Umuhimu wa ‘zoezi mfano’ la upigaji kura

Mgambo wakisikiliza kwa makini mafunzo ya usimamisi wa uchaguzi katika Mkoa wa Kilimanjaro mwaka 2015, ikiwa ni sehemu ya elimu ya upigaji kura. Picha ya Maktaba
Muktasari:
Leo tunaendelea kuangalia mahitaji ya kuelimisha wananchi kushiriki katika shughuli za uchaguzi kwa muda wote na kuanzia wakiwa watoto.
Wiki iliyopita tuliona umuhimu wa kutoa elimu kwa wapiga kura na jinsi gani bajeti inavyokwamisha utoaji wa elimu hiyo kwa upande wa Serikali na kwa taasisi za hiyari.
Leo tunaendelea kuangalia mahitaji ya kuelimisha wananchi kushiriki katika shughuli za uchaguzi kwa muda wote na kuanzia wakiwa watoto.
Bila kujali umri wa wananchi husika, kuna mahitaji mengi yanayohusiana na elimu kuhusiana na uendeshaji wa uchaguzi. Kuna mahitaji mengine yanayohusisha siasa za ushindani.
Kwa mfano, moja ya hitaji la elimu ya mpiga kura ni kuendesha zoezi la mfano wa uchaguzi (Mock Election) ili kutoa uelewa wa kutosha kwa wananchi kuhusu upigaji kura kwa kuweka wazi utaratibu mzima wa mchakato wa uchaguzi na kuondoa hisia potofu zilizojengeka miongoni mwa jamii kuwa huwa kuna wizi wa kura wakati wa uchaguzi.
Kwa mafano, nchini Chile siku ya upigaji kura, wapigakura huambatana na watoto wao na watoto hao pia hupiga kura sambamba na wazazi wao kwa lengo la kuwazoesha watoto hao kushiriki katika chaguzi kwa amani ili baadaye waweze kutumia haki yao kikamilifu.
Huu ni mfano mzuri wa kuiga kwani watoto hawa hujengewa siasa za uvumilivu mapema pamoja na kufanya maamuzi sahihi katika sanduku la kura kwa kuwachagua viongozi wanaowataka.
Kimsingi, mfumo wa elimu katika nchi ni moja kati ya nyenzo muhimu kwa wanaotoa elimu ya mpigakura. Mfumo huo utawasaidia wanaotoa elimu hiyo kufikiria nyenzo zilizopo kama fursa za mafunzo ya kuimarisha elimu ya uraia na elimu ya mpigakura.
Baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, elimu ya siasa ambayo ilikuwa inafundishwa kwa shule za msingi na sekondari ilisitishwa na badala yake somo la uraia likawa linafundishwa. Hata hivyo, ili kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu na shughuli za uendeshaji uchaguzi katika nchi ni muhimu elimu ya mpigakura ifundishwe sambamba na elimu ya uraia mashuleni.
Elimu ya Mpigakura hutolewa kusaidia usimamizi na uendeshaji mzuri wa uchaguzi ili kufikia lengo la kuwa uchaguzi huru na wa haki na kupunguza gharama zinazohusiana na uendeshaji huo.
Elimu hii inahusisha taarifa za msingi ambazo mpigakura anapaswa kuzipata ili kumhamasisha aweze kushiriki katika uchaguzi na aweze kupiga kura kwa ufasaha.
Vyombo vya habari vimekuwa vinahusika sana katika kutoa elimu ya mpigakura. Mbali na kutoa elimu hiyo, vyombo vya habari ni muhimu katika kuimarisha demokrasia na uchaguzi wa kidemokrasia.
Uchaguzi huru na wa haki siyo tu kuwa na uhuru katika kupiga kura, bali pia uelewa wa jinsi ya kupiga kura, ushiriki katika mchakato wa majadiliano na kupata taarifa kuhusu vyama vya siasa, sera za vyama, majina ya wagombea na sifa zao na mchakato mzima unaohusu uchaguzi ili kuwawezesha wapigakura kufanya maamuzi sahihi.
Vile vile, vyombo vya habari hutumika kama mlinzi wa uchaguzi wa kidemokrasia kwa kuweka uwazi katika mchakato wa uchaguzi. Kwa hakika, uchaguzi wa kidemokrasia bila vyombo vya habari ni mkanganyiko.
Mkurugenzi wa Idara ya Vijana ya Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani ambaye pia ni Profesa William Damon anasema “Hakuna hatari inayowakabili Wamarekani kuliko hata ugaidi kwa sasa, kama ambavyo wananchi wengi hawajui hatma ya maisha yao kwa kukosa wananchi ambao wanaweza kuendeleza uhuru ambao wamekuwa nao kwa miaka mingi.”
Profesa Damon anaongeza kuwa hali ikiendelea kama ilivyo sasa, vijana wengi wa Kimarekani wataishi bila kujua umuhimu wa jamii huru na faida zake.
Kauli hii ya Profesa Damon, inakuja kufuatia tathmini ya ufaulu wa somo la elimu ya uraia kwa Wanafunzi nchini Marekani kuwa unapungua siku hadi siku na kutishia kiwango cha Wamerekani wenye uelewa wa kutosha kuhusiana na uendeshaji wa shughuli mbalimbali zinazohusu elimu ya uraia nchini humo.
Wakati Wamarekani wanapata hofu kuhusu kushuka kwa kiwango cha uelewa katika elimu ya uraia, hapa nchini mwetu ndiyo tunaanza kutoa kipaumbele kwa jamii ya Kitanzania, tena kwa kiwango kidogo.
Wahenga walisema, “kawia Ufike” hivi ndivyo ambavyo Tume ya Taifa ya uchaguzi imeamua kutekeleza suala la kutoa elimu ya mpigakura kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa, Kailima Ramadhani, baada ya kutoa elimu ya mpigakura kwa umma kupitia maonesho mbalimbali, NEC imedhamiria kutoa elimu ya mpigakura katika vyuo vikuu vyote nchini.
Baada ya elimu ya Mpigakura kutolewa kwa muda mfupi na kutowafikia walengwa walio wengi mwaka juzi, NEC sasa imeamua kutumia kikamilifu fursa mbalimbali zinazopatikana kutoa elimu hiyo ili kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanapata elimu hii na kufahamu taratibu, kanuni na sheria zote zinazoendesha na kusimamia uchaguzi.
Kwa kuhitimisha, elimu ya mpigakura ni lazima itolewe sambamba na elimu ya uraia ili kuwapa uelewa wa kutosha wananchi walio wengi kuhusiana na uchaguzi.
Uchaguzi ulio huru na wa haki hauko kwenye kupiga kura tu, bali uhuru katika chaguzi ni pamoja na wapigakura kufahamu utaratibu mzima unaohusiana na mchakato wa uchaguzi.