USHAURI WA DAKTARI: Unaweza kupata ujauzito kipindi cha kunyonyesha?

Kweli wanawake wengi wanadhani kuwa hawawezi kupata ujauzito kipindi wananyonyesha hasa kutokana na kutopata hedhi au kupata hedhi kidogo katika miezi ya awali tangu wajifungue.

Kitabibu ni sahihi kunyonyesha na ni mojawapo ya njia ya asili ya uzazi wa mpango ambayo watu wenye imani za kidini wanakubali kuitumia.

Ieleweke kuwa uwezo wa kupata mimba unakuwa mdogo kwa mwanamke anapokuwa ananyonyesha mara kwa mara, ila sio sahihi kusema njia hii inakuzuia kupata mimba kabisa.

Njia hii inafanya kazi zaidi na kuweza kuzuia mimba kwa asilimia 98 endapo tu mtoto anapokuwa na umri wa miezi sita na anatumia maziwa ya mama tu akinyonya mara kwa mara, mchana na usiku.

Vile vile kama mama huyo atakuwa bado hajapata hedhi ya kila mwezi tangu alipojifungua.

Je, ni kwa vipi kunyonyesha ni njia mojawapo ya kuzuia ujauzito. Wakati mwanamke anapokuwa ananyonyesha huwa inazuia au kuchelewesha mzunguko wa hedhi kutokea.

Mwanamke anaponyonyesha husababisha kusisimuliwa kwa kichochezi (hormon) kijulikanacho kitabibu kama prolactin au milk hormon.

Kiwango cha kichochezi hiki kinapokuwa kipo juu mwilini huzuia viwango vya vichochezi vinavyochochea upevushwaji wa kijiyai cha kike (ovulation).

Na hii ndiyo sababu hata mizunguko ya hedhi ya wanawake wanaonyonyesha kutoonekana katika miezi ya awali baada ya kujifungua au anaweza kuwa na mzunguko ambao unabadilika badilika.

Kadri miezi inavyosogea baada ya kujifungua kiwango cha kichochezi cha prolactin hupungua, ndiyo maana wengi wanaonyonyesha huwa hawapati ujauzito katika miezi mitatu ya awali.

Kwa mwanamke ambaye ametoka kujifungua na ananyonyesha kabla ya kuanza tena kupata mzunguko wake wa hedhi, hutanguliwa kwanza na kuanza kupevushwa kwa kijiyai cha kike.

Wanawake wengi huwa hawajui kama kijiyai cha kike kimepevushwa na kipo tayari kuungana na mbegu ya kiume ili kutunga mimba, mpaka tu pale zinapopita wiki 2 na kupata hedhi yake.

Kwa kawaida kijiyai cha kike kisipopevushwa na mbegu ya kiume baada ya kushiriki tendo la ndoa ndipo hedhi hutokea.

Wanawake wanaopata ujauzito kipindi cha unyonyeshaji ni wale ambao watoto wao wanaacha kunyonya mapema au wanalala sana na kutonyonya vizuri usiku.

Hii ni kwa sababu kile kiwango cha kichochezi cha pralactin kinapungua, hivyo wanaweza kupata mimba ndani ya miezi mitatu mpaka tisa tangu alipojifungua.

Wanawake wengine wanaopata ujauzito kipindi hiki ni pamoja na wale ambao wamewaachisha watoto wao kunyonya na kuwapa maziwa ya chupa.

Pia wale ambao wanawanyonyesha huku wanawapa maziwa ya chupa katika miezi ya awali baada ya kujifungua nao wapo katika hatari ya kupata mimba kipindi hiki cha unyonyeshaji.

Vile vile watakapoanza kuwapa watoto wao vyakula huwa ni baada ya kufikisha miezi sita nao wanakuwa katika hatari ya kushika ujauzito wakiwa wananyonyesha watoto wao.

Hivyo tunaona kuwa mimba inaweza kutungwa kipindi cha unyonyeshaji.

Ni vizuri kama huhitaji kupata ujauzito kipindi hiki tumia njia nyingine za uzazi wa mpango mapema pale utakapokuwa tayari umeanza tena kujamiiana bila kinga na mwenza wako.