Profesa Bagadanshwa: Profesa aliyeshinda vikwazo vya kuwa mlemavu wa kutoona
Muktasari:
Ni profesa wa kwanza kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki Kati na Kusini mwenye ulemavu wa kutoona
Baadhi ya watu wenye ulemavu wanathibitisha kuwa ulemavu si kikwazo cha binadamu kutafuta haki ya msingi ya kupata elimu.
Tukiwathamini wenzetu wenye ulemavu na kuwajengea mazingira rafiki ya kujiendeleza kielimu, wengi wanaweza kufika mbali kielimu kama alivyo Profesa Edward Bagandanshwa wa Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa (Sekomu), aliyeipata hadhi hiyo ya juu kitaaluma hivi karibuni.
Profesa Bagandanshwa anathibitisha kuwa ulemavu si tiketi ya kukwepa elimu kama alivyohojiwa na mwandishi wetu.
Swali:Tueleze historia yako na namna ulivyopata ulemavu wa macho?
Jibu: Nilizaliwa mwaka 1959 katika kijiji cha Kaibanja Bukoba Vijijini, umbali wa kilomita 56 kufika Bukoba mjini. Ni mtoto wa pili katika familia ya Daudi Bagandanshwa na mkewe Apeneto Mbeoma. Nilipofikisha miezi sita baada ya kuzaliwa, nilikumbwa na maradhi ya surua na kwa kuwa wakati huo hakukuwa na chanjo, ikaharibu kabisa jicho langu la kushoto nikabaki na jicho moja la kulia.
Miaka saba baadaye wiki ambayo nilikuwa nimeandikishwa shule, nilikwenda kuchunga ng’ombe kama kawaida, ndipo mwenzangu aliporusha mshale na kunichoma jicho langu la kulia. Nilikimbizwa hospitali ya Ndolage na kufanyiwa operesheni kwa muda wa saa tano, lakini madaktari walisema nisingeweza kuona tena.
Swali: Ulipata ulemavu ukiwa tayari umeshaandikishwa shule, nini kilifuatia baada ya hapo?
Jibu: Ilipojulikana dhahiri kwamba sitoona tena, kanisa likaamua kuchukua jukumu la kufanya jitihada za kuhakikisha nakwenda shule. Aliyekuwa anashughulikia suala langu ni Dk Katabalo ambaye sasa ni marehemu. Huyu ndiyo chanzo cha mafanikio yangu, nimeazimia kwamba nitatenga siku niende angalau nikaione familia yake na Mungu atanisaidia kutekeleza hili.
Dk Katabalo alianza kufanya mipango ya kufuatilia shule tatu ambazo ni Buigiri ya Dodoma, Furaha ya Tabora na nyingine ilijulikana kwa jina la Iganga ya nchini Uganda. Waliojibu haraka maombi ya kunipokea ni shule ya Buigiri, hivyo mwaka 1968 nikawasili hapo nikisindikizwa na baba yangu.
Nilihitimu darasa la saba mwaka 1974 na katika darasa letu tulikuwa wanafunzi 10, wawili tukachaguliwa kujiujunga na Shule ya
Sekondari Mpwapwa.
Mpwapwa ni shule ya kawaida na ndani ya darasa letu, watano kati yetu tulikuwa ni wenye ulemavu wa kutoona. Mwaka 1978 tulihitimu kidato
cha nne name nikachaguliwa kwenda sekondari Mirambo Tabora.
Swali: Ikoje safari yako katika upande wa elimu ya juu?
Jibu: Mwaka 1982 nilijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nikisomea fani ya elimu na kuhitimu mwaka 1985. Nikarudi tena hapohapo kufanya shahada ya uzamili katika sayansi ya jamii, kabla ya kwenda Chuo kikuu cha Manchester, Uingereza kuchukua masomo ya udaktari wa falsafa mwaka
1994.
Darasa letu nchini Uingereza lilikuwa na wanafunzi 20 na mimi nikiwa mlemavu pekee. Hata hivyo tuliofanikiwa kupata shahada tulikuwa watatu, wengine tukawaacha.
Swali: Ili uwe profesa ni lazima pamoja na mambo mengineyo utoe machapisho ndani na nje ya nchi, unaweza kutaja baadhi ya machapisho uliyoandika?
Jibu: Machapisho niliyotoa ni pamoja na Teacher Education for Special Education in Tanzania lililotoka katika jarida la Journal of Issues and Practice in Education - JIPE (2004); Technologies
Deployed by Visually Impaired and Blind people in Tanzania to access Information katika jarida la Journal of Issues and Practice in
Education – JIPE (2006)
Mengine ni Models in staffing Special Education in
Tanzania jarida la Huria Journal, Vol.VI (2006); Advocacy Groups and Advocacy Activities in the education of the Visually Impaired and
Blind People in Tanzania, jarida la Journal of Issues and Practice in Education – JIPE (2006).
Machapisho mengine ni Counselling at the Workplace in Tanzania: What
can distance Education do? (Jarida la Huria Journal, Vol. 13); Partnerships and Collaborations in Educational Services for Visually Impaired and Blind People in Tanzania jarida la Tanzania
Journal of Special Education – TJSE (2014).
Pia nimeshiriki makongamano
mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.
Swali: Unauzungumziaje mtazamo wa wanajamii wengi kuhusu watu wenye ulemavu?
Jibu: Kwa kweli kuwa mtu asiyeona ni shida kidogo, jamii inamtazama kama mtu dhalili, asiyeweza kufanya chochote na ni wa kuhurumiwa na kusaidiwa daima.
Mtu mwenye ulemavu ukifanya kama wengine, unaonekana kama muujiza. Kwa mfano, mimi hata nikipendeza nikatoka na mke wangu,
wanamuuliza kwa nini uliolewa na huyu? Haya yanaingia hadi mahala pa kazi ukiwa na mafanikio wewe ni muujiza
Mfano mwingine kuna mkuu mmoja wa shule aliwahi kusema shuleni kwake ana walimu nusu akimaanisha walemavu wasioona. Hii ilimpa shida
kwani alilaaniwa kila pembe hadi akapoteza nafasi hiyo.
Aidha, liko suala la walemavu kutopewa nafasi katika ajira. Hili linakwenda kinyume na sheria namba mbili ya ajira. Inatakiwa mahali pa kazi angalau asilimia mbili wawe ni watu wenye ulemavu.
Kamishna wa ustawi wa jamii angeweza kufanya ukaguzi kuona kama linatekelezwa. Hakuna taarifa wala ushahidi kama sheria inavyoagiza ndivyo inavyotekelezwa.
Swali: Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa kinatajwa kuwa cha kipekee nchini, kwa nini?
Jibu: Upekee upo katika mambo mbalimbali mojawapo ni katika eneo la kuandaa wataalamu wa ngazi ya juu wanaowahudumia watu wenye ulemavu.
Kihistoria hapa nchini ulikuwa unaishia ngazi ya stashahada kwa wasioona pale Chuo cha Patandi au nje ya nchi, lakini chuo hiki sasa kinatoa
shahada ya kwanza na ya uzamili. Sekomu kimekuwa cha kwanza Afrika Mashariki kuanzisha shahada ya uzamili katika fani ya elimu maalumu.
Fani nne zinatolewa hapa ambazo ni ukiziwi, kutoona, ulemavu wa akili na fani ya ulemavu katika kusema na lugha.