Kila Mtanzania ni mshindi kwa alichofanya Rais samia
Mikutano ya siasa huru. Katiba mpya tunaiendea. Sheria kandamizi za vyama vya siasa zinafanyiwa mapitio kuelekea kuzirekebisha.
Yupo mtu anajiuliza, mshindi nani? Aliyeruhusu au walioruhusiwa?
Jawabu ni hili; wote wameshinda. Maana ushindi wa jumla ni wa Watanzania. Tamko la Rais Samia Suluhu Hassan, kuruhusu mikutano ya vyama vya siasa limelinda Katiba.
Hivyo Rais Samia ni mshindi kwa sababu amelinsa Katiba.
Ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa mantiki hiyo kila Mtanzania ni mshindi kwa sababu Katiba yao imelindwa.
Ulitokea wakati Katiba haikuheshimiwa, ikavunjwa kurejea kwenye mstari wa kuiheshimu na kuilinda, inapaswa kuwapa tabasamu Watanzania wote.
Ibara ya 20 ya Katiba inasema: “Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.”
Kikosi Kazi kilichoteuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Francis Mutungi, na kuungwa mkono na Rais Samia, ripoti yake ilikuwa na mapendekezo 19.
Mojawapo ilikuwa kuruhusiwa kwa mikutano ya vyama vya siasa. Hivyo, Kikosi Kazi nacho kimeshinda.
Vyama vyote vya siasa vilivyoamua tangu awali kushirikiana na Kikosi Kazi ili kuchakata agenda na hoja za kukwamua shughuli za kisiasa, vimeshinda. Sauti zao zimesikika. Rais Samia ameruhusu. Na amesema mikutano ni haki ya vyama.
Hata Chadema waliokataa kushirikiana na Kikosi Kazi kwa hoja ya kutokuwa na imani na baadhi ya wajumbe, nao wameshinda. Sauti yao ilisikika.
Chadema walikutana na CCM. Walizungumza. Rais Samia alikiri kuzingatia hoja zao hadi kufikia uamuzi wa kuruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, aliitwa majina mengi. Mitandaoni alipewa jina la dalali. Kwamba alikuwa akitumiwa na dola kusambaratisha upinzani.
Yeye alisema anashiriki mchakato wa kutengeneza barabara nzuri ya kisiasa.
Kwa mkutano wa Rais Samia na viongoz wakuu wa vyama vya siasa, na uamuzi uliofikiwa, bila shaka Zitto ni mshindi.
Waliokuwa wakimkejeli kwa maneno mbalimbali ya kashfa, wameona matunda ya mchakato alioamua kuushiriki ili kuleta mwanga mpya wa shughuli za kisiasa.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, tangu alipoachiwa huru Machi 4, 2022, kwa hati ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi, alionekana mpole.
Hakuwa yule aliyezoeleka wa harakati ngumu za kudai Katiba na mabadiliko.
Machi 9, 2022, Mbowe alipokuwa Iringa kuhudhuria kongamano lililoandaliwa na Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani (Machi 8), alisema kuwa alikubaliana na Rais Samia kujenga nchi yenye upendo, mshikamano na kuaminiana.
Kauli hiyo ya Mbowe na mabadiliko yake, akionekana kuwa laini, huku akifanya vikao kadhaa Ikulu na Rais, wapo waliombeza, wakasema amenunuliwa. Mbowe alisema, yapo mambo ya ndani alikubaliana na Rais Samia, ambayo haikuwa vizuri kuyasema hadharani.
Baada ya Rais Samia kuruhusu mikutano ya hadhara, hakuna tena wa kumbeza Mbowe kufanya vikao Ikulu mara kwa mara na mabadiliko yake.
Mbowe ni mshindi, kwani alijua nini alikitafuta na njia ipi ilikuwa sahihi.
CCM ni washindi. Imeonekana kuwa kama chama hawakuwahi kuwa na mkono katika kuzuia mikutano ya kisiasa.
Ulikuwa uamuzi binafsi wa aliyekuwa Mwenyekiti wao, Dk John Magufuli.
Nini kifuate?
Kujadili nini kifuate lazima tutazame kilicholeta mkwamo. Katiba imempa mamlaka Rais hata ya kuikanyaga.
Soma ibara kwa ibara hadi kumaliza zote, huoni mahali Katiba imewekewa ukuu wake.
Anapotokea Rais ambaye hapendi kukosolewa, anayetaka kufanya mambo yake bila kuhojiwa mithiri ya Dk Magufuli, ndio hukuta nchi inafungwa kisiasa. Shughuli za vyama vya siasa zinaharamishwa.
Kipindi cha Magufuli ilikuwa kufanya siasa ni kama biashara ya magendo.
Rais Samia, ameamua kuuhami mfumo wa vyama vingi vya siasa. Anaondoa chuki za kisiasa na kuruhusu mwanzo mpya wa siasa za kusikilizana sikio kwa sikio badala ya kutazamana jicho kwa jicho. Anaomba akosolewe kwa staha.
Kumaliza manung’uniko
Manung’uniko ya wapinzani yameondoka. Kesi za kisiasa nyingi zimefutwa. Waliokuwa na vilio vya kudhulumiwa stahiki zao kisiasa wamelipwa. Mfano ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, Tundu Lissu, alishakiri kulipwa fedha zake zote. Kuanzia matibabu, mishahara na kiinua mgongo cha ubunge.
Habari za kuaminika ni kwamba hata Mbowe, kuna madai yake ya jengo lililokuwa na Klabu ya Bilicanas, Posta, Dar es Salaam, lililovunjwa, shamba lake la Green House, Hai, Kilimanjaro, lililoharibiwa na mengineyo yanafanyiwa kazi.
Mpaka hapo, unarejea kwenye kauli ya Mbowe kuwa walikubaliana kufanya siasa zenye kulijenga taifa kwa upendo, kuheshimiana na kuaminiana. Tofauti za kisiasa au kiitikadi, zisiwe sababu ya kuharibiana au kudhulumiana mali.
Kuna sura mbili, ya Samia na Magufuli. Mmoja hakutaka kutabasamu na wapinzani wake wa kisiasa. Na aliamini kuwa njia ya kushinda uchaguzi ni kuwaminya wapinzani wake, wakose nguvu halafu afanye siasa peke yake aendelee kuchaguliwa na kuongoza.
Mwingine hana shida kutabasamu na wapinzani wake. Tena anasema si wapinzani bali wanaomsaidia kuona changamoto za nchi. Anaomba akosolewe, ajirekebishe, awatengenezee Watanzania maendeleo, aaminike na kuchaguliwa tena aendelee kuongoza.
Upinzani si uadui
Kabla ya Rais Samia na Magufuli, alikuwepo Rais Jakaya Kikwete, aliyependa kuketi na wapinzani wake wa kisiasa, alikunywa nao kahawa, walizungumza na kupoza joto.
Wanasiasa walikuwa huru kufanya mikutano kadiri walivyojisikia naye alikuwa tayari kuvumilia walichokisema na kukifanya.
Septemba 2017, Kikwete alipokuwa kwenye mkutano wa Jukwaa la Uongozi Afrika (ALF), uliofanyika Boksburg, Johannesburg, Afrika Kusini, aliikuna na kuipatia vilivyo jumuiya ya wapenda demokrasia.
Kikwete, aliikuna zaidi jumuiya ya vyama vya upinzani barani Afrika, kutokana na mada aliyotoa, akisema kuwa watawala hawapaswi kuwaona wapinzani wao kuwa maadui, badala yake wawachukulie ni washirika katika ujenzi wa utawala bora.
Rais huyo wa Nne wa Tanzania na Mwenyekiti wa Nne wa CCM, alisema kuwa vyama tawala na vya upinzani si maadui bali ni washindani.
Kwamba uwepo wa wapinzani ni kuwasahihisha watawala pale wanapofanya makosa na kuwazindua wanapolala.
Alichokizungumza kingine ni kuwa watu wa chama tawala wanaweza kutoona au kukosa ujasiri wa kuyasema makosa ya kiongozi wao aliye madarakani, hivyo wakawa wanaunga mkono makosa.
Mantiki hapo ni kuwa watawala badala ya kuwafurahia wanaowaunga mkono kwa kila jambo, wanapaswa kujitenga nao, maana huwapotosha kwa kuwavimbisha kichwa hata mahali ambapo wanavuruga.
Ni kwamba watawala badala ya kuwachukia na kuwanunia wapinzani wao, wanapaswa kuwategea sikio maana ndio ambao wanawawezesha kuyajua makosa na mahali ambako kunakuwa na upungufu.
Watawala wengi huwachukulia wapinzani wao kuwa ni wapiga kelele, walalamikaji na wasioona jema lolote la Serikali. Kwa msingi huo, huamua kuziba masikio na kutotaka kusikia chochote kutoka kwa viongozi wa vyama pinzani.
Tumefikaje sasa?
Utaona kuwa Kikwete na Samia wana mitazamo inayofanana. Hata hivyo, katikati ya Kikwete na Samia mabadiliko yalikuwa makubwa. Ofisini alikuwepo Dk Magufuli. Kwa maana hiyo, upepo wa kisiasa unaenda kulingana na matakwa ya mtu.
Nimekuwa nikifanya marejeo ya kitabu cha Profesa wa Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Chuo Kikuu cha Southern California, Gerardo Munck, kinachoitwa “Modes of Transition and Democratization” – “Miundo ya Mpito na Usimikaji Demokrasia”, kwa kuwa kina mantiki sana katika kuzielezea siasa za Tanzania.
Dhana ya “Revolution From Above” – “Mapinduzi Kutoka Juu”, iliyoelezwa na Munck, ukiitafsiri kwa ufasaha, utaelewa ni kwa nini mazingira ya siasa hubadilika kulingana na matakwa ya kiongozi. CCM waliruhusu mfumo wa vyama vingi. Waliunda sheria na kuandaa mazingira.
CCM hawakulazimishwa. Ndio maana Rais Samia alisema, alimwambia Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, kuwa chama chao ndio mzazi wa vyama vyote. Mazingira ya ujio wa mfumo wa vyama vingi ndio sababu.
Ukijumlisha ulaini wa Katiba pamoja na sheria zenye kulalamikiwa, hali ya kupwa na kujaa kwenye sura ya siasa za nchi, itaendelea. Akiondoka Samia, akija mwingine asiyetaka kuguswa, kuhojiwa wala kukosolewa kama alivyokuwa Magufuli upepo utarudi kulekule.
Suluhu ya jumla ili nchi isirejee ilipotoka ni Katiba bora. Shughuli za kisiasa zitambuliwe na zipewe ulinzi kwenye Katiba. Sheria zenye kuongoza shughuli za kisiasa zisitungwe kwa lengo la kukomoana bali ujenzi wa nchi kwa miaka mingi ijayo. Katiba izingatie maoni ya wananchi. Sio matakwa ya vyama au watawala.