Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaondoa marufuku ya mifuko ya plastiki

Muktasari:

Uamuzi huo ulitolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais juzi, wakati Naibu Waziri wa Mazingira, Luhaga Mpina na Mkurugenzi wa Mazingira, Dk Julius Ningu walipozungumza na waandishi wa habari kuhusu Siku ya Mazingira Afrika.

Dar es Salaam. Serikali imetengua amri ya kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki nchini baada ya kubaini kuwa itapunguza kasi ya uwekezaji na kuziweka rehani ajira za watumishi wa viwanda vinavyozalisha bidhaa hizo.

Uamuzi huo ulitolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais juzi, wakati Naibu Waziri wa Mazingira, Luhaga Mpina na Mkurugenzi wa Mazingira, Dk Julius Ningu walipozungumza na waandishi wa habari kuhusu Siku ya Mazingira Afrika. Akieleza kuhusu mifuko hiyo, Dk Ningu alisema Serikali imeamua kufanya hivyo ili kulinda viwanda vilivyoajiri mamia ya Watanzania tofauti na nchi nyingine zilizofanikiwa kuondoa matumizi yake kwa kutokuwa na wazalishaji wa ndani.

“Tunazo kampuni 26 zinazozalisha mifuko hiyo. Hatuwezi kuwaambia wasitishe uzalishaji wakati Serikali yenyewe inasisitiza uwekezaji na wao tayari wameajiri watu kadhaa mpaka sasa,” alisema.

Alifafanua kuwa mifuko itakayozalishwa itapaswa kuwa ya zaidi ya maikroni 30 itakayoweza kutumika zaidi ya mara moja, hivyo kupunguza inayotupwa na kuzagaa mitaani.

Agosti mwaka juzi, aliyekuwa waziri wa Mazingira, Dk Theresia Huvisa alipiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo na kutangaza ndani ya miezi mitano iliyokuwapo iwe imeshatumika na kusiwapo na uzalishaji au uagizaji mwingine.

Wakati waziri huyo akisema kuwa mifuko hiyo ni hatari kwa afya za binadamu na mazingira, Dk Ningu alisema haina matatizo na kubainisha kuwa tatizo lipo kwa watumiaji kuitupa hovyo.

Akisoma tamko la Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba, kuhusu maadhimisho ya siku hiyo, Mpina alisema kila mwananchi na mdau wa mazingira anapaswa kutimiza wajibu wake ili kupunguza athari za tabianchi zenye madhara makubwa kwa taifa na dunia.

Mpina alisema maadhimisho hayo yanalenga kujadili, kupitia na kurejea mikakati na mipango ya utunzaji wa mazingira na kuainisha changamoto zilizopo ili zitafutiwe ufumbuzi wa kudumu.

“Halmashauri hazikusanyi kati ya asilimia 80 na 90 ya taka zinazozalishwa kila siku hivyo kufanya baadhi ya miji kukithiri kwa uchafu. Serikali imeagiza kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi iwe ni ya kufanya usafi,” alisema Mpina.

Ili kujenga uwezo wa kuziondoa taka zinazokusanywa, naibu waziri huyo alisema ameziagiza halmashauri zote kuvunja mikataba na wazabuni ambao hawawezi kutekeleza majukumu.

Pia, alisema Serikali imezamilia kuwavutia wawekezaji wa viwanda vya kuchakata taka waanze nao kuzalisha umeme ambao utakuza sekta nyingine za uchumi huku ukiondoa kero iliyopo sasa.