Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TLS yafunua udhaifu vyuo vya elimu ya juu

Muktasari:

Kufeli kwa wanafunzi wanaosomea kuwa mawakili katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST), kumeibua mambo mengi makubwa, yakiwamo ambayo pengine baadhi ya watu wasingependa yawekwe hadharani.

Kufeli kwa wanafunzi wanaosomea kuwa mawakili katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST), kumeibua mambo mengi makubwa, yakiwamo ambayo pengine baadhi ya watu wasingependa yawekwe hadharani.

Tangu kutoka kwa taarifa za wanafunzi hao kufeli kwa wingi, mawazo mengi yametolewa, lawama nazo hazikukosa; kila upande ukitupa mzigo wa lawama kwa mwingine.

Hata hivyo, mjadala wa matokeo hayo ambao kwa siku kadhaa sasa umeteka hisia za wengi hasa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, umewaibua baadhi ya watu wanaoeleza hali halisi ya ujifunzaji vyuoni.

Uhalisia huo si kwa wanaosoma fani ya sheria pekee, bali kwa wanafunzi wengi kutoka fani mbalimbali katika taasisi za elimu ya juu.

Baadhi ya wadau wa elimu kwenye mitandao na katika vyombo vingine vya habari, pamoja na kukiri kuwapo kwa udhaifu kwenye mbinu za ufundishaji, menejimenti za vyuo, mitalaa na hata mifumo ya utahini, wanawanyooshea kidole wanafunzi kwa kuwa dhaifu wa kiweledi na kujituma, huku wengi wakishupalia ufaulu mkubwa tena kwa njia za mkato.

Tatizo ni mfumo wa elimu

Akizungumza na Kituo cha redio cha Magic FM cha jijini hapa. Mhadhiri wa sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Khoti Kamanga, alisema kilichotokea katika matokeo ya wanafunzi wanaosomea uwakili ni kiashiria cha udhaifu wa mfumo wa elimu kuanzia ngazi za chini unaochangia kuzalisha wanafunzi wasio na uwezo wanapofika ngazi za juu.

Akieleza mtazamo wake kuhusu matokeo hayo yaliyoshuhudia wanafunzi 26 wakifaulu kati ya 633, Profesa Kamanga alisema:

‘’Tunakwepa suala msingi amam kwa makusudi au la. Kukitokea tatizo fuatilia chimbuko. Narudia chimbuko kwa sababu bila kugundua hilo, utashughulikia tatizo juujuu. Chimbuko la ufaulu dhaifu katika shule ya sheria, ni mfumo mzima wa elimu.

‘’Ni mfumo unaowapeleka watoto wetu pale Law school, ni tatizo la mfumo unaowaandaa kuja vyuo na kisha Law school.Kuna wanafunzi wapo sekondari, lakini hawajui kusoma na kuandika… kati ya hawa wapo wanaopita katika mfumo na kujikuta wako chuo kikuu na kati yao, wapo wanaosoma sheria.

Sikanushi kama Law schoo hakuna tatizo lakini suala la msingi wanafunzi wanaokwenda pale kweli wanastahiki na wana sifa? Sheria waliyosoma kweli waliielewa? Wakiwa kidato cha sita, masomo ya historia, lugha na jiografia kama masomo mama ya hii fani waliyaelewa?... Ni ngumu kumeza lakini wengi wao hawana hizi sifa. Mimi nafundisha mwaka wa 31 chuo kikuu, unakuta mwanafunzi hata maelekezo ya mtihani anashindwa. Anaambiwa ajibu maswali manne anajibu matatu, tusiwalaumu Law school, tujue tatizo ni pana na liko kwenye mfumo mzima wa elimu.

Hoja ya mfumo wa elimu pia imegusiwa na mchangiaji aitwaye SaMM ambaye katika andiko lake katika kundi sogozi moja la Whatsapp aliandika yafuatayo:

‘’Environment (mazingira) nzima ya Elimu haichochei kujenga uwezo wa kufikiri,ime jikita kutafuta A tu...

No wonder ( haishangazi) siku hizi Straight A student wa account (mwanafunzi anayehitimu na alama A kwenye uhasibu) hawezi ku design, ku install na ku implement Accounting System ya New Entity bila ku copy & paste. Similarly to other professions (Vivyo hivyo kwa taaluma nyingine) iwe sheria, tiba, ufamasia, elimu na nyinginezo.’’

Kwa upande wake, Dk Mustapha Almasi wa Chuo Kikuu Mzumbe, anasema kilichopo ni kukosekana kwa nidhamu ya usomaji kwa wanafunzi.

‘’Ujifunzaji umekuwa wa kutegemea notes zaidi na pia kumekuwa na lawama nyingi kwa vijana kutaka kufaulu na kupata GPA kubwa. Hilo la nidhamu ya usomaji linaweza likawa limecangiwa na elimu tangu chini inayolenga kufaulu bila kujali maarifa,’’ anaeleza.

Vitabu vs vitini

Mejata Darweshi ni mhadhiri katika chuo kikuu kimoja kilichopo jijini Dodoma. Anasema alipojiunga na masomo ya shahada ya uzamili, alishangaa kuona wanafunzi wenzake, wakikacha kusoma vitabu na kukimbilia vitini vya walimu.

Akichangia mjadala katika mtandao wa Whasap, Mejata anaeleza:

‘’Tatizo watu tunakimbia kusema ukweli. Ukipanda mbegu mbovu utavuna mabua tu.

Mimi nakumbuka kabla sijaanza shule UDOM, mwaka mmoja kabla ya masomo nilichukua ‘course content’ ya kila somo nitakayosoma. Nikaangalia kila somo, nikapakua kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya intaneti vitabu angalau kumi kwa kila somo.

Nilipoanza kozi nikajikuta mimi ndiyo mzee. Lakini nilikuwa nashangaa kila tukimaliza darasa nawaacha wenzangu wamemzunguka mhadhiri. Siku moja na mimi nikawauliza wenzangu kwani huwa mnataka nini baada ya darasa kwa hawa wahadhiri? Kwa mara ya kwanza nikasikia neno vitini, wakiniambia huwa wanaomba vitini.

Sasa, nikawaambia kwa nini msisome vitabu? Kwa sababu hivyo vitini ni summary (mukhtasari) tu. Wakaniambia wewe mzee umekuja na ushamba wako hapa Bongo ni mwendo wa vitini tu!

Niliwaambia mimi nina vitabu latest (matoleo mapya) nitawapa. Haki ya Mungu walikataa kuvichukua. Lakini baadaye wakawa wanasema kichinichini huyu mzee wahadhiri wanampendelea kwa sababu ni mzee mwenzao, Daktari mmoja (jina namhifadhi) akawapa ukweli siku moja akawaambia nyie watoto tatizo hamsomi vitabu, hii level ya Masters siyo level ya kusoma vitini, ni level ya kusoma vitabu na machapisho.Watoto wetu sijuwi wamepatwa na nini.


Walimu, wanafunzi wote tatizo

Mdau mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Abu Fatma anasema ufaulu mdogo wa wanafunzi, unatokana na udhaifu wa pande zote yaani walimu na wanafunzi. Naye anatoa ushuhuda wake kwa kusema:

‘’Tatizo tunapambana kukosoa tulipoangukia na kusahau tulipojikwalia Mfumo wetu wa elimu kwa bahati mbaya kila wakati unavurugwa na kwa kufanya hivyo, kunasababisha wanafunzi kuwa waathirika. Nilishawah kupata kazi ya muda (part-time) katika vyuo vya elimu ya juu

Nikapewa fursa ya kufanya mihadhara katika ngazi ya kuanzia diploma mpaka shahada ya uzamili. Lakin pia nilikuwa nawaanda wahitimu wa shahada ya kwanza kwa ajili mitihani ya bodi fulani.

‘’Wakati huo nilijufunza baadhi ya mambo ambayo nasita kuilaumu TLS. Nikilijifunza haya:

Mosi, uwezo wa wahadhiri katika kuwaandaa wanafunzi kufanya mitihani ya bodi ni mdogo,

maana hata hao wahadhiri wengi wao walijaribu hiyo mitihan ikawashinda.

Pili, wahadhiri kuwajaza hofu wanafunzi wao wakiwa vyuoni kuhusu ufaulu wa mitihani ya bodi, hivyo wanafunzi wanajiandaa na mitihani wakiwa wamejiandaa kufeli kuliko kufaulu

Kuna wakati niliwahi kutoa swali nikawapa wanafunzi. Kuna mmoja akaenda katika chuo kikuu fulani kuomba msaada kwa mhadhiri ili amsaidie. Alichojibiwa yule mwanafunzi hilo swali ni la bodi, achana nalo.

Tatu, wanafunzi kutojiongeza katika usomaji. Wanafunzi wengi kwa sasa katika vyuo vya elimu ya juu, hawana muda kuingia maktaba kwa ajili ya kujisomea. Muda wao mwingi wanautumia kukariri vitini vinavyotolewa na wahadhiri wao. Kwa mazingira hayo, swali hata ukiwa umelifundisha ukibadilisha kidogo tu ujue wanafunzi zaidi ya asilimia 90 hawatoweza kulifanya.’’

Mwalimu Bakari Heri, alihitimu shahada ya kwanza katika fasihi na ualimu katika chuo kikuu kimoja kikongwe miaka ya mwanzoni mwa 2000.

Anasema kinachotokea sasa wanafunzi kutojituma kwa kukuza ufahamu kupitia usomaji vitabu na njia nyingine za udadisi wa mambo, kimekuwapo kwa muda mrefu vyuoni.

Anasema: ‘’Unadhani ni tatizo la vijana wa kileo tu? Nasi tumefanya hayo. Unajua ilikuwa ni kawaida unaanza chuo au unaingia mwaka fulani wa masomo, mwanafunzi unahangaika kutafuta madesa ya wanafunzi waliokutangulia, unayakusanya na kutoa copy ( nakala)

Sio kutafuta vitabu, hapana ni nakala za notes za watu waliopita, sijui mitihani ya zamani. Sasa kama unajua mhadhiri wako anarudia hata maswali kwenye mitihani, kwa nini usitafute huo mtihani na majibu ukawa nayo mkononi?

Anaongeza: ‘’Nenda vyuoni kote nchini, chunguza kwa nini kuna wafanyabiashara wengi wa kutoa copy? Wanafunzi hawana muda wa kuchimba mambo maktaba, unasubiri madesa hasa hasa vitini vya kozi nzima, unatoa nakala unajisomea. Kozi ileile, maswali yaleyale, kwa nini usumbuke na kujitesa... ndio elimu yetu hiyo... Tusilaumu watoto wa sasa, tuwape jukumu wenye mamlaka za kuangalia mustakabali wa elimu ya nchi hii.”

Wahasibu nao kama mawakili

Mafuriko ya wanafunzi kufeli masomo si kwa wanasheria pekee, hali hiyo imezoeleka hata katika fani nyingine ikiwamo ya uhasibu ambayo mitihani yake inasimamiwa na Bodi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu nchini (NBAA)

Idadi kubwa ya wanafunzi wanaofeli mitihani ya bodi hiyo, iliwahi kuibua mijadala mingi miaka ya nyuma.

Mfano wa karibu ni matokeo ya mwaka 2021. Katika taarifa ya matokeo hayo ambayo Mwananchi ilichapisha habari yake katika tovuti Desemba 29, yalionyesha watahiniwa 703 sawa na asilimia 18.2 ndio waliofaulu mitihani hiyo, huku watahiniwa 1818 sawa na asilimia 47 wakiangukia pua.

Watahiniwa hao walikuwa sehemu ya wanafunzi 3853 waliofanya mitihani ya bodi hiyo Novemba 2021, huku 1,332 wakitakiwa kurudia mitihani.

Akinukuliwa na Mwananchi, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, Pius Maneno, alisema katika taarifa yake kuwa watahiniwa 188 walifaulu mtihani wa CPA, idadi hiyo inafanya watahiniwa waliofaulu mitihani ya CPA mpaka mwaka huo kufikia 4,323 tangu kuanzishwa kwa mitihani hiyo mwaka 1975.

“Watahiniwa 1,208 kati ya watahiniwa 2,033 waliofanya mtihani wa taaluma ngazi ya Module E wamefeli mtihani huo huku watahiniwa 521 sawa na asilimia 25 watarudia masomo hayo”alisema.

Maneno alisema katika ngazi ya Mitihani ya Uandishi na Utunzaji wa Hesabu (ATEC 11) watahiniwa 56 sawa na asilimia 47 kati ya watahiniwa 117 waliofanya mtihani huo walifeli mtihani, huku watahiniwa 38 sawa na asilimia 32 wakitakiwa kurudia mtihani huo baada ya kufanya vibaya.

Nini kifanyike?

Mejata anasema ufaulu mdogo wa wanafunzi wa sheria na hata kwa makundi mengine ya kitaaluma, usichukuliwe kwa mtazamo wa kisiasa.

Mimi naona wamefeli kihalali. Na Watanzania tuwe serious (makini). Masuala ta kitaaluma tukishaingiza siasa tutakosea sana.Cheti cha ufaulu ni haramu kutolewa na mahakama au tume iliyoundwa kisiasa. Taaluma ni eneo huru, ambalo masuala yake huamriwa kitaaluma ili kulinda hadhi na ubora wa taaluma,’’ anasema.

Anaongeza: ‘’Hivi, siku wanafunzi wa udaktari, unesi, uhandisi na wengineo nao wakiingia mtaani kuwa wamefeli tutaunda tume yenye mrengo wa kisiasa? Mambo ya kutaka kufaulu kwa kusoma vitini hayajengi mtu kitaaluma. Watoto wetu wa sasa ni wavivu. ‘’

Imeandikwa na Abeid Poyo, Mwananchi
[email protected]