Mwanamume mmoja anamiliki wanawake sita (2)

Ombi Sanga ambaye ni Mhudumu w Afya ya msingi katika kijiji cha Ivalalila. Picha na Herieth Makweta
Muktasari:
Joyce Stone Mbilinyi (40) anasema: “Mimi nafanya shughuli za kulima, kukusanya magogo na kuchoma mkaa ili nipate fedha za kuniwezesha na familia yangu. Moto ukiathiri maeneo mengine hulipa faini ya Sh50,000 na kifungo juu.
Wiki iliyopita tuliwaletea sehemu ya kwanza ya makala haya kuhusu Kijiji cha Ivalalila wilayani Makete, Mkoa wa Njombe ambapo pamoja na mambo mengine ilieleza namna wanaume wa eneo hilo wanavyomiliki wanawake zaidi ya watano bila kujali athari zake. Leo tunawaletea sehemu ya mwisho. Endelea..
Joyce Stone Mbilinyi (40) anasema: “Mimi nafanya shughuli za kulima, kukusanya magogo na kuchoma mkaa ili nipate fedha za kuniwezesha na familia yangu. Moto ukiathiri maeneo mengine hulipa faini ya Sh50,000 na kifungo juu.
Wapo wanaume wanaosaidia lakini si wote. hapa kijijini kuna mambo mengi yasiyo mazuri hasa kuhusu suala la jinsia. Mwanamke anachukuliwa kama chombo cha starehe na mtumwa.”
Wanaume wanasemaje
Efedi Eskaka Chaula (40), anakiri kuwapo na tabia ya wanaume kumiliki wanawake zaidi ya sita akisema: “Ni kweli, wanaume tuna wanawake wengi hapa kijijini, lakini si kwamba wanaume ndiyo wanatafuta wanawake ingawa wapo wanaorithi wajane wa kaka zao au wadogo wao.
Ukweli ni kwamba wanawake wengi wanawahonga wanaume, ndiyo maana nao wanalazimika kuwa na wanawake wengi. Hata hivyo ni kama mila na desturi za kurithi na mitindo ya maisha kwa hapa kijijini.”
Naye kijana aliyeomba kutambulika kwa jina moja la Peter ( 21) anasema: “Mimi nina wanawake saba, wawili ni wasichana wadogo wanasoma sekondari na hawa watano ni wakubwa sana tu. Hawa wananipa fedha, zinanisaidia kumpa msichana ninayempenda, huyu mwingine natembea naye tu.”
Alipoulizwa kama anafahamu kuhusu gonjwa la Ukimwi Peter alijibu: “Kwa kweli najua, ila nimekata tamaa kwani najua lazima nimeathirika, sijawahi kupima kwa hiari ila kuna wanawake niliotembea nao zamani sana nikiwa na miaka 14 walishafariki kwa Ukimwi, hivyo na mimi najua ninao.”
Alipoulizwa iwapo ana ndoto za kuoa, Peter anajibu: “Nampenda sana msichana mmoja, lakini siwezi kuoa kwa kuwa najua atapata mimba na akienda kupimwa itagundulika kuwa ana Ukimwi hivyo ninaweza kufa haraka.”
Anasisitiza kuwa wanaume wengi waliopima na kugundulika na Virusi vya Ukimwi hufa haraka.
Hata hivyo Peter ni tofauti na Eliudi(26), anayedai kuwa wanawake wengi kijijini hapo wanaongea sana.
“Wanawake wengi wanaongea sana, wana gubu. Hili ndilo lililonihamisha kwa mke wangu wa awali na kuanza kuambatana na wanawake wengine,” anasema Eliud aliyekataa kutaja idadi ya wanawake alionao.
Ukimwi unavyosambazwa
Janga la Ukimwi haliishii wilayani Makete pekee kwani wasichana wengi waliowahi kufanya kazi nje ya kijiji hicho wanaelezea majanga waliyowahi kukutana nayo huko.
Neema mwenye miaka 44(si jina lake halisi) anasema: “Nilifanya kazi za ndani kwa kipindi cha miaka miwili, huko nilikutana na wanaume wengi wakiwamo waajiri wangu ambao walinitaka kimapenzi. Nilishiriki nao ngono kwa kuwa walinipa fedha, lakini baadaye niligundua kuwepo Virusi vya Ukimwi katika damu yangu. Sijajua nilipata nikiwa Makete au huko huko, kwani nilianza ngono nikiwa na miaka 13.”
Anasema kuwa baada ya kufuatilia waajiri wake wawili aligundua, kwamba mmoja aliyefanya kazi kwake awali na kuwahi kutembea naye alishafariki kwa ugonjwa wa Ukimwi.
Neema mwenye mtoto mmoja alirudi kijijini hapo miaka 10 iliyopita, lakini kwa kipindi chote amekuwa akitumia dawa za kufubaza makali ya Ukimwi ARV. Eliud aliyebainisha kutokuwa tayari kupima Virusi vya Ukimwi anasema aliwahi kufika jijini Dar es Salaam Juni 2010 “Nilipotofautiana na mke wangu, nilienda huko nikafikia Mbagala kwa rafiki yangu.
Yeye alikuwa akifanya biashara za vitunguu kutoka Iringa. Miezi saba niliyoishi huko nilikutana kimwili na wanawake zaidi ya watano, sikutumia kinga ila kwa mwanamke mmoja tu aliyenitaka nifanye hivyo. Wakati huo tayari nilikuwa na wasiwasi kuwa huenda nimeathirika, wasiwasi ambao mpaka leo ninao.”
Anasema kuna wanawake ambao hajui idadi yao aliokuwa akiwanunua maeneo ya Buguruni maarufu kama ‘Kimboka’ akieleza kuwa hakuwahi kutumia kinga kwa wanawake hao aliosema wanajiuza kwa bei rahisi tofauti na wanawake wanaojiuza kijijini hapo.
Uongozi wa kijiji
Mwenyekiti wa Kitongoji Gilifeli Chaula, anaeleza:”Semina mbalimbali zinatolewa kijijini hapa lakini bado hazisaidii, kwani wanaume ni wabishi na wajuaji, hivyo inakuwa ngumu kuwabadilisha misimamo yao.”
Anaongeza: “Wanaume wa hapa kijijini ni wafanyaji wa kazi ngumu, lakini wakipata fedha hukimbilia kwenye pombe na wanawake. Kuna wanawake hufika hapa kijijini kwa ajili ya kujiuza tu na hawa wanatoka mijini.”
Kaimu Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Nole Duniani Sanga anasema kuwa wanaume wengi wanalalamikia tabia za wake wao kuongea sana na wengi hufanya uamuzi usio sahihi.
Hata hivyo anaeleza kuwa tatizo hilo limesababisha idadi kubwa ya vijana kuondoka kijijini hapo, kwenda kutafuta afadhali ya maisha katika miji mikuu ya nchi kutokana na hofu ya kuambukizwa Ukimwi.
Viongozi Wilaya ya Makete
Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Makete, Leoncek Panga anasema kuwa aliwahi kukutana na kinamama wakamweleza hilo, lakini bado nilipokwenda kwa wengine hawakuweza kumweleza lolote na kuwa tatizo ni usiri walionao kwani katika semina wanazopewa hawaelezi matatizo yao inakuwa vigumu kung’amua tatizo kama hilo.
Anasema kuwa Ivalalila ni kijiji anachokitembelea zaidi kutokana na matatizo yaliyopo kijijini hapo. “Ninawaelimisha mara nyingi kuhusu suala hili, lakini wengi wao wanaonekana kukata tamaa, warsha na semina haziwasaidii,”anasema Panga.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Makete, Josephine Matiro anasema: “Sijawahi kusikia habari hii. Ni mpya kwangu. Ingawa mimi hufika Kijiji cha Ivalalila lakini wananchi wa pale ni wasiri mno. Nitalifuatilia hilo, lakini nina mkakati wa kuanzisha semina kwa vijana ili kusaidia kuondokana na dhana mbaya na umasikini.”
Anafafanua: “Mwanamke ana haki ya kukataa ngono, siyo lazima ampe mwanaume kila kitu anachohitaji huku akijua kina madhara kwake. Lakini wanaume wengi wa hapa wanafanya kazi kwa juhudi kubwa sana, upande wa matumizi yao ni ngumu kufahamu, huenda malalamiko ya wanawake yana msingi ni lazima yafanyiwe kazi.”
Matiro anasema kwamba kuna mikakati makini aliyoiweka kuhakikisha vijana wanakopeshwa na Benki ya Njocoba iliyopo Njombe mjini kwa ajili ya kufanya kazi mbalimbali za mikono na kilimo ili kuondokana na umaskini na kutokomeza janga la Ukimwi.
Mbunge wa Viti Maalumu CCM aliyepo katika Kamati ya Ukimwi, Leadiana Mng’ong’o anasema: “Nimeshafika katika kijiji hicho na hiyo ndiyo hali halisi, lakini elimu bado na walio wengi hawazingatii ushauri wa wataalamu. Kubadili tabia ndiyo hasa suala la msingi litakaloifikisha jamii ya Ivalalila katika hatua nzuri, kwani kijiji sasa kimeoza. Ni vyema watu wakabadili tabia.”
Anatanabahisha kuwa watu wengi siyo wadadisi kuhusu maisha ya mtu anayekutana naye kimapenzi akitahadharisha kwamba jambo hilo ni hatari.
“Wewe umekutana na mwanamke mjane, hujui mumewe emefariki kwa sababu gani nawe unajitumbukiza. Ndiyo, kama hujui kuhusu afya yako, kama una maambukizi, unaingiza maambukizi mapya hapo. Kama umeoa na ukawa na wake watano basi mkitegemezana hakutakuwa na hofu ya janga la Ukimwi, lakini huwezi kujua kama wote hawa watakuwa waaminifu,” anasema Lediana.
Anaasa kuwa ni vyema wakazi wa kijiji hicho wakatokomeza mila potofu wanazoendelea kuzikumbatia mila potofu, akionyesha masikitiko kwamba licha ya kufika mara kwa mara katika kijiji hicho kutoa elimu, lakini wakazi wake bado hawabadiliki.
“Nadhani hapa tuwajengee uwezo wanawake kwani tuna mkakati wa kutokomeza Ukimwi mpaka ufikie sifuri mwaka 2015,” anasema Mng’ong’o ambaye hivi karibuni alipata tuzo ya kimataifa ya Champion Awards kutokana na umahiri katika masuala ya Ukimwi, unyanyasaji wa kijinsia, sera na masuala ya uzazi na uzazi wa mpango.