ACT Wazalendo wakoleza sauti upatikanaji Katiba Mpya

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto kabwe akiwapungia mkono wafuasi wa chama hicho wakati akiwasili katika uwanja Tangamano uliopo jijini Tanga,Machi 8, 2023 kwa ajili ya mkutano wa hadhara wa chama hicho. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Safari ya kutambulisha dira ya ' ahadi yetu  ya ACT - Wazalendo yaanza huku kiongozi wa chama hicho Zitto Kabwe akisema watajikita kueleza changamoto za wananchi zipatiwe ufumbuzi  na sio kutukana watu.

Tanga. Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amesema katika mikutano yao ya hadhara watakayoifanya maeneo mbalimbali  hawatatukana  watu bali watazungumza masuala yanayohusu wananchi ili kupatiwa ufumbuzi na si vinginevyo.

Amesema lengo ni kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo husika zinapatiwa ufumbuzi ili kuboresha maisha yao kupitia shughuli za uchumi. Amesema ACT- Wazalendo ni chama cha tofauti kinachosimamia maslahi ya  Watanzania.

Ameeleza hayo leo Jumatano Machi 8, 2023 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Tangamano jijini Tanga, akisema mkutano ni mwanzo wa safari ya kujenga 'Taifa la Wote na Maslahi ya Wote'.

Amesema Tanga na Pwani ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika na vitendo ya wananchi wake kumbambikiziwa kesi, akisema chama hicho hakitachoka kuzungumza ili kuzuia vitendo hivyo visijirudie tena.

" Nikiwa hapa namkumbuka mzee wangu Salum Shamte (Mkurugenzi wa zamani wa Katani Limited- marehemu aliyefariki dunia mwaka 2020) ambaye alibambikizwa kesi ya uhujumu uchumi.

"Haya ni sehemu ya madhila tulipitia katika miaka saba iliyopita kwa watu kubambikiziwa kesi mbalimbali mfano mzuri mwenyekiti wetu wa mkoa huu aliyekaa miezi mingi gerezani," amesema Zitto.

Kutokana hilo, Zitto anasema ndio maana ACT - Wazalendo inasisitiza  uwepo wa Tume ya haki na ukweli ili kila mtu aliyeumizwa au kukumbwa na madhila mbalimbali ikiwemo kubambikiziwa kesi kwenda kutoa ya moyoni, katika tume hiyo ili yafanyiwe kazi.

"Kuna watu waliobambikiziwa kesi, wengine  walionewa waombe wafidiwe walionyangwa mali zao pia wafidiwe.

"Tunajua kuna tume imeundwa ya Jaji Othman Chande kwa ajili ya kutazama masuala ya haki ya jinai iongezewe wigo ili kutoa nafasi kwa wananchi kwenda kutoa maelezo kuhusu madhila waliyapitia," amesema.

Mbali na hilo, Zitto Kabwe amewataka wakazi wa Tanga kutokata tamaa na michakato ya kisiasa, akisema wakifanya hivyo watakuwa wametenda  makosa makubwa. Amesema Tanga imechangia sehemu kubwa katika Uhuru wa Tanganyika wanapaswa kuendeleza mapambano hayo ili kupatikana kwa Katiba Mpya.

" Tanga irejeshe heshima ile bila Katiba mpya hatuwezi kupata demokrasia, najua watu Tanga mmekuwa mstari wa mbele katika mageuzi, sasa tuendelee na hili kupata Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba mpya," amesema Zitto.

Ameongeza kuwa "Tunaomba mkubaliane na sera zetu ili kusonga kwa maendeleo ya Tanga katika sekta za viwanda,  bandari na kilimo hasa cha mkonge, naomba tusafiri pamoja katika safari hii na mtuunge mkono," amesema Zitto.

Katika maelezo yake, Zitto alisema ACT-Wazalendo ikipewa nafasi ya kupata uwakilishi mkoani wataleta mabadiliko makubwa katika sekta za uchumi hasa kufufua uchumi wa viwanda vilivyokuwapo katika miaka ya nyuma.