Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema inavyochanja mbuga mikoani, yasisitiza Katiba mpya

Muktasari:

  • Kupitia Operesheni ya Katiba Mpya na Free Tundu Lissu ngwe ya pili,  chama hicho kinaendesha mikutano katika Kanda ya Nyasa na Kanda ya Kati inayofanyika kuanzia asubuhi hadi jioni




Dar/Mikoani. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea kuchanja mbuga maeneo mbalimbali nchini kufanya mikutano ya hadhara huku kikiwataka wananchi kuendelea kukiunga mkono.

Kupitia Operesheni ya Katiba Mpya na Free Tundu Lissu ngwe ya pili, chama hicho sasa kinaendesha mikutano katika Kanda ya Nyasa na Kanda ya Kati inayofanyika kuanzia asubuhi hadi jioni na kuhudhuriwa na umati wa wananchi wanaojitokeza kusikiliza hoja mbalimbali zinazowasilishwa na viongozi wa chama hicho.

Mikutano ya Kanda ya Nyasa, inayojumuisha mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe na Rukwa, inaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche na Kaimu Katibu Mkuu, John Mnyika. Viongozi hao wamehamishia shughuli zao katika kanda hiyo wakitokea Kanda ya Kusini.

Kwa upande mwingine, mikutano ya Kanda ya Kati, inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Morogoro na Singida, inaongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema pamoja na mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, Boniface Jacob maarufu Boni Yai.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, leo akisimikwa kuwa Chifu wa Wangoni wa Mkoa wa Ruvuma leo Jumamosi Juni 20, 2026.

Baadhi ya hoja kuu zinazojadiliwa katika mikutano hiyo ni umuhimu wa Katiba mpya, ugumu wa maisha, tozo mbalimbali, uwajibikaji na uadilifu wa watumishi wa umma.

Leo, Jumatatu Juni 22, 2026, mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema dalili zinaonesha bado kuna mpasuko wa kisiasa ndani ya nchi ambao haujapatiwa ufumbuzi wa kutosha, licha ya mamlaka kuonesha nia ya kufanya maridhiano.

Amesema Chadema imeendelea kueleza malalamiko na manung’uniko yake hadharani, huku utekelezaji wa hatua zinazotarajiwa katika mchakato wa maridhiano ukionekana kusuasua.

“Chadema imekuwa ikitoa malalamiko yake mara kwa mara, lakini mamlaka hazionekani kulipa uzito wa kutosha suala hilo, utekelezaji wa baadhi ya makubaliano umekuwa ukicheleweshwa,” amesema Dk Mbunda.

Kuhusu mwitikio wa wananchi katika mikutano yao, Dk Mbunda amesema hali hiyo ni ujumbe kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwamba, licha ya changamoto mbalimbali, ikiwamo kunyimwa ruzuku, Chadema bado inaendelea kuungwa mkono na kuendesha shughuli zake za kisiasa.

Amesema hali hiyo inaweza kuwa changamoto kwa chama tawala, kwa kuwa hotuba za viongozi wa Chadema zimekuwa zikigusa masuala yanayowahusu wananchi moja kwa moja, hivyo kuongeza ugumu kwa Serikali na chama kilichopo madarakani kujibu hoja zinazotolewa.


‘Hatusafirishi watu’

Akizungumza jana Jumapili Juni 21, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Makambako mkoani Njombe, Heche amepiga kijembe kwa wapinzani wao akidai mikutano ya chama hicho imekuwa ikivutia idadi kubwa ya wananchi bila kulazimika kuwasafirisha kutoka maeneo mengine.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara leo Jumamosi Juni 20, 2026 Wilaya ya Songea.

“Wale jamaa wakija hapa hawalali. Ndiyo maana nimewaambia tangu juzi kuwa mchakamchaka huu tutawapeleka mpaka mfilisike au muendelee kuwasumbua matajiri kuomba fedha za kufanya mikutano. Kwa Chadema, mkutano kama huu tunahitaji kuutangaza tu, na nyomi ndiyo hii hapa,” amesema.

Heche amesema mikutano ya Chadema ni ya asili, jambo linalochangia wananchi kujitokeza kwa hiari yao kusikiliza hoja zinazowagusa moja kwa moja baada ya kukosa msaada wa kusemewa.

Amesema Tanzania ni nchi yenye rasilimali nyingi na uwezo mkubwa wa kuwapatia wananchi maisha bora, lakini bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali licha ya kupita miaka 65 tangu kupata uhuru.

“Tanzania ni nchi ya tatu duniani kwa kuwa na dhahabu nyingi, lakini bado tunashuhudia ukosefu wa mipango miji na mambo mengi yanafanyika kiholela. Chanzo chake ni ukosefu wa utawala bora unaozingatia masilahi ya wananchi,” amesema.

Heche amewataka viongozi katika ngazi mbalimbali kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na kutanguliza masilahi ya wananchi badala ya kujinufaisha wenyewe au kuwanufaisha waliowaweka madarakani.


Maadili, uwazi

Heche amesema viongozi wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kuepuka rushwa na matumizi mabaya ya madaraka huku wakiheshimu sheria na kusimamia haki kwa wote.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara leo Jumamosi Juni 20, 2026 Wilaya ya Songea.

Amesema uongozi wenye maadili na uwazi ni msingi muhimu kwa kujenga imani ya wananchi na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Heche amesema viongozi wanapaswa kusikiliza wananchi na kutekeleza ahadi walizotoa kwa manufaa ya jamii, badala ya kufanya uamuzi kwa masilahi yao binafsi bila kuzingatia sheria.

Heche amesema Tanzania ina kila rasilimali inayohitajika kufikia maendeleo makubwa, lakini mafanikio hayo yanategemea uwepo wa watu wenye maadili, siasa safi, matumizi sahihi ya ardhi na uongozi bora.

Amesema Katiba ya sasa imeweka misingi na haki mbalimbali muhimu kwa wananchi, lakini bado ina upungufu unaowazuia wananchi kuwawajibisha viongozi wao ipasavyo.

Amesema hali hiyo imechangia kuendelea kwa matumizi mabaya ya rasilimali za Taifa.

Pia, amedai deni la Taifa linaendelea kuongezeka na mzigo wake unabebwa na wananchi kupitia tozo na ushuru mbalimbali, jambo linalowaathiri zaidi wakulima na makundi mengine ya uzalishaji.

“Mkulima anapovuna mazao yake anakutana na tozo na ushuru wa aina mbalimbali. Mwisho wa siku mzigo huo unaangukia kwa mwananchi wa kawaida,” amesema.

Heche amesema changamoto nyingi zinazoikabili nchi zinatokana na mfumo wa uongozi usio na uwajibikaji wa kutosha, licha ya Tanzania kuwa na rasilimali nyingi kama madini, ardhi yenye rutuba na mifugo.

 “Tuna kila sababu ya kuwa Taifa lenye maendeleo makubwa, lakini bado tunashuhudia watoto wakisoma katika mazingira duni na wananchi wengi wakikabiliwa na umaskini. Haya ni matokeo ya uongozi,” amesema.

Pia, amewataka wananchi kuondoa hofu na kuungana kudai mabadiliko ya mfumo wa uongozi pamoja na upatikanaji wa Katiba mpya, akisema ukimya wa wananchi unatoa nafasi kwa baadhi ya viongozi kuendelea kutumia vibaya mamlaka na rasilimali za umma.

Amesema Chadema inaamini Katiba mpya itasaidia kujenga mfumo wenye usawa wa fursa kwa wananchi wote, hasa katika sekta ya elimu ili watoto waweze kushindana katika mazingira yanayofanana bila kujali hali zao za kiuchumi au kijamii.


Alichokisema Mnyika

Kwa upande wake, Mnyika amesema Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipaswa kusitisha shughuli zake na kuishinikiza Serikali kutenga fedha kwa ajili ya mchakato wa Katiba mpya, akieleza kuwa hilo ni hitaji la msingi kwa wananchi.

Amesema Chadema inashangazwa na kutokuwapo kwa fedha za mchakato huo katika bajeti mpya ya Serikali, jambo ambalo kwa mtazamo wa chama hicho linaonesha kutokuwapo kwa dhamira ya dhati ya kuutekeleza.

 “Kutokana na umuhimu wa Katiba mpya kwa wananchi, tulitegemea kuona bajeti ya mchakato huo ikitajwa wazi katika bajeti ya Serikali. Kutokuwapo kwake kunaonesha hakuna dhamira ya kuusukuma mbele mchakato huo. Katiba mpya ndiyo ajenda yetu kuu na hitaji la wananchi,” amesema Mnyika.

Amedai kuwa, chama hicho kinafahamu mbinu zinazotumiwa kuchelewesha mchakato huo kwa kuusogeza karibu na kipindi cha uchaguzi, hali inayoweza kutumika kama sababu ya kuahirisha utekelezaji wake na kuendelea kusubiri viongozi watakaochaguliwa mwaka 2030.