Magdalena Sakaya; Afichua sababu ndoa za wabunge kuvunjika
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya amewashauri wanawake wanaoingia kwenye ubunge kuhakikisha wanapangilia muda wao, ikiwamo kuzingatia familia kwa kuwa ndiyo kila kitu katika kazi zao.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Jarida la Familia, Sakaya anasema ‘ubusy’ ukizidi katika familia, ndoa ikivurugika hakuna kitu utakachoweza kufanya vizuri.
Anasema baadhi ya wabunge wanawake wanapopata ubunge husahau kuhudumia familia, akiwamo mume, bila kufikiri kuwa, nyuma ya mafanikio ya mwanamke kuna mwanamume.
“Wapo wenzetu baada ya kupata ubunge waliwadharau waume zao, hadi ndoa zao zikavunjika, lakini namshukuru mume wangu alifanya utafiti wake kwangu na hakuna alichobaini kuhusu mimi,” anasema Sakaya, ambaye amewahi kuwa mbunge wa viti maalumu mkoani Tabora kwa miaka 10.
Sakaya anasema wakati akiwa mbunge ilifika mahali mumewe akaanza kuwa na wasiwasi baada ya kujazwa maneno na watu, kwamba hana mke, “kutokana na mimi kutingwa kila mara na majukumu, kwa hiyo alihisi nina mchepuko.”
Je, anagawaje muda wa kazi na familia?
“Angalau sasa napata nafasi ya kukaa na familia, wakiwamo wazazi wangu, kwa kuwa nina muda ukilinganisha na kipindi cha nyuma, kiukweli sio kazi ndogo kuwatumikia wananchi hasa ukiwa na kiu ya kila jambo liende unavyotaka ili kuwaletea wananchi maendeleo,” anasema.
Sakaya, ambaye ni mwanasiasa mkubwa, anasema majukumu yake sio madogo, ingawa kuna unafuu kwa kuwa yupo nje ya Bunge tofauti na zamani.
Naibu katibu mkuu huyo wa CUF aliyewahi kuwa mbunge wa kuchaguliwa kwa miaka mitano Jimbo la Kaliua, anasema awali alikuwa akionana na familia yake siku chache kwa wiki kutokana na kukitumikia chama.
Anaonaje malezi ya watoto?
Sakaya, mwenye mtoto mmoja, anasema katika malezi ya sasa inasikitisha kuona mtoto hata kupika chai hajui, lakini enzi zake akiwa na miaka sita alikuwa akijua kupika chakula cha familia ya watu watano.
“Kiukweli malezi ya sasa hivi sio kabisa, kila kitu kinafanywa na msichana wa kazi, mwisho wa siku watu wakienda kuanzisha familia zao wanashindwa kutekeleza majukumu yao ya kifamilia na kuwa chanzo cha ndoa nyingi kuvunjika mapema,” anasema Sakaya.
Pia, anasema hivi sasa watoto wakienda kwa mtu wakipewa kazi wanaona wameonewa na hili ndilo linasababisha kuwa tegemezi pindi wanapomaliza shule, kwa kuwa wanategemea wamalize shule na kuajiriwa, wakikosa ajira hakuna kazi wanazozijua.
Hata hivyo, anawataka wazazi kurudi kwenye maadili ya watoto wao, kwa kuwa anachokiona kuna bomu kubwa linatengenezwa, huku akisema watoto wengi walioharibika ni kuanzia waliozaliwa miaka ya 1980 na kuendelea.
“Imefika mahali mtu mwingine huwezi kumuadhibu mtoto wa mwenzake kwa kukosea, kila mtu anaogopa kumuadhibu mtoto, wakiwamo walimu, kiukweli haya sio malezi,” anasema Sakaya.
Kwa nini kuna ukatili ndani ya familia?
Akizungumzia kukithiri kwa matukio ya kikatili ndani ya familia, Sakaya anasema chanzo ni kukosekana kwa mbegu ya upendo kuanzia kwa wazazi.
Anasema matokeo yake kukosekana mbegu ya upendo, kunahama na kuhamia kwa watoto na mwisho wa siku wanaona ni maisha ya kawaida.
Ili kukabiliana na vitendo hivyo, anasema madawati yanayoshughulikia malalamiko ya kesi za ukatili yawezeshwe kifedha na kusikiliza kesi hizi kwa wakati, lengo likiwa ni kuleta suluhisho.
Sakaya anasema wale wanaoshiriki kuwabaka au kuwalawiti watoto, sheria kali zichukuliwe, ikiwamo kuwahasi, jambo litakalosaidia wasiharibu wengine na wanaotaka kufanya hivyo kuogopa.
Kiongozi huyo wa CUF anasema zile kesi wanazosema ndugu wameamua kulindana na kukosa ushahidi, Serikali iingilie kati kuwashtaki kama zilivyo kesi nyingine za mauaji, kwa kuwa bila kufanya hivyo matukio hayo yatendelea.
Maisha yake ya utoto yalikuwaje?
Sakaya akiwa mtoto wa kwanza katika familia, anasema kauli ya baba yake aliyokuwa akiitoa mara kwa mara kuwa yeye ni lango la familia na akianguka familia nzima imeanguka wakiwamo wadogo zake ndiyo imemfikisha hapo alipo.
Sakaya anasema akiwa shule ya awali kisha msingi, hakubahatika kusoma vizuri kama watoto wengine kutokana na kuwa na jukumu la kuwalea wadogo zake wakati baba na mama wakiwa wanaenda kwenye mihangaiko ya kutafuta pesa.
Wakati huo anasema baba yake alikuwa ni mkulima, mama yake alikuwa akiuza kinywaji aina ya mbege.
Sakaya anasema alipofika umri wa kuanza shule, mama yake alimtaka kulea wadogo zake na hakutaka kusikia habari za shule na alipoona ana kiu sana ya kwenda, alimpa masharti kuwa kama anataka hivyo basi aende na wadogo zake.
“Mama aliniambia kama nataka kusoma niende na watoto kwa kuwa hana wa kumwachia akienda kwenye shughuli zake za biashara ya kuuza pombe,” anasema Sakaya.
“Katika wadogo zangu hao, mmoja alikuwa na miaka miwili na mwingine miake minne, hivyo wakati wa kwenda shule mmoja nilikuwa nikimbeba mgongoni na mwingine miaka minne namshika mkono anatembea mwenyewe hadi shule.”
Utaratibu huo wa kwenda shule na wadogo zake, anasema alianza nao tangu akiwa chekechea aliposoma miaka miwili kisha kwenda darasa la kwanza Shule ya Msingi Kombo iliyopo Kibosho.
“Hivyo nilipokuwa darasani wadogo zangu nikawa nawaacha nje wanacheza, wakilia natoka kwenda kuwabembeleza, na ikifika muda wa mapumziko wenzangu wakienda kucheza mimi naenda kuwanywesha uji,” anasimulia Sakaya.
“Hali hii ilinifanya nisijue michezo yoyote shuleni, kwa kuwa wakati wenzangu wanakwenda kucheza, mimi nikawa busy na watoto.”
Hata hivyo, alipoingia darasa la pili, anasema walimu wake waliona juhudi zake katika kuitaka elimu hiyo na kwenda kuzungumza na mama yake na kumwambia kuwa mtoto wake ana akili lakini hana muda wa kupumzika na kumuomba ampunguzie majukumu ya ulezi kwa kuwa akifika shule anaonekana amechoka pia.
“Kwa kuwa na watoto walikuwa wameshasogea umri na kuweza kubaki wenyewe, nikaanza kwenda mwenyewe shuleni, lakini nikirudi majukumu ni yaleyale, niwapikie watoto, kupika chakula cha familia na kufanya shughuli zote za usafi kabla na baada ya kutoka shule,” anasema Sakaya.
“Nilipambana kwa hali hiyo hadi nikamaliza darasa la saba lakini kwa bahati mbaya katika mtihani wa mwisho wa Taifa shule nzima hatukufaulu.”
Pamoja na hilo, kwa kuwa baba yake aliziona jihudi zake za kupenda kusoma, alimuahidi kuwa atampeleka shule ya kulipa na mwaka 1987 akampeleka Shule ya Wasichana Kibosho.
“Nashukuru baba alitekeleza ahadi yake hiyo ya kunisomesha na kila nilipofaulu mtihani alinipa zawadi, hivyo kuzidi kunipa moyo wa kusoma na katika mtihani wa kidato cha nne nilifaulu na kupata daraja la pili na kupangiwa Shule ya Msalato mkoani Morogoro.”
Alipomaliza kidato cha sita alipata daraja la pili, lakini hakutaka kwenda moja kwa moja chuo na kuomba akasome masuala ya mifugo Chuo cha Mifugo Tengeru, kwa kuwa ni kazi aliyoipenda.
“Nilipomaliza chuo nikaenda Dar es Salaaam, kufanya kazi ya fani hiyo kwa miaka miwili, lakini nikaona hailipi, nikaamua kwenda kujiendeleza Chuo Kikuu cha Sokoine mwaka 1998 na kusoma masuala ya wanyamapori,” anasema Sakaya.
Safari yake kuingia kwenye siasa
Sakaya anasema baada ya kumaliza Chuo cha Sokoine alipata kazi kwenye Shirika la Denmark linalojishughulisha na wanyamapori Kaliua na alifanya kwa miaka mitano kuanzia 2001 hadi 2005.
“Nikiwa huko nikawa nawaelimisha watu kuhusu faida za wanyamapori na namna ya kuweza kuishi nao vizuri na katika majukumu yangu, nikajikuta nafanya kazi na watu mbalimbali, wakiwamo madiwani na wabunge,” anasema Sakaya.
“Pia, nikawa nafanya shughuli nyingi za kijamii, ikiwamo kujenga madarasa, kazi ambayo ndio ilinisababisha nikasogea karibu na wanasiasa na wananchi kunikubali.”
Sakaya anasema wanasiasa hao waliona baadhi ya mambo alikuwa akiwatatulia na mengine yalipaswa kufanywa na wabunge au madiwani wao, hapo ndipo safari ya kushawishiwa kuingia kwenye siasa ilipoanza na mwaka 2000 akaamua kuchukua kadi CUF na kukaa nayo kwanza.
“Niliamua kuchukua kadi kwenye chama hicho kwa kuwa kimekuwa kikizungumzia masuala ya haki, mimi pia ni muumini mkubwa wa masuala ya haki.
“Ilipofika mwaka 2004, CUF wakaniomba nigombee nafasi ndani ya chama na ilipofika mwaka 2005 niliteuliwa kuwa mgombea viti maalumu nikiwa nipo kazini, walitaka nifanye kazi kotekote, lakini niliwaomba nifanye sehemu moja ili niweze kufanya vizuri zaidi kwa kutatua changamoto za wananchi,” anasema Sakaya.
Anazungumziaje nafasi za 50 kwa 50
Sakaya anasema nafasi za 50 kwa 50 katika uongozi nchini kwa sasa sio mbaya kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameweza kuwapa nafasi nyeti wanawake na sasa Tanzania imefikia asilimia 34, ingawa haijafikia Rwanda ambao wao wapo kwenye asilimia 55 na Uganda zaidi ya asilimia 40.
“Tumefikia huku kwa mchango wa Rais Samia, ameanza kuwarudisha wanawake katika nafasi mbalimbali tofauti na hapo nyuma walikuwa wakitolewa wanawekwa wanaume,” anasema Sakaya.
“Ni vizuri mama akiendelea na utaratibu huu kwa kuwa tukiweka wanawake wengi katika hizi nafasi za teuzi ni wazi Taifa litafika mbali, wanawake ni watu wanaopenda kuitendea haki nafasi wanayopewa na hili litawezekana kama tukianzia ndani ya vyama.”
Sakaya anasema changamoto ni baadhi ya makabila, yanapaswa kuondokana na dhana potofu kuwa mwanamke hawezi kuwaongoza, japokuwa kuna maeneo yameanza kubadilika taratibu huku akitoa mfano walipotoka wabunge Ester Matiko na Ester Bulaya, “katika mkoa ambao ulionekana hawaamini katika kuongozwa na mwanamke.”
Ndani ya chama chao, Sakaya anasema hili la 50 kwa 50 pia wanalizingatia, kwa kuwa kwenye baraza lao lazima robo ya wajumbe wawe wanawake.
Anasema kwenye bodi yenye watu tisa, kati yao lazima wawe wanawake, kamati ya utendaji ya Taifa nako kuwa watu 25, robo tatu ni wanawake, vivyo hivyo kwa kamati za wilaya hadi kata uwakilishi huo unafanyika.
Pamoja na nafasi hiyo waliyopewa wanawake ndani ya chama hicho, anasema kuna changamoto bado, ikiwamo wanawake wenyewe kutojiamini kama wanaweza kuongoza, hivyo kujikuta wakitumia nguvu kuwalazimisha kuwa viongozi.
Anafanya nini kwa sasa?
Baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Sakaya amejikuta akiwa nje ya bunge, uchaguzi ambao vyama vingi vya siasa viliulalamikia kwa madai haukutenda haki.
Sakaya anasema kwa sasa mbali ya kutumikia chama chake, anajishughulisha na kazi za kufuga samaki, kuku na kulima mazao ya mahindi na alizeti mkoani Morogoro.
Hata hivyo, pamoja na kuwa nje ya bunge, Sakaya anasema bado anapokea kero za wananchi na kuzishughulikia kwa kuwa anajuana na viongozi mbalimbali.
Akitolea mfano wa hivi karibuni, anasema alitatua tatizo la wananchi kutokuwa na umeme ndani ya wiki saba.
Pia, akiwa nje ya majukumu na kuwa huru vitu anavyopenda kufanya anasema ni kuimba kwaya na anaimba sauti ya nne.
Atarejea katika ubunge?
Licha ya mwaka 2020 haukuwa bahati kwake kuwa mbunge, Sakaya anasema hajakata tamaa kwa kuwa moyo wa kutetea wananchi bado anao na kuahidi mwaka 2025 atarudi ulingoni tena.
“Kama mnavyoona sasa Rais Samia amerudisha demokrasi, nina imani hata uchaguzi wa mwaka 2025 utakuwa huru na wa haki kwa wananchi kuchagua viongozi wanaowaona wanawafaa na sio kuwekewa watu na mimi sioni haja ya kutojitupa ulingoni tena kwa mara nyingine,” anasema.
Sakaya anatumia nafasi hiyo pia kukishukuru chama chake kuendelea kufanya mikutano ya hadhara, jambo analosema litasaidia kuwarudisha kwenye amsha amsha ya kisiasa wanachama na wananchi kwa jumla kwa kuwa wengi walishaonekana kukata tamaa.
Anawaahidi wananchi wa Kaliua na Tabora kuwa bado anawapenda na kuwaomba waenzi mazuri aliyoyafanya wakiwa pamoja na kuongeza kuwa itakapofika 2025 wasimtupe.