Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uboreshaji wa mfumo wa serikali za mitaa

Muktasari:

Katika ngazi ya kata watendaji wasiwe wajumbe wa kamati za maendeleo za kata bali kamati hizo ziundwe na wajumbe wa kuchaguliwa tu ambao ni wenyeviti wa serikali za vijiji na madiwani wanaowakilisha kata katika halmashauri. Watendaji wahudhurie vikao hivyo kwa kualikwa. Katika ngazi ya mtaa iundwe kamati ya kumshauri mwenyekiti wa mtaa.

Wiki iliyopita katika kona hii tulikuwa na mwendelezo wa historia ya serikali za mitaa nchini. Leo tunaendelea na mfululizo wa historia hii. Katika makala hii tutaelezea Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa, ulioanza rasmi mwaka 2000.

Kwa kutambua athari na matatizo ya mfumo uliokuwapo wa serikali za mitaa, Chama cha Mapinduzi katika ilani zake za uchaguzi za mwaka 1995, 2000 na 2005 kimeeleza wazi azma yake ya kuziimarisha serikali za mitaa ili ziweze kuwa vyombo madhubuti vya kutoa huduma bora kwa wananchi na kukuza demokrasia na uwajibikaji kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya wananchi kwenye maeneo yao.

Pia, Serikali kwa kushirikiana na wadau wakuu walikubaliana kuhusu taswira ya uboreshaji wa mfumo wa serikali za mitaa ambayo iliidhinishwa kama Agenda ya Kuboresha Mfumo wa Serikali za Mitaa ya mwaka 1996-2000. Taswira ya Serikali kuhusu mfumo mpya wa serikali za mitaa ni kuwa na serikali za mitaa zenye uhuru wa kujiamulia na kutekeleza mambo yao kwa kiasi kikubwa ilimradi zinafuata sera ya nchi na hazivunji sheria.

Vilevile serikali za mitaa zitakazowashirisha wananchi katika kupanga, kuamua na kutekeleza mipango na shughuli mbalimbali za maendeleo na kukuza ushirikiano na vikundi vya wananchi katika maeneo yao pamoja na kuwa imara, zenye uwezo wa kutekeleza maamuzi yao. Utekelezaji huo utawezekana kutokana na kuwa na rasilimali na madaraka yanayohitajika kutekeleza majukumu na kazi zao pamoja na watumishi wa kutosha wenye sifa, uwezo, stadi na ari ya kufanya kazi na ambao wataajiriwa na kuendelezwa kutokana na kustahili kwao.

Zitaendeleza shughuli zao kwa uwazi na uwajibikaji kwa wananchi na zitazingatia kikamilifu misingi ya utawala bora. Kiwango cha uwazi na uwajibikaji ndivyo vitakavyoelezea kiwango cha uhuru wa kujiamulia mambo yao na bila kuingiliwa na Serikali Kuu; Zitakuwa na majukumu na kazi zinazoendana na mahitaji halisi ya wakati wa maeneo yao, hali ya kiuchumi na ya kijamii ya maeneo yaliyo chini ya mamlaka yao ziwe na miundo inayozingatia aina ya majukumu, kazi na mazingira ya kila Halmashauri.

Katika mfumo huo wa serikali za mitaa, viongozi (madiwani) na watumishi wa Serikali za Mitaa watatakiwa kuwa na uadilifu usiowekewa mashaka.

 

Uboreshaji wa mfumo

Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa uliandaliwa na kuidhinishwa na Serikali mwaka 1998 ili kuimarisha mfumo wa serikali za mitaa ambao ungeziwezesha kutekeleza masharti ya utawala bora unaozingatia uwajibikaji, uwazi, demokrasia na ushirikishwaji wa umma.

Vilevile, Serikali iliidhinisha mkakati wa upelekaji madaraka, majukumu na rasilimali kwa wananchi kupitia serikali za mitaa ambao ndio unaotumika katika kutekeleza maboresho yanayohitajika katika mfumo uliopo wa serikali za mitaa.

Sheria zilizopo zinazohusu serikali za mitaa zifanyiwe mapitio na hatimaye kufanyiwa marekebisho ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuzingatia halmashauri kupewa uwezo wa kuajiri na kusimamia watumishi wake, kusimamia mapato na matumizi yake na kuwajibika moja kwa moja kwa wananchi na kutoa ruzuku kwa halmashauri. Zingine ni kuweka utaratibu mzuri wa mgawanyo wa mapato na vyanzo vya mapato kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, kubainisha uhusiano mpya kati ya mamlaka hizo mbili sambamba na kuweka utaratibu mzuri wa uhakika ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuharakisha maendeleo kwa kutumia demokrasia unafanikiwa.

Jambo jingine ni kusogeza madaraka karibu zaidi na wananchi kwa kuziimarisha ngazi za chini za halmashauri ili ziweze kufanya uamuzi wa kimaendeleo ambayo yanagusa maisha ya kila siku ya wananchi.

Sheria mbalimbali za kisekta zifanyiwe marekebisho yanayopasa ili ziendane na uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa; ikiwa ni pamoja na kuzifanya Bodi na Kamati za Huduma kuundwa na kuwajibika kwenye halmashauri zinazohusika. Ofisi ya Waziri Mkuu iainishe na kuorodhesha sheria za kisekta zinazohusika.

Katika ngazi ya kata watendaji wasiwe wajumbe wa kamati za maendeleo za kata bali kamati hizo ziundwe na wajumbe wa kuchaguliwa tu ambao ni wenyeviti wa serikali za vijiji na madiwani wanaowakilisha kata katika halmashauri. Watendaji wahudhurie vikao hivyo kwa kualikwa. Katika ngazi ya mtaa iundwe kamati ya kumshauri mwenyekiti wa mtaa.

Iundwe kamati ya kuratibu na kuwianisha uboreshaji wa kisekta na wa serikali za mitaa chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu. Wajumbe wa kamati hiyo wawe ni pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara za Fedha, Utumishi, Mipango, Elimu, Afya, Kilimo, Ujenzi, Maji, Ardhi, Maendeleo ya Jamii na Wizara nyingine kama itakavyohitajika kwa nyakati mbalimbali. Uanzishwe mpango waalumu wa mafunzo yahusuyo serikali za mitaa; na mitalaa katika shule na vyuo ijumuishe masomo ya serikali za mitaa.

Itaendelea..