Ndani ya boksi: Ney wa Mitego atupwe selo tu! Tumemchoka...

Ney wa Mitego

Ni hivi. Kuna dada muda huu yupo hospitali akiongea kwa siri na daktari amtoe mimba. Na dada mwingine yupo chumba cha pili akiomba daktari amsaidie, kwani ni mwaka wa saba huu hajapata mtoto.

Na kuna mwanadada mida hii yupo sehemu anatia saini kwenye hati ya talaka, kuwa haitaki tena ndoa yake. Lakini mida hii pia kuna mwanadada yupo kanisani, kapiga goti chozi jingi likimtoka akiomba Mungu ampatie mume. Ninachojaribu kusema hapa ni kuwa, kila mwanadamu na kila kitu duniani kina upande wake wa pili wa maisha. Unaweza kuwa na hiki, lakini huna kile alichonacho mwingine. Ukiachana na Sugu, Profesa Jay na mwanaFA. Ambao ubunge wao ni kigezo tosha kwamba wanajua kujieleza. Pia kuna wanamuziki wengi nchini wanaojua kujieleza. Na pia kuna wasanii wengi ambao linapokuja suala la kujieleza hugeuka mtihani kwao.

Afande Sele pamoja na udhaifu wake mwingi alionao, lakini mwamba ni mmoja kati ya wasanii wanaoweza sana kujieleza, kufafanua jambo na likaeleweka. Kabla hajapata ustaa mitaa ya Moro aliitwa Radio One, kutokana na kuongea sana, kiasi kwamba anaweza kukupiga kamba ukashawishika kumsikiliza na kumuamini. Uliza watu. Ule uwezo wa mtu kupokea, kuchambua, kuchanganua. Na zaidi kutafsiri na kulielezea jambo kwa lugha inayoeleweka. Unaweza kuwa na kipaji cha kuandika na ‘kufloo’ kama Fid Q, lakini likija suala la kujieleza ukawa sifuri kabisa. Jambo moja ambalo wengi hawajui ni kwamba kuongea ni ujuzi, kipaji na akili kama vipaji vingine. Siyo kitu chepesi kabisa. Wapo watu wenye heshima na wengi ni viongozi wakubwa. Lakini wakipewa nafasi ya kuongea ni ziro, utawaonea huruma. Na pia unaweza kuziba masikio kwa aibu unayosikia kutoka kwao. Ndio maana siyo wote ni wachungaji, wanasiasa, washereheshaji au wachambuzi. Kwa sababu vitu hivyo vyote vinahitaji watu wanye uwezo wa kupokea, kuchambua, kutafsiri, kuelezea na kufafanua jambo lolote. Tena kwenye nyomi la watu.

Uwe na utulivu wa akili, mitambao ya mwili, mikato ya sauti pindi ukiongea na uso wako wakati ukiwasilisha jambo. Utajiri wako wa ‘kontenti’, na kuunganisha matukio na visa. Na uwezo mkubwa wa kutetea hoja yako, yaani uwe ‘fulu pakeji’.

Wengi hawana uwezo wa kuelezea jambo hata kwa dakika tano au kumi. Atakutia aibu na heshima ikashuka. Ndiyo maana wenye akili zao huwa na wasemaji. Ambao michongo yao ni kufafanua, kujibu hoja na maswali na kuelezea mambo kindakindaki. Kwa ‘Madoni’ wenye heshima ‘tauni’. Wanaojifahamu kuwa siyo waongeaji wazuri, hutoa dili la usemaji kwa wana wanaolingana nao kiheshima. Siyo staili zile za Baba levo, Mwijaku na wenzao. No! Usichanganye mada hapa, sina maana hiyo.

Fid Q ni mmoja wa wasanii ambaye hana uwezo wa kuzungumza. Licha ya uwezo mkubwa wa kuchana na kuandika. Lakini ukitaka aongee na wana utakuwa unampa mzigo mzito sana. Kumbuka ‘ishu’ ya ‘Tivu ake’. Unaweza usimuelewe kutokana na lugha anayotumia pengine. Na wapo walioamua kumuweka kwenye daraja lao. Lakini Chid Benz anaweza sana kuzungumza, kuelezea na kuchambua jambo. Amekuwa rafiki wa maiki za vitivii vya ‘onlaini’, kwa sababu hiyo. Mbali ya ukali wake wa kuchambua masuala kadhaa. Pia ni bingwa wa majibu ya papo kwa papo, usipokuwa makini anakutoa nishai. Kichwani yuko vyede. Mengine ni mapito tu.

Kuna Mondi. Huyu pia ana uwezo wa kujieleza na kufafanua jambo. Anazo akili za kuzungumza mbele ya kamera. Huwezi kuona kazinguliwa na swali la mtu. Ana utulivu sana akiwa kwenye ‘tempa’ ya kueleza mambo yanayohusu kazi au biashara yake. Kuna Jaydee na Alikiba, mara kadhaa wamekiri, kwamba suala la kujieleza hawawezi. Pia Jide aliwahi kusema kuwa hata siasa anashindwa kwenda nazo sawa kwa sababu hiyo. Mambo ya kufafanua sana ‘ishu’ hawezi. Wamuacheee! Majani zamani hakuwa mwepesi wa kufanya mahojiano. Lakini miaka ya karibuni amekuwa mtu wa kuongea mara kwa mara. Huyu ni prodyuza mwenye uwezo mkubwa wa kuzungumza jambo akaeleweka. Hata Master Jay pia yuko vizuri sana. Na kuna mwamba hapa ambaye hubebwa na tabia ya kuongea sana kwenye nyimbo zake. Lakini sijajua kama ana uwezo huo huo katika kufafanua mambo yale kwa uwezo mkubwa nje ya studio. Namuongelea Ney wa Mitego. Jamaa yuko poa kwa asilimia kubwa. Kwenye kufafanua yaliyo ndani ya uwezo wake, fani yake ama jamii yake. Yuko tofauti na wasanii wengi wa sasa hivi. Kuna wakati unaweza ukajiuliza Ney anatafuta pesa, sifa au basi tu? Ngumu sana kumuelewa. Kama pesa wanazo kina Mondi na hawaimbi anachoimba Ney. Kama ni umaarufu mkubwa wanao ambao hawaimbi anachoimba Ney mara kwa mara. Sasa Ney yeye anaimba ili apate nini? Wanaotaka kumkamata haraka kamateni huyo. Wabongo hawataki anachoimba Ney. Ndio maana mitandaoni stori kubwa ni Mbosso na Konde Boy. Huyu Ney anayejiita Sauti ya Watu, watu wa wapi? Mbona hatuoni ‘vyuzi’ ‘yutyubu’ za kutosha kwake kama zile za wale wanaojiimbia mapenzi miaka yote? Tangu Konde Boy atoke kisanii, lini aliimba ngoma kali nje ya mapenzi? Lakini kwa mangoma yake hayo ya mapenzi kidogo azawadiwe ubunge awamu iliyopita. Ina maana walijua kuwa mwimba mapenzi ndio rahisi zaidi kuwakilisha jimbo. Sasa Ney yeye vipi? Kamateni huyo. Kwenye wimbo anatuuliza eti yupi muoga, mtawala aliyezuia kufanya mikutano ya siasa. Au wapinzani wasiofanya mikutano huku wakijua ni haki yao? Kwa maneno haya nani wa kusikiliza huu wimbo? Nani wa kuupenda na kuufuatilia? Huyu dogo akamatwe. Kama kweli kuna watu wanataka kumdaka watakuwa sahihi sana. Na mimi nitawapongeza, kwa kuwa sioni mantiki ya wimbo huo. Wabongo sisi tunataka msanii anayetoa ngoma za mapenzi, anayetupa maujanja ya kumiliki pisi kwa wingi.

Kimsingi shida zetu ni kuona mabango ya mapenzi barabarani na mabusu mitandaoni. Tunataka kuona viuno vya Zuchu na Mondi wakikata jukwaani. Fujo za Konde na Kajala, hizo ndio shida zetu sisi. Sasa kelele za Ney zinaturudisha enzi za Mtikila na sera za Gabachori. Kwa nini asidakwe? Kamateni huyo. Eti kuna sehemu anasema mabinti hawana ajira kazi yao kudanga. Hao mabinti wa wapi wanaowaza ajira? Wakidanga inamuhusu nini? Kwanza mabinti zetu hawana shida za ajira, wao wape bando wasome umbea wa Mange.

Binti zetu wape ‘smati foni’, kifurushi na pozi wafuatilie penzi la Paula. Wasikie kelele za chawa wanaosifia watu na ‘koneksheni’ za ngono. Hizo ndio shida za watoto wa kizazi hiki, sasa yeye sauti ya watu wa wapi hao? Huyu ni wa kukamatwa tu.

Kama kweli kuna mtu anataka Ney akamatwe, namuunga mkono. Hata mimi sivutiwi na mtu anayeimba au kuongea vitu ambavyo siyo shida zetu, vijana tunata kujua penzi la Wema na Whuzo.

Shida zetu Wabongo kidoogo labda maamuzi ya ovyo ya marefa wa ligi kuu. Siyo mgao wa maji, umeme wala bei za luku. Anapojiita sauti ya watu, hao watu gani? Twende ‘yutyubu tuone kipi kinafuatiliwa zaidi kati ya ‘Sauti ya Watu’ na ‘Mapenzi Yataniua’.

Ney analalamika kuwa kodi zetu ndio zinafanya viongozi wanunue ‘Vieite’. Hizi ni chuki zake tu, mbona kina Mondi na Konde, wanamiliki ‘vieite’ kwa kuimbia watu mapenzi? Sasa yeye badala ya kuimba mapenzi apate ‘vieite’, anaishia kusuta watu. Kamateni huyo.

Ukitaka kujua shida za Wabongo. Wachukue Ney na Konde, washushe mtaani. Waambie kila mtu agonge ngoma zake kalikali. Atakayeondoka na kijiji ndio utapata jibu kwamba hivi shida za Wabongo ni umeme, maji na ajira au shida yao ni mapenzi tu?

Kibaya zaidi wataanza kutaja na jina la Kajala wakimuomba Konde Boy aipandishe babe yake. Sisi shida zetu ni mapenzi, mengine ni kiherehere tu cha kina Ney wa Mitego. Watanzania hatutaki mambo magumu magumu ambayo hayana maana. Ney anashangaa shida kibao lakini wapinzani wamekaa kimya. Mbona hakushangaa Wabongo kukaa kimya, wapinzani walipokaa jela? Ndio ujue wapinzani nao wamejua shida za Wabongo ni mapenzi siyo maji, ajira, umeme, katiba mpya wala rushwa.

Wimbo wa Ney haufai kwa kizazi hiki cha bata batani. Wakitaka kumdaka wafanye fasta. Sisi zetu ni singeri zinazotupa mzuka wa kusaka totozi. Na ngoma za kubembelezea mibebezi. Ajabu mastaa wa kizazi hiki wote wanagonga ngoma za mapenzi. Yeye sijui katokea wapi? Mimi nashangaa anafanya nini mtaani mpaka sasa? Kamateni weka selo huyo.