Miaka 52 baada ya uhuru; Viwanda vikubwa ni asilimia 0.4

Viwanda vikubwa vyenye mitambo kama hivi ni asilimia 0.4 ya viwanda vyote vilivyoko nchini. Picha ya Maktaba.
Muktasari:
Licha ya Taifa kuwa na umri wa miaka zaidi ya 52 tangu ipate uhuru, idadi ya viwanda vikubwa ni asilimia 0.4 ya viwanda vyote viliyoko nchini
Ni mwaka wa 52 sasa tangu nchi ipate uhuru, lakini hali ya maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla inaonekana kutokua kwa kasi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ni wastani wa asilimia 18 ya kaya za Tanzania zinaishi katika nyumba zilizounganishwa na umeme. Maana yake ni kuwa kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaishi gizani kutokana na kukosa nishati hiyo.
Azma ya Tanzania kwa mujibu wa Mpango Elekezi wa Mwaka 2010 – 2025 ni kuhakikisha uchumi unabadilika na Tanzania kuwa ya kipato cha kati.
Aidha iko Dira ya Taifa ya mwaka 2025 ambayo inalenga kuelekeza nguvu za kuendeleza sekta ya viwanda, biashara na masoko.
Sekta ya viwanda kwa mwaka 2011/2012 ilikua kwa asilimia 7.8 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.9 mwaka wa fedha 2010/2011 na mchango wake katika Pato la Taifa uliongezeka kutoka asilimia 9.6 mwaka 2010/2011 na kufikia asilimia 9.7 mwaka 2011/2012.
Ongezeko dogo la mchango wa sekta ni matokeo ya mdororo wa uchumi duniani na mgao wa umeme. Hata hivyo, uzalishaji katika baadhi ya viwanda uliongezeka.
Kwa mfano, uzalishaji wa chuma uliongezeka kwa asilimia 19.7 kutoka tani 33,384 mwaka 2010 hadi tani 39,955 mwaka 2011. Ongezeko hilolilitokana na kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa hizo katika soko. Hata hivyo wachumi wanasema kiwango hiki ni kidogo mno, ukilinganisha na rasilimali ambazo Taifa inazo.
Maendeleo ya viwanda
Halmashauri zijipange kuunga mkono jitihada za Serikali kukuza sekta ya viwanda na kuinua uchumi wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda vya kati ifikapo mwaka 2015.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda anasema halmashauri zote za mikoa zinapaswa kutenga maeneo maalumu ya uendelezaji wa viwanda.
Takwimu za wizara hiyo zinaonyesha kuwa asilimia 88 ya viwanda vyote hapa nchini ni vichanga wakati asilimia 10.5 ni vidogo. Asilimia 0.2 ni vya kati huku asilimia 0.4 vikiwa ni viwanda vikubwa.
Ili kufikia lengo la kuinua uchumi wa nchi, ni muhimu wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wakawezeshwa ikiwamo kwa kutengewa maeneo maalumu kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao.
Kwa mujibu wa Dk Kigoda, Serikali imejiwekea mkakati maalumu ya viwanda mikoani, akisema kuwa utakuwa na tija kubwa kwa wananchi endapo upatikanaji wa nafasi kwa walengwa hautakuwa na urasimu au rushwa.
Eneo la ekari 107 lililotengwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) Dodoma na ekari 120 mkoani Singida kwa lengo la kuanzisha na kuendeleza Vijiji vya Viwanda, vitakuwa chachu ya maendeleo ya bidhaa za ngozi katika maeneo hayo.
Changamoto iliyopo kwa wajasiriamali ni kuhakikisha bidhaa wanazozalisha zinakuwa na ubora wa kimataifa na hili linawezekana kama elimu itatolewa ili kuwajengea uwezo.
Rais Jakaya Kikwete amewahi kuwaasa wamiliki wa viwanda kuwa “Wakati wote wekezeni kwa teknolojia iliyo juu ili kuwapa wananchi bidhaa zilizo bora. Msipofanya hivyo hata kama Serikali itawalinda wananchi watazisusa bidhaa zenu sokoni,” aliasa Rais na kusisitiza kuwa:
“Katika miaka kumi ijayo, Tanzania itakuwa ni nchi kubwa zaidi Afrika Mashariki. Hakuna uchumi utakaokua pasipo uwekezaji, ni vizuri mkatengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji wengi zaidi.”
Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) Dk Samweli Nyantahe anasema “Kuna taasisi nyingi zinazosimamia biashara hapa nchini na zote zinaendeshwa kutokana na michango ya wenye viwanda. Hili linafanya gharama za kufanya biashara kuwa kubwa, hivyo kuzuia wenye mitaji midogo kuingia sokoni”.
Viwanda na mikopo
Upatikanaji wa mikopo kwa wajasiriamali na wafanyabishara wadogo urahisishwe ili utekelezaji wa miradi hiyo uwe na uafanisi na tija inayotazamiwa.
Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema sekta ya viwanda, biashara na masoko haiwezi kupiga hatua bila ya hatua za makusudi za kuweka mazingira mazuri ya kuiendeleza, kwani licha ya Taifa kuwa na uhuru kwa zaidi ya miaka 52 sasa bado mazingira ya kufanya biashara siyo mazuri.
Mpango Elekezi wa mwaka 2010/2025 umetoa dira inayoonyesha Tanzania ielekee kwenye nchi ya kipato cha kati kupitia ujenzi wa uchumi. Kwa sababu hiyo Wizara tayari imeshaandaa Mkakati wa kuelekea kwenye lengo hilo.
Wanazuoni wanasema kuna uwezekano wa kufikia malengo yaliyowekwa ya kuufanya uchumi wa Tanzania kuwa wa viwanda vya kati licha ya kushindwa kufanya hivyo kwa muda wa zaidi ya miaka 50 ya uhuru.
Dk Ulingeta Mbamba kutoka Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS) anasema kuwa iwapo Serikali itapunguza maneno na kufanya utekelezaji wa miradi iliyopangwa ndani ya muda uliopangwa nchi itakuwa na maendeleo makubwa.
“Logistics (Usafirishaji) ikirahisishwa itakuwa chachu kwa wajasiriamali kuzalisha zaidi na hivyo kukuza sekta ya viwanda.
“Iwapo soko la ndani litapanuliwa, fursa zitaongezeka na wafanyabiashara hawataogopa ushindani unaoletwa na bidhaa kutoka China au nchi nyingine zilizoendelea,” anasema Mbamba na kuongeza kuwa mazingira magumu yanasababisha biashara kuwa rahisi kati ya Tanzania na nchi zilizoendelea kuliko baina ya mkoa na mkoa, ndani ya nchi na hata nchi jirani.
Wakati Taifa linapokuwa na umri mkubwa kama huu wa miaka zaidi ya 52 baada ya uhuru ni suala la msingi kufanya jitihada za dhati ili jamii inufaike na maana ya uhuru uliopo.