Vifaa vya ujenzi ni dhaifu

Baadhi ya Nondo zinazotumika katika shughuli za ujenzi Tanzania
Muktasari:
Aprili, mwaka huu, jengo lenye urefu wa ghorofa 16 lililokuwa Mtaa wa Indra Gandhi jijini Dar es Salaam liliporomoka na kuua watu 36 na wengine kujeruhiwa.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) hivi karibuni imevifungia viwanda vinne vya kutengeneza nondo vilivyopo jijini Dar es Salaam. Pia TBS ilizuia shehena ya tani zaidi ya 3,500 zenye thamani ya Sh5.6 bilioni kuingia sokoni.
Hatua hiyo ya TBS imezua maswali mengi kwa kuwa viwanda hivyo vimekuwa vikizalisha bidhaa hiyo kwa miaka kadhaa bila ufanisi wake kuhojiwa.
Wadadisi wa mambo wamebainisha kwamba uamuzi huo ni moja ya jitihada za Serikali katika kudhibiti maafa ya kuporomoka kwa majengo nchini Tanzania.
Wahandisi wachukue hatua
Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Waandisi Tanzania, Mhandisi Swalehe Kasswera amebainisha kwamba kama TBS itaendelea kufanya hivyo, mkakati huo unaweza kuwa suluhisho la kuzuia kuporomoka kwa majengo nchini.
“Kama wafanyabiashara hao wamesimamishwa, hivyo ni vyema TBS ikawa makini ili wasiingize bidhaa hizo sokoni, hiyo itasaidia kulinda fedha ambazo zingetumika kununua bidhaa ambazo siyo bora,” anasema.
Kwa uzoefu wake anasema katika masuala ya ujenzi amebaini kwamba nondo nyingi zinazotengenezwa nchini zinafaa kwa ujenzi wa nyumba za kawaida tu na siyo ghorofa kwa sababu ukizikunja zinavunjika.
“Katika suala hili, pia waandisi nao wana jukumu kubwa, kwani wanatakiwa wawe makini na vifaa vyote vinavyotumika kwenye ujenzi, wanapobaini kwamba havina ubora wasilazimishe kuvitumia bali wazuie na wachukue hatua zaidi.
“Tatizo linalojitokeza, wapo wafanyabiashara ambao wanajali zaidi kupata fedha na kuliko kutengeneza bidhaa bora,” anasema Mhandisi Kasswera.
Ofisa Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile anasema uamuzi huo umetekelezwa baada ya TBS kuchukua sampuli ya vipande kadhaa vya nondo na kwenda kuvipima kwenye maabara yao na kubaini kwamba hazina ubora unaotakiwa.
“Tutakuwa tukifanya ukaguzi kwa kushtukiza katika kampuni kubwa zinazouza vifaa vya ujenzi kwa baadhi ya viwanda vimetajwa kuwa ni vinara wa kuzalisha bidhaa ambazo hazina ubora,” anasema Andusamile.
Katika kampuni ya vifaa vya ujenzi ya FMJ iliyopo Buguruni Dar es Salaam, Mkurugenzi wa kampuni hiyo Fatina Said aliamriwa kusimamisha shughuli za kuuza nondo tani 379 ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kufuatilia viwanda ambavyo alivitaja kwamba alinunua bidhaa hiyo.
Maofisa hao wa TBS waliwasili pia kwenye kampuni ya Kamaka, Tabata wilayani Ilala jijini Dar es Salaam na kuamuru viongozi wa kampuni hiyo kusimamisha mauzo ya shehena ya tani 1,000. Akizungumzia hatua hiyo Meneja wa Biashara na Mauzo wa kampuni hiyo, Mubarak Dollah anakiri kuwapo kwa nondo zenye ubora tofauti ambazo zimekuwa zikizalishwa nchini na zinazotoka nje ya nchi.
Anabainisha kwamba nondo zinazotengenezwa nchini, zina ubora hafifu kiasi cha kushindwa kuhimili uzito mkubwa.
Vyuma chakavu
“Tatizo ni kwamba hizi nondo haziwezi kuwa bora kwa kiwango kinachotakiwa kwa kuwa malighafi inayotumika kuzitengeneza ni vyuma chakavu, kwa hiyo ni wazi kwamba haziwezi kuwa bora kama tunavyotarajia, lakini sisi tunauza sana hizo kutokana na utofauti wa bei, wengi wananunua hizo kwa kuwa tani moja inauzwa Sh1.3 milioni ikilinganishwa na tani moja ya nondo kutoka nje ambayo inauzwa Sh2 milioni,” anasema Dollah.
Mwanasheria wa TBS, Baptista Bitao anasema hatua ya kusimamisha uuzaji wa nondo hizo ni ya kwanza ikifuatiwa na kwamba wategenezaji wa nondo ambazo hazina ubora watasakwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Anabainisha kwamba watu hao wakibainika kuwa na hatia watachukuliwa watafungwa jela miaka miwili au kulipa faini ya Sh50 milioni.