ONGEA NA AUNT BETTIE: Nimemlea mwanaye, anirudishie gharama

Nilimuoa mwanamke aliyekuwa na mtoto wa miaka miwili. Nilimuuliza kuhusu baba wa mtoto akasema alimkataa.

Licha ya mimi kuzaa naye, watoto wote niliwapa haki sawa na wengine na sasa yupo kidato cha tatu, baba yake halisi anamtaka.

Naomba nisaidie ushauri kwa sababu sitaki amchukue kwa kuwa alimkataa nikamlea, ikitokea akamchukua nataka anirudishie gharama zangu za matunzo kwa miaka zaidi ya 15 niliyomlea kama mwanangu nikimgharimia kila kitu.

Pole na hongera kwa kuwa na moyo wa kujali. Kwanza kabla sijakushauri ulipaswa uniambie mkeo anasema nini katika hilo, yeye ndiyo muamuzi wa mwisho. Nasema muamuzi wa mwisho kwa sababu ndiye aliyekuambia baba wa mtoto kamkataa, sasa aseme hadharani kuwa ulimkataa sikupi mtoto na si wako kama ulivyosema mwenyewe hapo awali.

Au ndiyo ni mwanaye lakini simpi au nampa kwa sababu hii na ile. Tofauti na hapo atakuwa ana mawasiliano naye na ndiyo sababu ya ukimya wake.

Ushauri wangu ni kuwa mtoto hang’ang’aniwi, mtambana mnavyoweza kwa kuwa kuna maneno maneno ya baba yake halisi kumtaka atamtafuta tu hata iweje, akikutana na mambo tofauti na malezi yako atarudi. Mwingine atakupenda na kukuheshimu, lakini bado atakuwa na mawasiliano mazuri na baba yake na siyo mapenzi kama aliyonayo kwako.

Pia, siku nyingine likitokea jambo kama hilo, lifanye kisheria. Ungekuwa umemlea huyu mtoto kisheria kwa maana ya kumuasili asingekuletea haya maajabu ya kukitaka ulichokikataa.

Ombi langu ni kuwa usijali sana kuhusu gharama ulizotumia, huyo binti atabaki kuwa mwanao tu siku zote kwa sababu mapenzi yake kwako yatabaki palepale.

Kwa sababu ukifanya vitu kwa kumkomoa huyo mwanamume kutokana na tabia yake mbaya, utajiharibia, msukumie Mungu na ukizingatia ana ndugu zake uliozaa na mama yake, hivyo bado ni mwanao.


Hanitaki, lakini haachi kuwasiliana na ndugu zangu

Namshangaa huyu mwanamke, ninapompigia simu hapokei, wala ujumbe mfupi hajibu. Lakini cha kushangaza kutwa anachati na kuwapigia simu ndugu zangu huku akijidai hakuna tatizo kati yetu.

Nakiri kweli ilitokea sintofahamu baina yetu ambayo tulishindwa kufikia muafaka akaamua tuachane. Nimejaribu kumbembeleza kadiri ya uwezo wangu, lakini akakataa katakata, licha ya kujaribu mara kadhaa kumpigia simu na kumtumia ujumbe hajibu. Anavyowasiliana na ndugu zangu huku mimi ananipotezea naona kama ananidharau na nimeamua kuendelea na maisha yangu.

Nishauri niende ofisini kwake kumueleza aachane na ndugu zangu, maana aliwajua kupitia mimi.


Haina haja kwenda ofisini kwake kumueleza lolote, huyu bado anakupenda ila ana hasira za mlichogombania ndiyo maana anashindwa kumalizana na wewe. Mtu asiyekupenda hawezi kuwajali ndugu zako hata siku moja. Mpe muda tu, hata hao ndugu zako anajipanga kuwaeleza ili mkutanishwe mmalize changamoto yenu, usichukue maamuzi ya hasira. Nakukumbusha asili hasa ya mwanamke anapenda kubembelezwa, kama hapo awali ulikuwa humfuatilii sasa amepata nafasi ya kuliona hilo. Niamini mimi bado anakupenda, wala usimkatie tamaa.

Kwanza hujasema ulimfanya nini, labda ulimpiga tukio kubwa kiasi anakupenda lakini anasita kukusamehe maana hajui kitakachokuja baadaye.