Chifu Yemba bado anautaka urais, achukua fomu kuomba ridhaa

Kada wa Chama Cha Wananchi (CUF), Chifu Yemba amechukua fomu ya kutia nia kuwania Urais wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Muktasari:
- Hatua ya Yemba kuchukua fomu hiyo inafikisha idadi wanachama wawili kuitaka nafasi hiyo kwenye chama hicho.
Dar es Salaam. Kada wa Chama cha Wananchi (CUF), Chifu Yemba amechukua fomu ya kuomba ridhaa kwa chama chake kuwania nafasi ya urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Yemba aliyewahi kuwania nafasi hiyo mwaka 2015 kupitia Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), amekabidhiwa fomu hiyo leo Jumanne Julai Mosi, 2025, katika ofisi za chama hicho zilizopo Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza.
Hatua ya Yemba kuchukua fomu hiyo inafikisha idadi wanachama wawili wa chama hicho kuania nafasi hiyo akitanguliwa na Kiwale Mkungutila, huku kwa upande wa aliyechukua fomu akiwa Hamad Masoud Hamad pekee.
Akizungumza na Mwananchi baada ya kukabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa CUF Wilaya ya Nyamagama, Amran Amran, kada huyo amesema licha ya kuwania nafasi hiyo mara kadhaa bila mafanikio, lakini anaamini bado anayo fursa ya kuingia tena kuomba ridhaa hiyo.
“Nimechukua fomu ya kutia nia leo katika ofisi za chama chetu Nyamagana,”amesema Yemba.
Awali, Katibu Mkuu wa CUF, Husna Mohamed Abdallah akizungumza na Mwananchi alisema huenda idadi hiyo ikaongezeka kwa sababu pazia la uchukuaji na urejeshaji fomu linatarajiwa kufungwa rasmi Julai 15,2025.
“Nafasi ya urais wa Tanzania ni hao wawili Yemba na Mkungutila lakini tunategemea idadi itaongezeka kwa sababu muda bado upo wa watu kutia nia kabla ya kujifungia na kufanya mchujo wa kumpata mmoja,” amesema Husna.
Alipoulizwa kuhusu Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kama ana mpango wa kuchukua fomu, amejibu kuwa hajaonesha nia bado.
“Nafikiri tusimsemee ingawa hajaonyesha nia pengine huenda anaweza kuonyesha nia hiyo baadaye, kwa kuwa muda bado upo, jambo lolote linaweza kujitokeza,” amesema Husna.
Akimzungumzia Romanus Mapunda aliyejiunga na chama hicho hivi karibuni kutoka Chadema, Husna amesema yuko mbioni kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ya ubunge jimbo la Mtwara Mjini.
Amesema awali, Mapunda alionyesha nia ya kutaka kuomba kuwania kiti cha urais, lakini amebadili nia yake hiyo.
“Katika nafasi zingine za udiwani na ubunge shughuli za uchukuaji na urejeshaji fomu zinaendelea mikoa yote na mpango wetu baada ya mchakato huu kukamilika tutajifungia kufanya mchujo,” amebainisha Husna.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa CUF Tanzania Bara, Othman Dunga amesema shughuli zingine zinaendelea ikiwamo kufanya mikutano ya hadhara na kuzindua matawi.
“Tuko mkoani Mtwara tunaendelea na mikutano ya hadhara sambamba na kufungua matawi na kupokea wanachama wapya wanaojiunga kutoka vyama vingine,” amesema Dunga.
Amesema wamejipanga kwenda kushindana katika uchaguzi mkuu kwa kuweka wagombea wanaokubalika baada ya kufanyika mchujo wenye haki na unaozingatia sifa.
Chaumma
Katika hatua nyingine, licha ya jana, Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kufungua pazia lake la uchukuaji na urejeshaji fomu, lakini mpaka leo alasiri hakuna kada aliyejitokeza kuchukua fomu.
Jana Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu alipuliza kipyenga kwa wanachama wote wenye nia ya kugombea nafasi ya ubunge na udiwani kupitia chama hicho, wajitokeze kuchukua fomu kuanzia leo Julai Mosi, huku akisema nafasi ya urais imewekwa kiporo.
Pamoja na kufungua milango hiyo kiliweka masharti kwa anayetaka kugombea ubunge au udiwani viti maalumu, sharti aanze kuonyesha nia ya kugombea kata au jimbo kwa nafasi tarajiwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Mwananchi imezungumza na Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara wa chama hicho, Benson Kigaila leo, amesema kwa kuwa shughuli imeanza, wataanza kujitokeza kuanzia kesho na kuendelea kwa kuwa muda bado upo.