Prime
Simulizi ya Kanali Kipingu alivyomuoa mtoto wa ‘mwenye nyumba’
Wakati huo hakuwa na nyumba wala gari, alikwenda kama alivyo na kueleza hisia zake kwa binti wa mwenye nyumba na kumuomba akubali kumuoa.
Hiyo ilikuwa mwaka 1975, Kanali mstaafu, Iddi Kipingu akiwa kijana anayejitafuta kimaisha, mazingira aliyomkuta binti yule ndiyo yalimvutia, na kusema moyoni mwake huyo ndiye mkewe.
Anasema alimkuta binti huyo wa Kimanyema katika mazingira ambayo aliamini huyo ndiye anafaa kuwa mke wa maisha yake.
"Nilikwenda kumtembelea kaka yangu aliyekuwa amepanga Magomeni Makanya, hapo ndipo nilikutana na Siose Ngomesha kwa mara ya kwanza. Nilimkuta anatwanga kisamvu, nikamuuliza kaka yangu huyu binti vipi? Kaka akaniambia achana naye kabisa, ni mtoto wa mama mwenye nyumba," anasema Kipingu, katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika nyumbani kwake Makonde, Dar es Salaam.
Akiwa sambamba na mkewe, Kipingu anasema wakati huo alikuwa akiishi hosteli, pia alikuwa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
"Alikuja kwangu hana shuka wala nyumba, mara ya kwanza aliponiambia anataka kunioa, mwenyewe nilimpenda, alikuwa ni kijana maridadi, mcheshi, nilivutiwa naye," anasema Siose.
Leo hii, Kipingu na mkewe wanakwenda kutimiza miaka 50 ya ndoa, wakiwa na watoto wanne na wajukuu, miaka ambayo anasema ilikuwa ya kuvuka milima na mabonde.
"Tulipigwa na mawimbi tofauti tofauti, lakini tuliyashinda, katika mapito yote, nimshukuru mke wangu," anasema.
Waliwezaje?
Kipingu anasema alimfuata binti huyo kwa uhalisia, bila kutumia uongo ili ampate, jambo ambalo vijana wengi wa sasa hawawezi na hicho ndicho kimekuwa chanzo cha ndoa nyingi za wakati huu kutodumu.
Si kama Kipingu ndiye wa kwanza au atakuwa wa mwisho kudumu kwenye ndoa kwa miaka 50, wapo wanaozidi hiyo.
Hata hivyo, mazingira aliyopitia, umaarufu aliokuwa nao, wakati huo akiwa winga machachari wa Yanga, msomi wa chuo kikuu, kisha mkuu wa sekondari ya Makongo, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania (FAT, sasa TFF) na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) anaeleza namna alivyoweza kuvuka milima na mabonde na kuhakikisha ndoa yake haitetetereki.
Kipingu alimkuta mkewe wakati huo bado binti, akilelewa na shangazi yake, alimuomba kaka yake ambaye ndiye alikuwa mpangaji kwenye nyumba hiyo amsaidie.
Wakati huo, mkewe alikuwa ni sekretari wa waandishi wa habari Uhuru na Mzalendo na Kipingu akiwa ni mwanafunzi wa chuo kikuu, hana kazi.
"Mimi nimekulia kijijini, ni mtoto wa kwanza kwetu, tena wa kiume, mazingira ya kwetu Wasambaa, maji ni ya kuchota milimani, nishati yetu ni kuni, hatuna umeme hivyo lazima kutwanga. Nilimpokuta bibie anatwanga, nikasema huyu ndiye binti ninayeweza kumpeleka kwa mama.
Siose anasema siku anakutana na Kipingu kwa mara ya kwanza, hakwenda kazini, hivyo alilazimika kufanya zile kazi za nyumbani za usafi, kisha akawa na jukumu la kutwanga.
"Kumbe wakati nayafanya hayo, kuna mtu alikuwa akiniangalia kwa wazo la mke, hata alipotahadharishwa kuwa ni mtoto wa mwenye nyumba asijaribu kunisogelea, hakurudi nyuma," anasema Siose, huku akitabasamu.
Akizungumzia mazingira hayo, Kipingu anasema wakati huo yeye alikuwa ni msomi wa chuo kikuu ambako kulikuwa na kila aina ya marafiki, na wasichana wa kila aina.
"Pamoja na yote, nilisema hapana huyu ndiye mke wa maisha yangu. Niliona ataingia kwenye mfumo wa maisha ya kule kijijini kwetu, halafu ilikuwa ni fedheha sana kijana kuwapelekea wazazi mke ambaye haendani na mfumo wa maisha ya kijijini kwetu.
"Nilipomkuta anatwanga nilimuona huyu ni mke, nilimpa ndugu yangu kazi ya kumfuatilia, mtaa ule pia kulikuwa na mjomba wangu hivyo habari zake zote nikawa nazipata.”
Anasema wakati huo alikuwa na fursa zote za kukutana na wanawake wa kila aina, kwani alikuwa msomi, pia mcheza mpira wa timu kubwa ya Yanga, tena akiwa nyota wa timu hiyo, lakini hakuhitaji mwanamke ili mradi mwanamke, bali mke.
"Nilipomueleza nataka kumuoa, hakukataa, naye alinipenda, nilipohitimu Chuo mwaka 1977, tukafunga ndoa mwezi Oktoba tukiwa tumefahamiana kwa miaka mitatu," anasema.
Misukosuko ya ndoa
Anasema walipata mtoto wa kwanza Machi 1978, ambaye aliongeza furaha ya ndoa yao na miezi michache baadaye akamuacha mkewe na mtoto mchanga, yeye Kipingu akaenda vitani.
Wakati huo waliishi Tandika Maghorofani na mkewe akifanya kazi Uhuru na Mzalendo ambazo zilikuwa Tazara.
"Tulikuwa tumeanza maisha hatuna kitu, niliona kawaida, hata kazini nilikuwa natembea kwa miguu, tunapitiana na wafanyakazi wenzangu tunatembea.
"Hata wakati nikiwa na mimba, nilikuwa natembea kutoka Tandika kwenda Tazara, hadi siku najifungua ilikuwa hivyo, na hii hata kwenye mazoezi ilimisaidia kujifungua salama," anasema mkewe.
Kipingu akizungumzia misukosuko ya ndoa, anasema ilikuwa ni mingi na hadi wanakwenda kufikisha miaka 50, haikuwa kazi rahisi.
"Ambacho kimetufikisha hapa, kikubwa kabisa ni kuvumiliana, lakini jambo la pili ni kumuelewa mwenzako na mimi na mke wangu tulikuwa na muda wa kuelewa".
Anasema tangu siku ya kwanza amemwambia jinsi anavyompenda, mkewe alimuelewa na kutambua mazingira yake halisi.
"Alifahamu nipo chuo kikuu, sina chochote, lakini wakati ule ajira zilikuwa wazi, ukimaliza tu chuo unapata kazi.
"Nilipomfuata, nilienda kama nilivyo sina kazi, ila nina uhakika wa ajira nikihitimu," anasema na ndivyo ilivyokuwa, kwani baada ya kuhitimu alipangiwa kazi JKT Mgulani na kupewa nyumba ya kuishi Tandika.
Anasema hata alipokuwa chuo, mkewe alikuwa akipewa taarifa kila ambacho yeye Kipingu alifanya, kwa kuwa alikuwa pia mchezaji staa wa Yanga wakati ule na waandishi wa habari walikuwa wakifanya kazi na mkewe.
"Kilichonisaidia zaidi, sikuwa na mambo mengi, ilikuwa ni chuo na mpira, hii ilisaidia kutokuwa na mengineyo.
"Sikuwa na vishawishi vingine zaidi ya maeneo ya chuo au hostel, hata hivyo starehe yangu ilikuwa ni mpira na kwa kuwa nilishaamua hawa waishie chuo lakini kwenye familia yangu ni huyu na nilimudu hilo," anasema
Anasema ukionyesha maisha feki ili kumvutia mwenza, mnapofika kwenye uhalisia akiwa na matumaini makubwa akikuta sivyo ni mgogoro.
Kinachowashinda vijana wengi
Kipingu anasema, ndoa nyingi nyakati hizi hazidumu kwa kuwa vijana wanaoana katika mazingira ambayo sio ya uhalisia.
Anasema wengi wanaanzisha uhusiano baada ya kukutana na wenza wao kwenye casino, kwenye hoteli kubwa, kwenye fukwe na maeneo mengine ambayo si ya uhalisia.
"Kuna wengine wanatumia uongo hadi kuazima magari, nguo ili mradi ampate binti, jambo ambalo linasababisha wengi wao kuachana mapema kwa kuwa mazingira ya mwanzoni ambayo yalipaswa kuwa ya uhalisia yanaanza kwa uongo.
"Hata wachache wanaodumu, ni busara tu ndiyo huwa inasaidia, kwani ndoa za siku hizi nyingi zina matatizo mengi, mengine yanachochewa na wazazi.
Anasema utakuta binti anaolewa kwa sababu wazazi wake wanataka waone anaolewa katika mazingira fulani ambayo ni ya tofauti na uhalisia wa muoaji.
"Yale mazingira ambayo wazazi wa muolewaji wanayatarajia kwa mtoto wao yanapokosekana, ndipo matatizo yanaanza.
Inafikia hatua mume anaweza kupeleka malalamiko ya mkewe kwa wazazi wa binti, wao badala ya kutuliza ndio wanakoleza moto na ndoa nyingi tumezishuhudia hayo yanatokea," anasema.
Ukweli ukorofi wa mama mkwe
Kuna baadhi ya watu huwa wanaamini mama wa mume ni adui, wengine hawaelewani kabisa, lakini kwa mke wa Kipingu, anasema kama ukiwa na upendo na mkweo naye atakupenda tu.
Siose anasema kwa imani yake mkamwana kufikia hatua ya kugombana na mama mkwe ni ukosefu wa maadili.
"Niliolewa kabla sijaenda ukweni kwangu, ila wao walikuwa wakija, hadi nilipojifungua ndipo nilikwenda, lakini wakwe zangu na ndugu wa mume wangu walinipenda. Hawakuwa na ukabila, mimi mtu wa Kigoma, mume wangu Msambaa wa Tanga.
"Kuna saikolojia ya kuwa ndani ya ndoa na namna utayapokea mapungufu ya ukweni na kukubali mazingira, mila na vitu kama hivyo, usipokuwa na maandalizi hayo ni ngumu,” anasema Siose.
Ushauri kwa wanandoa
Mama huyu anasema ndoa ni taasisi muhimu inayopaswa kuheshimiwa, hivyo kabla ya kufanya uamuzi wa kuingia inahitajika mtu awe na hekima.
Anasema unakutana na mtu anataka uwe mke wake na kukutambulisha kwao, inabidi kuipokea hiyo hali kwa upekee.
"Ukimkubalia, ndani ya nafsi yako unatakiwa uwe na upendo wa dhati, umpende jinsi alivyo, si kwa sababu ya kitu, ingawa hii hali nyakati hizi inapotea, sijui wanaangalia sana mali.
"Mtu anaingia kwenye ndoa akiwa tayari ameweka hesabu zake kwamba akiingia atapata moja, mbili, tatu, vikikosekana ndoa hiyo haipo," anasema.
Anasema, yeye alipoolewa na Kipingu hakuwa na chochote, walipendana kama walivyo, hakuwaza mume mwenye gari wala nyumba, hivyo walivitafuta pamoja.
Kwa upande wake Kipingu yeye anaamini mazingira yaliyopo sasa ndiyo chanzo cha ndoa nyingi kutokudumu, huku vijana wengi wakionekana kukosa uvumilivu
"Siyo kama vijana wa sasa wanataka iwe hivyo, lakini mazingira yanawalazimisha, maisha ya kila siku hivi sasa yana vipotoshi vingi vya namna watu wanavyoyaelezea, hivyo kuyafanya yawe ya tofauti.
"Utaona hata vijana wanaomaliza vyuo, hata mentality zao huwa ni gari, nyumba na sio wavulana tu hata wasichana, hali hii inasababisha kutokuwa na uvumilivu baina yao wakiingia kwenye ndoa," anasema.
Kipingu anasema maisha ya ndoa yanahitaji uvumilivu na subira, jambo ambalo kwenye mazingira ya sasa hakuna subira, ndiyo maana ndoa nyingi zinaishia kuvunjika.
"Zamani haikuwa hivyo, mnapanga na mkeo baada ya miaka sita au muda fulani ndipo tuanze kujenga au kununua gari na vitu vingine, tofauti na sasa mazingira yanawalazimisha kuingia kwenye ndoa bila uhalisia.