Chadema Kaskazini yalalama viongozi wake kushikiliwa, Polisi yatoa ufafanuzi
Muktasari:
- Inadaiwa kuwa viongozi hao walikamatwa Julai 4 na 5, 2026, katika maeneo tofauti kwa kile alichodai ni tuhuma za kuratibu maandamano yaliyopangwa kufanyika jana Jumanne Julai 7.
Arusha. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, kimelalamikia kukamatwa na kuendelea kushikiliwa kwa viongozi wake wanne wa mikoa ya Tanga na Manyara, kikidai walikamatwa kwa tuhuma za kuratibu maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Julai 7, 2026.
Viongozi wanaotajwa na chama kuwa wamekamatwa na Jeshi la Polisi ni pamoja na Katibu wa Chadema Handeni Vijijini, Ramia Kisalazo, anayeshikiliwa Kituo cha Polisi Handeni; Katibu wa Bawacha Mkoa wa Tanga, Nusura Kihiyo; Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Korogwe, Ezekiel Mbwilo, wanaoshikiliwa Kituo cha Polisi Korogwe; pamoja na Katibu wa Bavicha Wilaya ya Mbulu, Emanuel Hari, anayedaiwa kushikiliwa katika Kituo cha Polisi Babati mkoani Manyara.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi juu ya madai hayo leo Jumatano, Julai 8, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema kuna watu wanaoshikiliwa kwa tuhuma za makosa ya mtandao na uchochezi, lakini hakuthibitisha kama ni viongozi wa Chadema.
"Sijui kama ni viongozi wa Chadema au laa. Ninachojua ni kwamba kuna watu kadhaa tuliowakamata kwa tuhuma za makosa ya mtandao na uchochezi," amesema Mchunguzi.
Amesema upelelezi wa kesi hizo unaendelea na utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa kulingana na matokeo ya uchunguzi.
Kamanda Mchunguzi amesema pia operesheni za kuwabaini na kuwakamata watu wanaodaiwa kuhusika na makosa ya uchochezi, makosa ya mtandao na makosa mengine zinaendelea mkoani Tanga.
"Lengo ni kuhakikisha Mkoa wa Tanga unaendelea kuwa salama na tulivu ili wananchi waendelee na shughuli zao za kila siku za kujenga Taifa," amesema Mchunguzi.
Leo Jumatano, Julai 8, 2026, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Yohana Kaunya ameiambia Mwananchi kuwa viongozi hao walikamatwa Julai 4 na 5, 2026, katika maeneo tofauti kwa kile alichodai ni tuhuma za kuratibu maandamano yaliyopangwa kufanyika jana Jumanne Julai 7.
Amesema maandamano hayo hayakufanyika, hivyo chama hakioni msingi wa viongozi hao kuendelea kushikiliwa.
"Maandamano yenyewe hayakufanyika, hivyo hatuelewi walikuwa wanaratibu nini. Ndiyo maana tunalaani vikali vitendo hivi vya kuwakamata viongozi wetu," amesema Kaunya.
Hivyo, ametoa wito kwa Jeshi la Polisi kuwaachia viongozi hao bila masharti, akidai wanaendelea kushikiliwa bila kufahamishwa rasmi sababu za kukamatwa kwao.
Kaunya amesema hali hiyo inaibua maswali kuhusu uzingatiaji wa utawala wa sheria, haki za binadamu na haki za msingi zinazolindwa na Katiba.
"Endapo kuna tuhuma zozote dhidi yao, Jeshi la Polisi linapaswa kuzingatia taratibu za sheria kwa kuwafahamisha sababu za kukamatwa kwao na kuwafikisha mahakamani ndani ya muda unaotambuliwa na sheria," amesema.
Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani naye amesema hakuwa na taarifa za kuwapo kwa kiongozi yeyote wa Chadema anayeshikiliwa na jeshi hilo mkoani humo kwa tuhuma hizo.
"Kwa sasa niko nje ya ofisi, lakini taarifa za awali nilizonazo zinaonyesha Mkoa wa Manyara uko shwari na hakuna mtu yeyote tunayemshikilia kwa tuhuma hizo," amesema.