Suala la njaa,Ukame nchini lisiwatenganishe viongozi wetu nchi hujengwa kwa umoja

Mkazi wa Nyamazobe jijini Mwanza, Kelvin Robert akiangalia shamba lake la mahindi Desemba mwaka jana, yaliyonyauka baada ya kukosa mvua. Picha ya Maktaba
Muktasari:
Au ni kwa vile msimamo wa Rais wetu haukuonyesha upendeleo wa wazi wazi kwa viongozi wa dini? Inawezekana viongozi wetu wa dini wametambua ukweli kwamba ujenzi wa Taifa letu ni mradi wa pamoja?
Je, huu ndiyo mwisho wa ukimya wa wanateolojia wetu? Tumekuwa tukihoji ukimya wa “Wanateolojia wetu” au tabia yao ya kuibuliwa na matukio na hasa matukio yasiyopendelea msimamo wao.
Tunaweza kuhoji ni mtu gani anataka kumchonganisha Rais John Magufuli na viongozi wetu wa dini? Au ni kweli kwamba sasa wakati umefika wa viongozi wetu wa dini kupingana wazi wazi na kiongozi wa nchi? Viongozi hao wameweka woga pembeni?
Au ni kwa vile msimamo wa Rais wetu haukuonyesha upendeleo wa wazi wazi kwa viongozi wa dini? Inawezekana viongozi wetu wa dini wametambua ukweli kwamba ujenzi wa Taifa letu ni mradi wa pamoja?
Je, huu ndiyo mwisho wa ukimya wa wanateolojia wetu? Tumekuwa tukihoji ukimya wa “Wanateolojia wetu” au tabia yao ya kuibuliwa na matukio na hasa matukio yasiyopendelea msimamo wao.
Utamaduni ni kwamba Serikali ikiwapendelea viongozi wa dini, hata kama Serikali hiyo inakwenda kinyume na kutenda matendo kinyume na haki za binadamu, viongozi wetu wa dini wanakaa kimya.
Sasa, viongozi wetu wa dini wamejitokeza kusema kuna njaa wakati kiongozi wa nchi akisema hakuna njaa na kuweka wazi kwamba mwenye mamlaka ya kutanganza njaa ni yeye. Viongozi wa dini wameitisha sala nchi zima kuombea mvua.
Je, ni kwa nia njema ya kushiriki mradi wa pamoja wa kulijenga Taifa letu au kuna kitu nyuma ya pazia? Rais, bila kificho anasema hizi ni njama za wanasiasa na waandishi wa habari.
Viongozi wa dini wameamua kujilipua au wanasimamia msimamo wao wa kufa wakitetea ukweli? Ni msimamo wa kudumu au ni kutegemea matukio?
Kabla sijasonga mbele, nifafanue maana ya neno “teololojia”. Kwa lugha ya kawaida na nyepesi, Teolojia ni elimu ya dini na mambo yote yahusuyo imani na Mungu.
Mwanateolojia ni mtaalamu aliyesomea teolojia na kuibuka na uwezo wa kuchambua kwa ufasaha nadharia ya madhehebu ya dini na kuielezea ili iendane na kueleweka katika sehemu fulani na kwa wakati uliopo.
Wanateolojia wanaandika vitabu vya kuiongoza jamii katika mambo ya imani ndani ya maisha ya siku kwa kuzisoma alama za nyakati.
Wanafundisha shuleni na vyuoni ili kujenga imani pevu miongoni mwa vijana. Wanateolojia wengine ni waanzilishi wa shule za mawazo “School of thoughts”. Katika nchi zilizoendelea wanateolojia ni watu mashuhuri na wanaheshimika maana dini umekuwa msingi mkubwa wa maendeleo katika nchi hizo.
Pia, ikumbukwe kwamba wanateolojia ndiyo kundi linalounda jumuiya ya viongozi wa kidini. Hawa ndiyo mapadri, masheikh, maaskofu, makardinali na mapapa.
Kwa sababu ya historia na unyonge, wanateolojia wa Tanzania hawasikiki, wamejawa woga na wala siyo mashuhuri. Tunao mapadri, wachungaji, masheikh, maaskofu na kardinali.
Tunao wanaofundisha shuleni na vyuoni na wengine wanaandika vitabu, lakini ukiwabana kwa hoja nzito wako tayari kuyakana hata maandishi yao wenyewe.
Kama anavyosema Frieder Ludwig kwenye kitabu chake cha “Church and State in Tanzania: Aspects of Changing Relations, 1961-1994. London, 2001”, Kanisa barani Afrika linatuhumiwa kwa kutotumia madaraka ya kusema. Hii ni kasoro ya matumizi ya madaraka.
Anadhani sababu kadhaa zinazuia kanisa kusema kama viongozi wa kanisa wanaishi mbali na watu wanaopaswa kuwasemea, dhambi za kanisa zisizotubiwa zinalizuia kusema ustaarabu na uungwana wa kutunza urafiki na kanisa kutoguswa na yale linayopaswa kuyasemea.
Muundo wa kanisa
Kanisa limepoteza mawasilinao na wasomi ambao waliliacha na hao hao ndiyo wanaofanya uamuzi mkubwa wa sera na mifumo katika nyanja za siasa, uchumi na jamii kwa kuwa si wanafunzi tena, bali ni wanachama wa kanisa.
Wanaibadili jamii bila nguvu ya ushawishi wowote katika kanisa hata kama kuna wanaodhani wanakanisa walio serikalini wanafanya hivyo kwa maagizo ya kanisa.
Kanisa limepoteza mawasiliano ya kweli na maskini wa vijijini ambao ndiyo wengi. Linawahudumia kimwili kwa kuwapa huduma, lakini kiroho wanahudumiwa na vikundi vipya vinavyoibuka na ambavyo ujuzi wake katika kuijenga jamii endelevu haujapimwa.
Kwa kutambua hali hii, taasisi za dini zinahitaji kuwa na mkakati wa kudai na hatimaye kurejea katika mshikamano wake na maskini wa vijijini na kuunda daraja la maongezi na wasomi walio mijini.
Hatua hii yaweza kupeleka mabadilliko makubwa katika muundo na mazoea ya kanisa. Hii inahitaji moyo jasiri, kwa sababu ni ama kanisa libadilike au libakie ni nafasi ya waoga wasiopenda kuukubali ukweli unaowahusu.
Kisiasa na kijamii kanisa naamini lina ruhusa ya kuunda maoni yake lenyewe na kuwa tayari kuyatetea. Tatizo ni kupinga bila kupendekeza jipya au kupinga kwa msimu kama ilivyo sasa hivi tunapoelekea kwenye tishio la ukame nchini.
Hakuna anayependekeza la kufanya zaidi ya kupingana na Rais Magufuli kwamba kuna njaa. Je, mabishano haya yanachangia nini katika mradi huu pamoja wa kuleta maendeleo katika Taifa letu la Tanzania? Ni hatari kuwa na kanisa au taasisi ya kidini isiyo na mshikamano na maskini au wasomi.
Imani ya jamii na amani na kuleta maendeleo ni mradi wa pamoja tena wa muda mrefu. Tanzania tuna kipindi cha miaka zaidi ya 50, katika mradi huu wa pamoja.
Pamoja na kutenganisha dini na Serikali, historia imeonyesha kwa wema na ubaya, kuwa mashirika ya dini ni washirika wa pamoja na Serikali katika kujenga imani ya jamii, amani na kuleta maendeleo.
Mathalan makanisa tangu hata kabla ya uhuru yamejihusisha na utoaji wa huduma za jamii; mashule, ustawi wa jamii, afya ya msingi na afya ya jamii.
Maendeleo, kilimo, maji, miundo mbinu, ufundi, jinsia na nyinginezo, utetezi kupitia elimu ya haki za msingi, maafa, kampeni dhidi ya deni la nchi, sera bora na mazingira na uraia.
Kutokana na mnyumbuliko wa historia hiyo safari ya miaka 50 ya Uhuru imetuonyesha wazi kuwa mshikamano wa kujenga imani hii siyo kitu cha kudumu.
Hutokea katika safari, baadhi ya wajenzi wakageuka wabomoaji wa imani ya jamii, wengine kuwa watazamaji na hata wengine kuwa waathirika wa makundi haya mawaili.
Likitokea hilo, ujenzi wa imani ya jamii huchukua sura ya mgogoro wa kijamii na hatimaye kuua kabisa imani ya jamii na amani katika jamii.
ili kujenga imani ya jamii na amani, ni lazima kiongozi awe kiongozi wa dini ama Serikali, awe na maadili ya madaraka na matumizi yake, madaraka yasiyokuwa na maadili ni chanzo cha kukosekana kwa imani na amani.
Pia, kiongozi awe mtu wa kujitoa au kujitolea, viongozi wengi katika jamii hapa Tanzania bila kujali taasisi gani wanatoka, hivi sasa wanafanana kwa jambo moja kubwa: kwamba, wanaamini kuwa nguvu yao ya ushawishi katika jamii inatokana na wingi wa mali walizonazo, visomo walivyopata na pengine wanatoka vyama gani.
Wapo wengine lakini wachache wanaodhani dini zao, makabila yao na jinsia zao vina nafasi katika kuwafanya waaminike katika jamii
Tamaa na uchu wa mali
Tamaa na uchu wa mali kwa viongozi wa jamii imeharibu kizazi cha viongozi wazuri hasa vijana na kuzalisha kasumba kuwa si rahisi kuwa kiongozi bila kuwa na mali.
Vipawa vingi vizuri vya viongozi vijana vimeharibiwa na dhana hii na uwezekano wa kuharibika zaidi ni mkubwa kuliko kinyume chake.
Uwezekano wa kubaki kiongozi mwadilifu ukiwa na mali nyingi ni dhana isiyotekelezeka kwa sababu mali nyingi huondoa unyenyekevu na kubadilisha hali ya kiongozi katika kufikiri, kuamua, kutenda, kuvumilia, kukosoa au kukosolewa.
Ili kuleta maendeleo ni lazima kupigana na umaskini, uzoefu wa taasisi za dini na viongozi wake uainishe sura kuu nne za umaskini katika Tanzania, yaani umaskini wa madaraka, umaskini wa kukosa mshikamano,umaskini wa jinsia na umaskini wa eneo aliko mtu.
Imani ya jamii kwa taasisi za dini ni budi ijengwe kwa kuangalia ni jinsi gani vyombo hivyo na viongozi wake wanafanya kuondoa sura za umaskini, badala ya kukazana kuondoa uhaba wa vitu na kufanya mambo ya kisasa na kudhani hayo ndiyo maendeleo.
Ni vyema maendeleo ya Taifa changa kama la Tanzania yajikite kwenye vitu vinne yaani, utambulisho, uhuru, ushirikishwaji na kujitegemea.
Kwa kuwa dhana nyingi maarufu za maendeleo (hasa za ki-magharibi) zimejengwa katika harakati za kuondoa uhaba na kuhodhi mali ni bora taasisi za dini zikajenga katika uwanja wa kuichambua nadharia ya maendeleo ili kuionya na kuitahadhalisha jamii dhidi ya athari za maendeleo yasiyotokana na upevu wa fikra za watu wenyewe.
Taasisi za dini zikizama katika harakati za maendeleo zinazofanywa kwa kuegemea dhana za kigeni, jamii ikiharibikiwa itazilaani taasisi hizo kwa sababu ni wajibu wa taasisi kubainisha kasoro zilizomo katika dhana ngeni za maendeleo.
Mifano iko mingi inayoonyesha kuwa imani ya jamii kwa taasisi za dini hailetwi na mali za taasisi hizo (vituo, miradi na program), bali inajengwa na misimamo ya taasisi hizo na viongozi wake katika kutetea haki iliyo katika umbo lolote inayomhusu mwanadamu na mazingira yake.
Inaleta heshima kama taasisi ya dini na kiongozi wake wanafahamika wanasimama wapi katika masuala ya msingi katika jamii ili imani ya jamii iweze kujengwa na misimamo ya namna hiyo si lazima iwe ni ile inayopendwa na watu wengi.
Sauti ya leo ya viongozi wetu wa dini ya kutangaza njaa, ikiwa ni kinyume na tangazo la Rais Magufuli isiwe ni sauti ya muda tu au kusukumwa na mawazo hasi, bali uwe msimamo wa viongozi wetu wa dini wa kushiriki mradi wa pamoja wa kulijenga na kuleta maendeleo katika Taifa letu la Tanzania.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana kwa baruapepe: [email protected] au [email protected] na simu namba +255 754 633122