ACT-Wazalendo wahamia Pemba kukusanya maoni hatima SUK

Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Othman Masoud akizungumza na wanachama wa chama hicho wa Wete, Pemba katika mwendelezo wa ziara yake  kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mwenendo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Muktasari:

Baada ya kukusanya maoni ya wanachama wa ACT-Wazalendo wa Mjini Unguja, makamu mwenyekiti wa chama hicho, Zanzibar, Othman Masoud amehamia kisiwa cha Pemba akishirikiana na mwenyekiti wake, Juma Duni  Haji.

Dar es Salaam Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Othman Masoud Othman leo Jumapili, Desemba 4, 2022 ameanza ziara Pemba ya kukusanya maoni ya wanachama wa chama hicho, kuhusu mwenendo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Hatua hiyo imekuja baada ya Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar kufanya ziara kama hiyo katika mikoa ya kichama ya ACT-Wazalendo ya Mjini Unguja iliyofanyika kwa nyakati tofauti wiki iliyopita.

Pia, ukusanyaji wa maoni hayo umekuja baada ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kumteua Thabit Idarous Faina kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Faina analalamikiwa na ACT-Wazalendo wakidai utendaji akiwa kwenye taasisi miaka iliyopita haukuwa wa haki na usawa.

Kinacholalamikiwa na ACT -Wazalendo ni kwamba Faina ndiye alikuwa bosi wa ZEC katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ulioshuhudia wagombea wao zaidi ya 16 wakienguliwa bila sababu za msingi na uchaguzi ukifanyika katika mazingira ambayo yasiyo huru wala ya haki.


Kutokana na hatua hiyo, ACT-Wazalendo iliazimia kushuka chini kwa wanachama na wananchi wa Zanzibar ili kupokea maoni yao kuhusu mwenendo wa SUK ndani ya miaka miwili kama una nia njema kwa Wazanzibari.


Katibu wa Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT- Wazalendo, Salim Bimani ameliambia Mwananchi leo Jumapilli Disemba 4,2022, Othman baada ya kufika Pemba alikwenda moja kwa moja katika mkoa wa kichama wa Wete kuzungumza na wanachama wa ACT.


“Kesho itakuwa zamu ya mwenyekiti (Juma Duni Haji), kuzungumza na kupokea maoni ya wanachama wa mkoani, Chakechake na Micheweni kuhusu mwenendo wa SUK. Mchakato wa ukusanyaji wa maoni haya utakamilika Disemba 6 mwaka huu.


“Desemba na Disemba 8 tutazindua kampeni za jimbo la Aman shughuli itakayoongozwa Kiongozi wa chama, Zitto Kabwe,” amesema Bimani.


Wiki iliyopita baadhi ya wanachama wa ACT-Wazalendo wa Unguja waligawaganyika katika maoni yaliyokusanywa na viongozi wa chama hicho, kuhusu mwenendo wa SUK kwa chama hicho kubaki au kujitoa ndani ya Serikali hiyo.


Baadhi yao walisema ni vyema ACT-Wazalendo ikaendelea kubaki ndani ya SUK ili kujua kinachoendelea katika Serikali huku wengine wakitaka chama hicho, kijitoe kwa madai ya kwamba walichookubaliana hakitekelezwi. Wengine walikwenda mbali zaidi wakitoa masharti mbalimbali ya kubaki ndani SUK.


Walieleza hayo kwa nyakati tofauti mbele ya Othman aliyekuwa akiongoza mchakato wa kukusanya maoni ya wanachama kuhusu hatua hiyo, akishirikiana na Duni.


Kombo Ussi Juma alikishauri chama hicho, kijiondoe akidai Serikali haitendei haki uwepo SUK. Alisema baadhi ya Wazanzibari walikuwa na imani SUK itawavusha kutoka katika changamoto mbalimbali, lakini imekuwa tofauti.


Wakati Sirima Khamis Hamza alisema, “mheshimiwa Othman upo kwa mujibu wa sheria usijaribu kunyanyuka katika kiti chako bali ongeza juhudi ili kila kitu kilichokubaliwa katika maridhiano basi kitendeke.Tunataka kila mwezi utoe taarifa ya namna makubaliano ya maridhiano yaliyotekelezwa ili tusonge mbele,”


Akizungumzia maoni hayo, Masoud alisema mchakato huo ndio utaratibu wa ACT-Wazalendo unavyowaelekeza kuwasikiliza na wameyachukua maoni yao na kwa ajili ya kuyafanyia kazi.


 “Wapo wanaosema tutoke na wengine tubaki, hiki ndicho tunachokitafuta, kila mmoja ana mawazo na sababu zake. Huu ni mwanzo tutakwenda katika mikoa yote, ni kweli kuna mambo hayakubaliki ikiwemo uteuzi wa Faina kama ambavyo chama kilivyotoa msimamo,” alisema.