Sukari ya maisha ndiyo pingu ya maisha

Kwa mujibu wa sheria na taratibu za sehemu kubwa ya dunia ikiwamo Tanzania, ndoa ni muungano wa hiari baina ya mume na mke. Hiari yao huwapeleka mbele ya imani au sheria ili kurasimisha jambo lao.

Hakuna ndoa ya aina yoyote isipokuwa ya mwanaume na mwanamke. Mila, tamaduni na imani zinatofautiana juu ya aina za ndoa. Kuna zinazoruhusu mwanamume kuoa zaidi ya mwanamke mmoja, na zipo zinazotambua ndoa ya mume mmoja kwa mke mmoja.

Mifumo yote miwili ina sababu zake kutokana na aina ya maisha inayoyaishi, na mwanandoa ana hiari ya kuchagua mfumo anaoutaka kabla hajakula kiapo cha ndoa.

Kule Mashariki ya Kati kuna vita isiyo na mwisho. Wanaume wanauana vitani na kuacha wajane na watoto wasio na msaada na uhaba wa waoaji.

Hivyo wanaume walio ndani ya ndoa waliwaoa wajane na mabinti waliokuwa hatarini kutoolewa ili wapate thawabu.

Lakini huku Afrika wanaume walihitaji nguvu kazi ya ziada kwenye mashamba yao makubwa, walioa wanawake wengi ili kupata watoto wengi kama rasilimali watu kwenye uzalishaji mali. Kwa mfano machifu na watemi walihodhi ardhi kubwa wakarithishana kiukoo na kifamilia walifikia hata kurithishana wake na watoto ilimradi ardhi yao iendelee kumilikiwa nao.

Sehemu zingine utajiri wa mafuta, wazawa walimiliki ardhi na kuuza mafuta kwa Serikali na wageni. Waarabu walirithishana utajiri huo kindugu na kuonana wao kwa wao kwa kuogopa kuziacha mali zao kwa wageni. Maendeleo huja kutokana na changamoto.

Ndoa za aina hii zilikuwa na migogoro miongoni mwa matala kama wivu, ugomvi, ushindani na kadhalika. Hata palipokuwa na matatizo ya kiasili kinamama walitupiana macho na kunyosheana vidole.

Vyote hivyo vinasababishwa na mapenzi na matarajio ya akinamama kutoka kwa waume zao. Changamoto hizi zilisababisha mifarakano ya kifamilia na hata mauaji.

Walioyakwepa hayo waliingia kwenye ustaarabu wa ndoa za “Mume mmoja, mke mmoja.”

Hawa wanaungana na wale walioamini kuwa ndoa ziliumbwa mara tu baada ya mwanamke kuibuliwa kutoka kwenye ubavu wa mwanamume na haukuibua wanawake zaidi ya mmoja, wala mwanamke hakuibuliwa na mbavu za wanaume zaidi ya mmoja, basi kila mmoja ana wake hata kama bado hajazaliwa.

Hawa nao walikutana na changamoto za kutosha katika uwanja wao kuliko ambavyo walifikiria. Ukizingatia maisha ambayo kinamama nao wanachangia pato la ndani, mama anaweza kuchakarika kwa ujasiriamali mchana kutwa, na wakati huohuo akihitajika kuihudumia familia. Atachoka na kushindwa kutumikia idara hizi mbili kikamilifu.

Hakika katika hili mama anahitaji usaidizi. Kwa kuwa yeye na mumewe waliapa kuishi katika “mwili mmoja” hadi siku ya mwisho, suluhisho pekee lililopo ni kumuajiri mjakazi kwa ajili ya kusafisha nyumba, akuwaandaa watoto kwenda shuleni, atafua nguo za familia na kadhalika.

Ukaimu huo utaendelea hadi pale mama mteule atakaporejea. Mama mmoja alifanya kosa kujivisha taji lisilo lake.

Alijinyosha sofani kando ya mumewe akitazama TV, akisubiri huduma ya mjakazi kama vile mumewe alivyosubiri huduma yake. Kama vile haitoshi, aliponong’onezwa na baba kuhusu muda wa kulala, naye akaurusha mpira kwa dada: “Hebu kamtandikie baba yako, anataka kulala.”

Baba akagundua kuwa anahudumiwa na dada; na hapo ndipo aliporudisha kumbukumbu zake. Kimsingi ili mwanamume huyu afanye kazi yake kiutimamu, alihitaji msaidizi wa nyumbani.

Akamteua msichana mwenye vigezo katika nafasi hiyo na kufunga naye ndoa. Msichana huyu (ambaye sasa ni mwanamke) akaona kuwa naye anahitaji msaidizi wa baadhi ya majukumu yake.

Hili ni jambo timamu kabisa, lakini akakengeuka na kumkumbusha mumewe hadithi iliyomfanya atafute mke.

Macho ya mwanamume ni sawa na macho ya tai. Kwa kasi ya ajabu yanaona na kuakisi jinsi haja yake inavyoweza kukidhiwa na dada kwa weledi zaidi kulinganisha na mkewe aliyechoka.

Sasa ndoa inaingiwa na kigugumizi; dada anaanza kupewa fursa za maandalizi ya kurithi kiti cha mama; na mama kwa kulitambua hilo ndipo anapokumbuka shuka kungali kumekuchwa.

Kwanza kwa “hasira” ataruka mtaani kufanya lile linalofanywa na mumewe ndani.

Lakini baadaye atajiona mjinga, “kwani mbwa akikung’ata nawe umng’ate?” Atarudi kwenye suluhisho mbadala bila kuzingatia kuwa penye mzoga ndipo nzi hukutanika.

Bila kujua ataangukia kwa “waganga wa kurudisha mvuto”, wachungaji feki na “mashehe ubwabwa” kila mmoja akiwa na mistari yake ya kushiba.

Pamoja na wanandoa kuanzisha masakata kama haya, wao ndio wanaobaki kuwa wahanga wakuu.