Sura ya kisomi ya uchaguzi Marekani

Wamarekani wakiwa katika mkutano wa kampeni.
Muktasari:
“Ninavyojua mimi kazi ya Rais ni kuweka mazingira mazuri ya kazi na ajira kwa wananchi wao na kwa kweli Obama amefanikiwa. Hilo lilidhihirishwa na Romney mwenyewe alipokuwa akilinganisha takwimu za ajira tangu Obama alipochukua madaraka. Alikuta uchumi ukiwa mbaya lakini amejitahidi kuuinua, kwa mwaka 2010 alijiwekea lengo la kukuza ajira ambapo aliweza kukuza hadi ajira 500 kwa mwezi, alitoa mifano kwenye kampeni zake…”
TUMESHUHUDIA uchaguzi wa Marekani hivi karibuni ambapo Rais Barrack Obama ameibuka na ushindi wa asilimia 50 huku mpinzani wake Mitt Romney akimkaribia kwa kupata asilimia 48.9. Kutokana na umaarufu wa taifa hilo kubwa duniani, uchaguzi huo umekuwa mjadala mkubwa ulimwenguni.
Moja ya mijadala ya uchaguzi huo ulirushwa wiki iliyopita katika kipindi cha ‘This week in perspective’ na kituo cha televisheni cha TBC1, ukiwashirikisha wabingwa wa masuala ya siasa ndani ya nje ya nchi.
Walioshiriki katika kipindi hicho kinachoongozwa Adam Simbeye, ni Mhadhiri wa Sayasi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Daudi Mukangara, Mtaalamu wa Mawasiliano na sera za umma kutoka Marekani, Profesa Nicolas Boas na Mhadhiri mstaafu wa falsafa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Azaveli Lwaitama.
Mbali na hao walioonyesha maeneo kadhaa ambayo Tanzania inaweza kujifunza, wasomi mengine waliohojiwa kwa nyakati tofauti wameweka bayaka kwamba hakuna la kujinza Marekani.
Profesa Mukangara anasema licha ya Obama kukabiliwa na changamoto nyingi, alifanikiwa kuinua uchumi wa Marekani na kumfanya akubalike zaidi.
“Obama alikuwa akikabiliwa na changamoto nyingi na mojawapo ilikuwa ni kuyumba kwa uchumi. Bush aliacha hali ya uchumi ikiwa mbaya na ndiyo hali ilimsababisha mpinzani wa Obama kwa mara ya kwanza, John MacCain kushindwa. Kwa hiyo Obama aliingia madarakani akijua kabisa anakwenda kupambana na suala la uchumi,” anasema Profesa Mukangara na kuongeza:
“Ninavyojua mimi kazi ya Rais ni kuweka mazingira mazuri ya kazi na ajira kwa wananchi wao na kwa kweli Obama amefanikiwa. Hilo lilidhihirishwa na Romney mwenyewe alipokuwa akilinganisha takwimu za ajira tangu Obama alipochukua madaraka. Alikuta uchumi ukiwa mbaya lakini amejitahidi kuuinua, kwa mwaka 2010 alijiwekea lengo la kukuza ajira ambapo aliweza kukuza hadi ajira 500 kwa mwezi, alitoa mifano kwenye kampeni zake…”
Naye Profesa Boas anasema kuwa suala la ajira lilikuwa ndiyo siri pekee iliyomfanya Obama ashinde, kwani tangu alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza moja kati ya mambo muhimu aliyoahidi ni kuongeza ajira na alifanikiwa.
Kwa upande wake Dk Lwaitama anagusia suala la vyombo vya habari akisema kuwa vimekuwa vikikuza mambo kiasi cha kumpandishia umaarufu.
“Unaweza kusema kuwa vyombo vya habari vinapotosha, lakini ukweli ni kwamba ndiyo vilivyompandisha chati. Inawezekana ndiyo sababu ya kushindwa kwa Romney, vyombo vya habari viliwashawishi hata wale wasiomtaka Obama wampende, inawezekana pia ametekeleza ahadi lakini vyombo vya habari pia vimechangia.
Akizungumzia zaidi utendaji wa Obama, Profesa Mukangara anasema ana idadi ya ahadi 225 na amezitekeleza…
“Sitaweza kuzitaja zote kwa sasa ila ninachotaka kusema hapa ni kwamba Wamarekani wamemchagua Obama kutokana na rekodi yake.
Kwa upande mwingine Profesa Mukangara anagusia kampeni ambapo anamkosoa Romney aliyesema atapunguza kodi, lakini wakati huo huo anasema ataondoa misamaha ya kodi.
“Unajua misamaha ya Marekani ni tofauti na hii ya hapa kwetu. Kwa mfano kuna watu wanaopewa misamaha ya kodi kwa kuhudumia makundi ya jamii kama yatima, wajane. Kwa hiyo ukiwakatia misamaha hao umewaumiza hata masikini. Lakini alichosema Obama ni kwamba watu wa hali ya chini walipe kiasi kidogo kuliko matajiri,”
“Hata kwenye masuala la uhamiaji, Romney alikuwa na mikakati migumu wakati huu Marekani inabadilika lakini bado anakuja na masharti magumu.”
Afrika itegemee nini?
Akijadili manufaa ya uchaguzi huo kwa Afrika na Tanzania kama nchi, Profesa Boas anasema kwa kuwa Obama amekuwa akitetea amani duniani hata Tanzania inaweza kufaidika na pia kwenye uchumi katika mipango ya Marekani kuzisaidia nchi masikini.
“Jingine ni suala la Uafrika, tunaweza kusema kuwa kwa muda mrefu Waafrika hawajawahi kuingia White house, lakini Obama ameweza. Hata kwenye matumizi ya fedha za misaada kwa nchi masikini. Wamarekani ni watu wanaofuatilia sana, fedha zinazotolewa kama msaada ziwafikie walengwa. Kwa hiyo Obama atajitahidi kufuatilia maendeleo ya nchi masikini kama Tanzania,” anasema.
Akizungumzia hoja hiyo, Profesa Mukangara anamtaja Obama katika sura mbili;
“Kwanza Obama kama mtu mweusi na Obama kama Mwamerika. Ni mtu anayejua na kufuatilia watu wa mataifa mbalimbali. Tunajua kwamba wakati wa utoto wake aliwahi kuishi Indonesia na pia aliwahi kutembelea Kenya kwa hiyo anauelewa wa watu wa mataifa mengine,” anasema.
Hata hivyo anasema kuwa Obama hatafanya kazi kwa ajili ya Waafrika, bali kwa Wamarekani waliomchagua ingawaje kihistoria Tanzania na Marekani zimekuwa marafiki.
Kwa upande mwingine wakiujadili uchaguzi huo, wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wana maoni tofauti.
Mhadhiri wa Sayansi ya siasa wa chuo hicho, Dk Benson Bana anasema Tanzania inayo mambo ya kujifunza kutoka katika uchaguzi huo tangu kwenye kampeni hadi kwenye ushindi.
“Watanzania tunaweza kujifunza katika kampeni zao za kistaarabu na masuala muhimu yalijadiliwa kama vile ajira, afya na uchumi. Sisi hapa kwetu hatuna jipya katika kampeni zetu. Kingine ni kukubali matokeo pale unaposhindwa, umpongeze aliyeshinda, huo utamaduni haupo kwetu. Kingine ni michango ya wanachama kwa ajili ya uchaguzi iliyofikia dola 2.58 bilioni, hapa kwetu hatujui kuchangia vyama vyetu na wala hatusikii harufu ya ufisadi,” anasema Dk Banna.
Hata hivyo anasema Watanzania hatupaswi kubweteka na Obama ila tujipange upya kwa ajili ya maendeleo yetu wenyewe.
Kwa upande wake, Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala anasema jambo muhimu la kujivunia katika uchaguzi huo ni kule kuona kwamba Mwafrika wa kwanza ameingia Ikulu ya Marekani.
“Hii ni alama tu kwamba mtu mweusi ameingia Ikulu ya Marekani. Huko nyuma Waafrika tumeteswa, tumepelekwa mateka utumwani, tumedharauliwa, kwa hiyo ni jambo la heshima kwa Mwafika kuwa ikulu hakutakuwa na woga tena,” anasema Profesa Mukandala.
Hata hivyo anasema hakuna la kujifunza katika uchaguzi wao hasa kwa kuwa hauonyeshi kuwa na demokrasia ya kweli.
“Hatuna la kujifunza kwa suala la demokrasia, kwa mfano Rais wao hachaguliwi kwa mtu mmoja na kura moja. Ile ‘electoral college’ ina uwiano tu wa kura, ni tofauti na sisi ambao kila kura ya mtu ina thamani kwa hiyo demokrasia yetu ni nzuri zaidi,” anasema.
Kuhusu manufaa ya Obama kwa Tanzania Profesa Mukandala anasema hatupaswi kumwangalia kama suluhisho la matatizo yetu badala yake tutafakari na tuchekeche mambo yetu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kigoda cha cha taaluma cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji anasema uchaguzi wa Marekani hauna funzo kwa Tanzania wala hakuna cha kujifunza kutoka kwa Obama mwenyewe.
“Uchaguzi huo hautufundishi lolote, kwanza hauna ile demokrasia tunayoihubiri. Uchaguzi ulijaa ufisadi… huwezi kuona lakini jiulize yale mabilioni ya hela yalichangwa na nani kama siyo makampuni makubwa kwa manufaa yao? Yale yale tunayokataza hapa.
“Tusitegemee lolote kutoka kwa Obama, labda kama tunataka kuongezwa vyandarua,” anasema Profesa Shivji.