Wanandoa ni sawa na kata na mtungi
Muktasari:
- Unapomlinda, kumtunza na kumtunzia siri mwenzako, unajilinda na kujitunzia siri zako mwenyewe. Ukimbomoa, naye anaweza kukubomoa. Ukimjenga, atakujenga.
Canada. Kuna usemi kuwa siri ya mtungi aijuaye kata. Kama wewe ni mtungi, nani ni kata yako? Je, nani ajuaye siri zako au za mwenza wako zaidi ya nyinyi wawili kuliko mtu yeyote?
Nyinyi ni mitungi na kata baina yenu. Japo, tunaweza kusema ni jambo linalojulikana kwa wote, wawili mnajuana kuliko hata wanavyowajua wazazi wenu.
Hii ni kwa sababu binadamu huendelea kukua. Hivyo, kuna vitu mlivyo navyo ambavyo wazazi wenu hawakuona na hawataona isipokuwa nyinyi tu katika uhai wenu.
Kata haina midomo hata ingekuwa nayo, tunadhani isingetoboa siri ya mtungi ambao una mdomo. Uzuri, viwili hivi huwa havikosani wala kuadhiriana bali hutunziana siri. Mtungi hata uiumize vipi kata, kata katu haitatoboa siri yake. Na wanandoa, japo wana midomo, wanapaswa kuwa mitungi na kata.
Walindane, kutunzana, na kutunziana siri zao. Kwa hiyo, wasibagazane, kudhalilishana, kudhulumiana wala kusalitiana. Kwani, wakipuuzia haya, wajue watakaoumia ni wao iwe kwa pamoja au tofauti.
Kuhifadhiana, kulindana na kuteteana siyo hisani wala ombi bali haki na wajibu kwenu nyote sawia. Kwa sababu kila anayetenda haya hamtendei mwenziwe bali hata yeye mwenyewe.
Unapomlinda, kumtunza na kumtunzia siri mwenzako, unajilinda na kujitunzia siri zako mwenyewe. Ukimbomoa, naye anaweza kukubomoa. Ukimjenga, atakujenga.
Isitoshe, kama ulivyo wewe, naye atakufanyia hivyo hivyo kama umfanyiavyo vingenevyo awe na matatizo yake. Unapomuumiza mwenzio, unajiumiza mwenyewe. Kwani, naye anaweza kukuumiza kama umuumizavyo hivyi wote mkaishia kuumizana.
Kumbuka. Kama ulivyo binadamu mwenye akili kubwa na timamu na asiyetabirika, naye pia ni binadamu mwenye sifa kama zako hata wakati mwingine kukuzidi katika baadhi ya mambo. Kama ulivyo mkweli au mkatili, naye kadhalika anaweza kuwa hivyo.
Swali la kujiuliza
Katika kuangalia ukweli wa kuhifadhiana, wanandoa wajiulize swali moja kuu. Inakuwaje muweze kuvuliana nguo lakini mfungiane mioyo? Mnawezaje kujuana siri na udhaifu wenu halafu mvitoe hadharani? Je, mnafanya hivyo kwa faida au hasara ya nani?
Hao mnaowapa siri zenu na kubomoana mnayajua yao? Hata mkiyajua, kwani lazima mjiumize au kujivua nguo kwa sababu wao wamejivua nguo na kujiumiza?
Katika sheria nyingi za nchi nyingi, kuna vipengele vinavyowaachia haki wanandoa kulindana hata kwenye baadhi ya makosa isipokuwa udhalilishaji wa watoto. Hata hivyo, bado mwenza anayo haki ya kuamua kutoa au kutotoa ushahidi dhidi ya mwenziwe katika kesi yoyote.
Mfano, mke au mume haruhusiwi kutoa ushahidi wa kumbomoa mwenziwe kisheria chini ya kile kiitwacho ‘spouse privilege au spouse immunity’, yaani kinga au upendeleo wa wanandoa ili kudumisha amani na mshikamano wa ndoa.
Kwa kujua unyeti wa ndoa, sheria za makosa ya jinai, pamoja na ukali na ukale wake, bado vinatoa kinga na upendeleo ili kuwawezesha wanandoa kuhifadhiana na kulindana. Hakuna kosa kubwa duniani kama kuua.
Japo, kisheria, mke au mume anayo haki na ulazima wa kutoa ushahidi dhidi ya mwenziwe pale atuhumiwapo kwa kosa kubwa kama hili, bado, anayo haki ya kukataa na asilazimishwe wala kuvunja au kukiuka kipengele chochote cha sheria.
Kwanini sheria hutoa haki na upendeleo kwa wanandoa kutotoa ushahidi unaoweza kuwaumiza wenzao? Katika ndoa, wawili hulishwa viapo vya kulindana na kutunzana mbali na kuaminiana na kupendana katika kila jambo kwenye maisha yao ya ndoa hadi kifo kiwatenganishe. Japo si dini zote hutoa kiapo kama hiki, kuna chembe za kuapa katika kila ndoa; ziwe za kimila au za dini za kimapokeo.
Kiapo hulishwa wawili tu walioamua kwa hiari yao kuachana na familia zao na maisha yao ya kabla ya ndoa na kuishi pamoja kwa haki, upendo, na usawa. Kwa kulishwa kiapo, wawili mnatoka nchi kavu na kuingia kwenye mtumbwi wa pamoja ambamo mnasafiri wawili pekee yenu. Hivyo, mmoja akiutoba mtumbwi akidhamiria kumkomoa mwenzake, naye atajikomoa kwa vile mtazama wote. Usishangae. Katika kuzama huku mwenzio akapona nawe ukapotea.
Hivyo, wanandoa wajue kuwa kulindana na kuteteana siyo hiari, hisani, wala upendeleo, bali ni wajibu. Hii ni kutokana na ukweli kuwa kila wanachofanyiana, huwarudia. Kimsingi, kila wanachofanyiana, wanajifanyia wenyewe.