Je, utajiri wa gesi kusini ‘utaibeba’ Tanzania kiuchumi?

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo akimuelekeza jambo Rais Jakaya Kikwete wakati wa ufunguzi wa mradi wa gesi, Kinyerezi. Kulia ni Makamu wa Rais. Dk Mohamed Bilal.

Muktasari:

Lakini sasa Serikali inasema imejipanga  kuzalisha umeme vijijini kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2015.

Ni zaidi ya miaka 50 sasa tangu Tanzania imepata uhuru huku Watanzania wasiozidi asilimia 18.4 wanapata umeme na kati ya hao, asilimia 6.6 wanaishi vijijini ambako maeneo mengi hayana huduma ya nishati ya umeme.

Kutokana na hali hiyo wananchi wengi wanaoishi vijijini wanatumia taa ya chemli, vibatari au kulala gizani kwa sababu hawana nishati ya umeme baada ya serikali imeshindwa kufikisha huduma hiyo wakati mijini watu wanakosa nishati hiyo kwa kuwa umeme unauzwa ghali.

Lakini sasa Serikali inasema imejipanga  kuzalisha umeme vijijini kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2015.

Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, William Ngeleja aliieleza kwamba serikali itaongeza bajeti ili kuhakikisha kwamba nishati hiyo inapatikana vijijini kwa wakati muafaka.
Lakini tukigeukia upande wa pili, wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanaamini ikiwa taifa hilo lenye watu zaidi ya milioni 40 litakuwa na umeme wa uhakika, uchumi utakua kwa kasi zaidi kuliko sasa.
Wanabainisha kwamba uchumi utakuwa kwa zaidi ya asilimia 7 kwa mwaka kwa sababu shughuli nyingi za kiuchumi zitaongezeka kwa mfano,  kuanzishwa kwa viwanda vidogo vya kushindika chakula au matunda.

Tatizo la kuwapo kwa tatizo la umeme nchini linasababishwa na uhaba wa maji ambayo ni chanzo kikubwa cha kuzalisha umeme nchini. Sababu nyingine ni baadhi ya mitambo kuchakaa au wizi wa mafuta katika vyanzo vya kuzalisha au kusambaza nishati hiyo.

Bomba la gesi Mtwara hadi Dar
Wakati serikali ikijipanga kusambaza umeme vijijini,  baadhi ya wananchi wameonyesha wasiwasi ni vipi umeme utafungwa katika nyumba za nyasi au kuezekwa kwa nyasi vijijini.

Mkazi wa Kinyerezi, jijini Dar es Salaam, Salim Khalfan ni mmoja wa wananchi ambaye amefurahia kuwapo kwa mpango wa kuzalisha umeme wa kutumia gesi katika eneo la Kinyerezi, lakini  anahoji ni vipi umeme utaunganishwa kwenye nyumba za nyasi hasa maeneo ya vijijini.

Kutokana na hali hiyo anashauri wananchi hasa wanaoishi vijijini wapewe elimu nzuri na wawezeshwe kuinua pato lao ili wajenge nyumba bora zinazokidhi viwango vya kuwekewa umeme.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema kauli ya kupunguza umasikini  kwa wananchi bila kusambaza umeme sehemu zote nchini, itabaki kuwa ndoto.

Anasema kutokana na kuwapo tatizo la umeme, Serikali imejipanga kutumia umeme wa gesi kutoka Mtwara kwa lengo la kuhakikisha wananchi wengi zaidi wakiwamo wa vijijini wanapata umeme.

Kauti hiyo ilitolewa na Profesa Muhongo wakati Rais Jakaya Kikwete akiweka jiwe la msingi kuzindua mradi wa miundombinu ya gesi asilia katika eneo la Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
Ujenzi wa bomba kuu la kusafirishia gesi asilia la inchi 36 kutoka Mtwara kupitia Lindi, Pwani hadi Dar es Salaam lenye umbali wa kilometa 532, litaanza kujengwa ili kutoa huduma hiyo mijini na vijijini.

Akizindua mradi huo katika eneo la Kinyerezi jijini Dar es Salaam, Rais Kikwete ameeleza kufurahishwa na kazi kubwa iliyofanywa na Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika mradi wa ujenzi wa miundombinu hiyo ambao utazalisha megawati 3,000 kwa siku.
Rais Kikwete amesema ifikapo mwaka 2015 megawati 2,780 zitahitajika ili kukidhi mahitaji ya nishati hiyo na megawati 3,000 zitakazozalishwa kutokana na chanzo cha gesi zitatumika kutatua tatizo la mgao wa umeme na kuuza nchi nyingine za nje.

Rais anaeleza kwamba  gesi hiyo haitatumika kuzalisha umeme peke yake bali serikali ina dhamira ya kuzalisha mbolea hivyo Tanzania itakuwa moja ya mataifa ya Afrika yanayozalisha mbolea nyingi na kuinua sekta ya kilimo nchini.

Vilevile gesi itatumika viwandani, magari, na kupikia majumbani na sasa TPDC inatengeneza mtandao wa jiji zima la Dar es Salaam ili wananchi watumie gesi badala ya mkaa.

Mradi kugharimu Sh1.8 trilioni
Kikwete anaishukuru Serikali ya China kwa kukubali kutoa mkopo wa masharti nafuu wa Dola 1.225 bilioni za Marekani ili kutekeleza mradi huo. “Hakuna nchi yoyote ambayo ingeweza kutoa mkopo mkubwa kiasi hicho kwa masharti nafuu,” anasema Rais Kikwete.

Vile vile China imetoa kibali kwa mashirika yake kama China Petroleum Technology and development Corporation (CTPDC) na Benki ya Exim kutathmini ya mradi na kuikopesha fedha Serikali ya Tanzania.

Wakati rais akieleza hayo baadhi ya watu waliokuwa wakishuhudia uzinduzi wa mradi huo wamehoji kwanini mkopo utoke China, na mradi wapewe Wachina. Kwanini tathmini ya gharama za mradi zifanywe na mtoa mkopo, badala ya kampuni binafsi?

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Yona Kilaghane ujenzi huo unafanywa na Kampuni ya China Petroleum Technology Development Corporation (CPTDC), ikisaidiana na Kampuni za China Petroleum Pipeline Bureau (CPP) na China Petroleum Pipeline Engineering Corporation (CPEC).

Kilaghane anasema fedha za mradi huo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Exim, Benki ya China na pia utasimamiwa na Serikali ya nchi hiyo. Serikali ya Tanzania itachangia asilimia 10 ya mradi huo.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini Profesa Muhongo anasema Serikali imeweka kipaumbele katika kuzalisha  umeme kwa kutumia vyanzo vingine ambavyo ni gesi asilia, makaa ya mawe, maji, upepo, jotoardhi, tungamotaka, na jua ili kumaliza tatizo la mgao wa umeme nchini.

Gesi nyingi ipo baharini
Anaeleza kwamba  gesi iliyopo nchini ni takribani futi za ujazo trilioni 33 sawa na mapipa ya mafuta bilioni 6 na kwamba gesi nyingi ipo baharini kwenye maji ya kina kirefu.
Profesa Muhongo anasema kiasi cha gesi hiyo ni futi za ujazo trilioni 25 ambayo ipo baharini na kwamba ina uwezo wa kukidhi mahitaji ya nchi ya umeme wa MW 2,780 kati ya miaka 35 mpaka 89 iwapo Tanzania itatumia futi za ujazo milioni 400 kwa siku.

“Mradi unalenga kukusanya gesi asilia kutoka Mnazi Bay-Mtwara, SongoSongo, Kiliwani (Songo Songo), Mkuranga, Ntorya na pia kutoka kwenye bahari ya kina kirefu,” anasema Profesa Muhongo.

Profesa Muhongo anasema kwa sasa hatarajii kusikia kutangazwa umeme wa dharura wala mgao, huku akiwatahadharisha  wananchi  kujihadhari na watu wanaojiita wataalamu wa gesi, mafuta na madini ambao wamekuwa wakipotosha mchakato mzima wa kuchimba madini na gesi.

“Baadhi ya watu hao ni wale ambao wamepata mafunzo ya wiki mbili na kupewa vyeti vya mahudhurio ya semina, lakini kwa sasa ndio wanaojifanya ni wataalamu wa madini ya urani, gesi, mafuta na madini, anasema Profesa Muhongo.