Raha, karaha ya ndoa kwa wanafunzi vyuoni

Achana na uhusiano wa kihuni unaochangia kuwapo kwa ziitwazo ndoa za rejareja kwa wanafunzi wengi wa vyuo vya elimu ya juu.

Unajua kama vyuo hivyo ni maeneo ya watu kupata wenza? Kwa baadhi ya wanafunzi, uhusiano wao huwa ni wa dhati kiasi cha kufikia kufunga ndoa za maisha wakiwa masomo.
Je, kitendo hicho ni raha karaha? Mwananchi linaangazia ushuhuda wa baadhi ya watu walioptia hali hiyo wakiwa wanafunzi.Simulizi ya Shabani Omar

Katika simulizi ya maisha yake, mkazi wa Dar es Salaam na mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shaaban Omari, anasema haoni ubaya wa aina yoyote kwa watu kuoana wakiwa chuoni kwani tayari wanakuwa ni watu wazima wanaoweza kufanya uamuzi wa maisha yao.

Shaaban anasema maisha ya chuo na ndoa hayana tatizo kwa watu waliopendana kweli, ingawa anakiri kuna changamoto nyingi za majaribu.

“Mimi nilioa nikiwa mwaka wa tatu na mke wangu alikuwa mwaka wa pili sote tulikuwa wanafunzi wa ualimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,maisha ni mazuri na hayana changamoto zozote,” anasema Shaaban.

Anamtaja mke wake Dk Mboni Ruzegea (Mkurugenzi wa Maktaba Tanzania) waliyeanza naye maisha wakiwa vijana hadi sasa wamejaliwa kuwa na watoto wanne ambao watatu wako ngazi ya vyuo vikuu.

Omari, ambaye ni mtaalamu wa lugha ya Kiingereza akiwa na sifa ya kufundisha maelfu ya wanafunzi nchini, anaeleza namna safari yao ya kindoa na mkewe ilivyoanza kutoka kukataliwa na wazazi wa upande wa mwanamke, kubezwa na kuzodolewa na wanafunzi wenzao hadi kuishi chumba kimoja cha kupanga.

Lakini kikubwa zaidi ni namna maisha yao yalivyowavutia wengine kiasi cha kuwafuata na kuwaomba ushauri.

“Wazazi wangu walibariki hilo, waliniamini na kunipa nafasi ya kuchagua ingawa walijua bado sina uwezo wa kujitegemea, lakini wazazi wa mwenzangu waligoma kabisa japokuwa mtoto wao aliweka msimamo kwangu,”anasimulia.

Anasema kuwa maisha hayakuwa magumu sana, japo alilazimika kuchangamka zaidi katika utafutaji, kwani alishakuwa na familia.

Akaanza kujibidiisha kwa kufundisha kituo cha Magomeni Lions Club ambako alikuwa anapata fedha za kutosha.

Anaeleza jinsi alivyogeuka pia kuwa msaada kwa mke wake ambaye wakati huo alikuwa mwanafunzi, lakini tayari akawa mjamzito na kisha kulea mtoto hivyo ilikuwa lazima amsaidie kwenye masomo ili asikwame. Jambo la kutia moyo kwa wenza hao lilikuwa ukweli kuwa wote walikuwa wakisoma kozi zinazofanana, hivyo ilikuwa rahisi kusaidiana kwenye masomo na hatimaye wote kuhitimu wakiwa na alama za juu kwenye ufaulu.

Anasema kwa sehema kubwa gharama za maisha yao zilitegemea fedha walizokuwa wakipata kutoka serikalini, huku yeye akiongeza mfuko kupitia ufundishaji.

“Wazazi mara zote wanakuwa ni changamoto kwa watoto, utakuta upande mmoja unakuja na hoja dhaifu kuwa kijana bado hana kazi kwa hiyo binti ya atapata shida, bila kujua hata wenye kazi unafika wakati wanakosa kazi na maisha yanakwenda kombo, tuache hayo,” anasisitiza.

Hata hivyo, Omari akikumbukia baadhi ya changamoto alizopitia, anaonya kuhusu tabia ya baadhi ya wanavyuo wanaoanzisha uhusiano kwa ajili ya kutimiza mahitaji ya mwili na tamaa.

‘’Baadhi ya marafiki zangu waliamua kuanzisha uhusiano na wengine walifaulu hadi leo wanaishi na wake zao wakiwa watu wazima na familia,’’ anaeleza.

Ili kuepuka hayo, anasisitiza vijana waingie katika uhusiano usiokuwa wa majaribio, kwani hakuna zuio la kuoa au kuolewa kwa mtu anayesoma.
 

Simulizi ya Mwalimu Rehema Enock

Mwalimu Rehema Enock, alihitimu masomo yake mwaka 2017 katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom). Anasema zipo raha na karaha kwa wanafunzi kuwa ndani ya ndoa wakiwa masomoni.
Rehema anayefundisha mojawapo ya shule katika halmashari ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, alifunga ndoa akiwa mwaka wa kwanza wa masomo huku mumewe akiwa mwaka wa mwisho wa masomo ya udaktari.

Tofauti na ndoa ya Shabani Omari na mkewe waliokuwa chuo kimoja, wawili hawa walikuwa katika vyuo viwili tofauti, lakini anasema hakuna kilichoharibika, kwani malengo ya ndoa yao yalitimia kama walivyotarajia.

“Kikubwa ni malengo na kujiheshimu, lazima utambue kuwa unabeba majukumu mawili kwa wakati mmoj. La kwanza ni masomo na la pili ni kama mke au mume wa mtu, na kwangu nilifaulu yote, namshukuru Mungu,” anasema Rehema.

Anasimulia kuwa wanafunzi wenzake na hata wahadhiri, walijua kuwa anasoma wakati ameolewa hivyo kuna mahali heshima iliongezeka na hawakupenda kumchanganya katika makundi yao.

Hata hivyo, anataja changamoto aliyokuwa akikutana nayo, ni suala la unyonyeshaji kwani ilibidi wakati mwingine akae darasani hadi usiku akiwa na mtoto mdogo anayetaka kunyonya.

“Masomo ni muhimu lakini mtoto ni muhimu zaidi, je hapo unawezaje kujigawa na ukifanya mchezo unakuta umeumia kwa pande zote,lakini ilikuwa ni uvumilivu na maamuzi,” anasema Rehema.

Kuhusu ushauri wake kwa wanafunzi wa vyuo kuoana wakiwa masomoni, anasema hakuna ubaya kama wataamua kwa malengo, kuliko kuishi kinyumba halafu mwisho wa masomo wanaachana.
 

Wasemavyo wengine

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha St John's cha jijini Dodoma, Fredrick Golden anasema suala la wanafunzi wa vyuo vikuu kuishi kama wanandoa, lipo ingawa anakiri kuwa lina raha na karaha zake.

Anataja makundi mawili ya wanavyuo wanaoweza kuishi na wenza wao. Kundi la kwanza ni wanaotoka kazini akisema wana haki ya kuoa au kuolewa. Kundi jingine ni la wanaotoka shuleni moja kwa moja ambao kwake anaona ipo haja wasubiri.

Anasema hata yeye alikuwa miongoni mwa waliopata wachumba akiwa chuoni, ingawa hakuishi na mke wake kama wanandoa. Alilazimika kusubiri hadi alipomaliza chuo ndipo akaoa.

"Kwa wanaotoka kidato cha sita, cha nne au vyuo wakaja kusoma chuo kikuu, ushauri wangu wangesubiri kuliko kuharakia maisha. Lakini kundi la pili ambao wameanza kufanya kazi, sioni dhambi wakiishi kama mume na mke ilimradi wawe wamefuata sheria na utaratibu wa Mwafrika," anasisitiza Golden.

Anataja hatari zinazowakumba vijana wanapokurupuka kuoa au kuolewa mapema, ikiwamo kukosa muda wa kufanya vizuri upande wa taaluma.

Hatari nyingine anasema ni kuwapo kwa matukio ya vipigo au hata vifo vya wenza, pale kunapotokea matukio ya kusalitiana.

’Wasikimbilie mapenzi wakati wa masomo, wanaongeza vitu vingi vichwani, hivyo kupoteza uwezo wa ufikiri kwenye masomo,’’ anasema.

Kwa upande wake, aliyekuwa Rais wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Mzumbe George Lubeleje, anasema ndoa vyuoni ni nyingi, lakini zimekuwa tatizo kwa baadhi kushindwa kutimiza malengo.

Anasema wakati wa uongozi wake alishakutana na matatizo ya mizozo ya wanafunzi, huku wengi wakishindwa kuvumiliana na kujikuta wakiingia kwenye mizozo na malalamiko kwa serikali za wanafunzi.
 

Mtazamo wa viongozi wa dini

Sheikh wa Mkoa wa Dodoma Mustafa Rajabu Shabani anaitaja ndoa njema ni ile inayohusisha wazazi na kwamba lazima ifanyike kwa uwazi mbele ya jamii.

“Ndoa ni sehemu ya ibada, haihitaji watu kukurupuka, hata kwa viongozi wa dini hawatakiwi kuruhusu mambo hayo yafanyike kwa kukurupuka, kwani wanaweza kusababisha majuto kwa siku za usoni,”alisema Mustafa.

Kwa upande wake, Kasisi wa Kanisa la Anglikana Pareshi ya Chamwino Ikulu, Mchungaji Bezaleli Chibago, anasema ndoa sahihi ni ya vijana waliokubaliana kihalali na kujitambulisha kwa wazazi, kisha wakafuata taratibu bila kujali kama wanasoma au walishamaliza.
Mchungaji Chibago anasema hakuna hatari kwa vijana kuanza maisha yao vyuoni, ila anatahadharisha kuwa ndoa hiyo isiwe ya kificho.

“Wakioana kwa kufuata utaratibu haina shida yoyote, waliopendana wanatakiwa kufuata taratibu kama zilivyo ikiwemo kushirikisha pande mbili za wazazi au ndugu na wafunge ndoa bila kuwekewa vikwazo,” anasema Mchungaji Chibago.

Kuhusu kukwepa gharama na sherehe ukumbini, alisema viongozi wa dini wanaweza kushawishi kwa upande wa mzazi wa kike ili wakubaliane na kumruhusu muoaji afunge ndoa, kwani mahali haipaswi kuwa kikwazo ingawa ni utaratibu na utamaduni wa Kiafrika.