tui bubu la nazi na uache lichemke hadi liive, mchuzi uwe mzito kama roast.
Banika vipande vya kuku ulivyovikata kwa muda wa robo saa, huku ukivigeuzageuza ili viive kwa joto.
Baada ya hapo vitakuwa tayari na weka kwenye sufuria, kisha miminia ule mchuzi mzito na ufunike halafu upalie kwa kuweka mkaa juu kama wali.
Acha nyama ikauke vizuri kwa muda wa dakika kumi, hapo mlo wako utakuwa tayari.
Kuku wa kupaka anaweza kuliwa kwa wali, ugali, tambi, mkate hata maandazi.
Imeandaliwa na Elizabeth Edward
[email protected]