Ahmed Kipande alivyong’ara na Kilwa Jazz

Ahmed Kipande 

Muktasari:

Wakati wa sherehe za Uhuru akiwa na bendi yake walitumbuiza wimbo wa kusifia Taifa huru.

Zanzibar. Ahmed Kipande ni mwanamuziki nguli aliyeshiriki kikamilifu katika uhamasishaji wa maendeleo na kupigania Uhuru wa Tanganyika akiwa na bendi yake ya Kilwa Jazz.

Bendi hiyo ya Kilwa Jazz ilishiriki kikamilifu siku Tanganyika inapata Uhuru Desemba 09, 1961 kwa kimba wimbo wa kusifia nchi yetu kupata Uhuru kutoka wa Wakoloni.

Chini ya uongozi wa Ahmed Kipande, Kilwa Jazz ilishiriki kikamilifu kutoa burudani wakati mikakati ya kufanya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye meneo ya makao makuu ya bendi hiyo jijini Dar es Salaam mwaka 1964.

Ahmedi Kipande na bendi yake waliteuliwa na Serikali ya Tanganyika kwenda kushiriki sherehe za Uhuru wa nchi za Malawi na Uganda.

Historia ya mwanamuziki huyu iliyotolewa na mwanawe wa mwisho Kipande Ahmed, aliyeeleza kwamba jina kamili la baba yake alikuwa ikiitwa Ahmed Mohammed Kipande na alizaliwa mwaka 1937 Kilwa Kivinje mkoani Lindi.

Miaka michache baada ya kifo cha mama yake, Ahmed Kipande alifuatana na baba yake kuja Dar es Salaam na akaanza masomo katika Shule ya Uhuru Wavulana eneo la Kariakoo, Dar es Salaam.

Katikati ya miaka ya 1950, Kipande alianza kupiga muziki akitumia ala iitwayo ‘Violin’, katika Bendi ya Tanganyika Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Zimbe Kidosi.

Bendi hiyo ilikuwa na makao makuu yake katika Mtaa wa New ambao sasa unaitwa Lumumba.

Wanamuziki wa miaka hiyo walianzisha bendi wakizipa majina ya maeneo wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga Jazz na kadhalika.

Ahmed Kipande aliyekuwa ametoka Kilwa Kivinje mkoani Lindi naye akishirikiana na mwanamuziki mwenzake aliyetajwa kwa jina moja la Shamte, nao wakaamua kuanzisha bendi ya watu kutoka Kusini ya Kilwa Jazz mwaka 1958.

Kilwa Jazz ikaanza kujizolea umaarufu kwa kutunga na kuimba nyimbo mbalimbali zikiwemo za siasa, mapenzi na za uhamasishaji kupata Uhuru wa Tanganyika.

Alitunga na kuimba wimbo wa ‘TANU yajenga nchi’, nchi yetu’ ‘Enyi vijana tujenga yetu, Doli na ‘It can be done, play your part’

Zingine zilikuwa za ‘Rozi wauwa’, ‘Nipate lau nafasi’, ‘Nacheka cheka Kilwa leo’ na ule wa Maneno hayafai’

Wimbo wa Nacheka cheka ulitungwa na Ahmed Kipande baada ya kukopi wimbo wa Tabu Ley na John Bokelo wa ‘Mokolo nokokufa’ halikadhalika nyimbo za Nacheka cheka Kilwa leo na Maneno hayafai ambazo kutoka wimbo wa ‘Course au Povouir’ wa T.P.OK. Jazz.

Mwaka 1973 Kilwa Jazz ilialikwa na kutumbuiza kabla ya onyesho la gwiji la muziki wa dansi, Franco Makiandi na Bendi ya T.P.OK. Jazz iliyefanya onyesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Luambo Makiadi baada ya kuzisikiliza nyimbo hizo alimfuata Ahmed Kipande na kumpongeza kwa umahiri wake wa ‘kokopi na kupesti’ pasipo kukosea.

Akimsifia baba yake Kipande Ahmed alisema kwamba mwaka 1961 siku Tanganyika inapewa Uhuru kutoka kwa Wakoloni, Bendi ya Kilwa Jazz ilikuwa uwanja wa taifa ikiporomosha muziki, ilitoka na wimbo wa kumshukuru Mungu kwa kupata Uhuru.

Mtoto huyo wa marehemu Ahmed, aliimba mistari michache ya wimbo huo …“ Ewe mola tunakuomba uibariki Tanganyika yetu na jirani zetu, Uhuru tumepata lakini Nyoyo zinasikitika wenzetu wanateseka, wakoloni wa mewashika…”

Bendi ya Kilwa Jazz ilikuwa na makao makuu yake katika kona ya Mitaa ya Muhoro na Jangwani ambapo siku moja ilipiga muziki nje ya ofisi yao na kuwashangaza watu kuona bendi ikipiga muziki mchana.

Lakini ilikuwa mipango kamambe ikipangwa maeneo hayo na viongozi wanamapinduzi siku chache kabla ya mapinduzi ya Zanzibar viongozi walikuwa wakipanga mikakati ya mapinduzi yaliyouondoa utawala wa Kisultani mwaka 1964 huko Zanzibar.

Bendi ya Kilwa Jazz baadaye haikueleweka na jamii kwa kuwa wengine wakafika mbali zaidi wakizusha maneno kwamba ni bendi ya Serikali ‘eti’ ilikuwa ikialikwa kutoa burudani katika sherehe nyingi za kitaifa.

Kilwa Jazz pia ilialikwa kutoa burudani katika sherehe za ndoa ya mmoja wa mawaziri wa Serikali ya Tanganyika wakati huo, Oscar Kambona.

Ahmed Kipande katika sherehe hiyo alionyesha kipaji chake kwamba siyo cha kubahatisha. Alitunga wimbo wa papo kwa papo wa kuwasifia wanandoa hao Oscar Kambona na mkewe.

Yaelezwa kwamba Kambona aliinuka kutoka kwenye kiti cha maharusi na kwenda kumkumbatia Kipande, kisha akamtunza pesa.

Ni miaka 27 sasa tangu Ahmedi Mohammed Kipande afariki dunia, Aprili 27, 1987 baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi kwa kipindi kirefu.

Alizikwa kwenye makaburi ya Tandika Maguruwe, mkoani Dar es Salaam Aprili 28,1987.

Mungu ailaze roho ya marehemu Ahmedi Kipande Mahala pema peponi, Ameni.