Prime
Chuki ya wageni Afrika Kusini ndiyo hulka halisi ya Waafrika?
Baadhi ya waandamanaji wanaopinga uwepo wa raia wageni nchini Afrika Kusini. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Hadhi ya Afrika Kusini imeporomoka. Mamlaka za utalii zimeshatoa taarifa ya uwepo wa wimbi la ukatishaji ziara za kitalii nchini humo, kutoka kwa wageni wa mataifa mengine ya Afrika. Ukatishaji huo wa ziara, unahusu Wanigeria na raia wa nchi nyingine ambao kwa kawaida hufanya matumizi makubwa ya fedha wakiwa Afrika Kusini.
Afrika Kusini imejikuta ndani ya kitabu kibaya cha mataifa mengine ya Afrika. Mgogoro wa kidiplomasia unachipua, nchi hiyo inapoteza uwezo wake wa ushawishi (soft power), duniani.
Vicheko vya mataifa mengine ya Afrika baada ya Timu ya Taifa ya Afrika Kusini (Bafana Bafana), kuchapwa na wenyeji, Mexico, 2 – 0, katika mechi ya ufunguzi, Kombe la Dunia 2026. Wasanii wa Afrika Kusini kufutiwa ziara zao kwenye nchi mbalimbali Afrika. Ni mavuno ya chuki ambayo raia weusi wa Afrika Kusini, wameipanda dhidi ya Waafrika wenzao.
Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini, Mmamoloko Kubayi, aliamua kutoka na kuuleza umma kuwa wasanii wa Afrika Kusini, wanapata wakati mgumu, kwa sababu hawatakiwi kufanya ziara za kikazi kwenye mataifa mengine ya Afrika, hivyo kuwakosesha vipato.
“Wasanii wengi wa Afrika Kusini hutumbuiza ndani ya bara la Afrika, na wengi wao wamejikuta mialiko yao ya kazi imefutwa. Msanii mmoja mwanamke alinifikia na kunieleza kuwa mialiko yake yote ya kutumbuiza Afrika imefutwa. Haya ni mapato ambayo raia wa Afrika Kusini amepoteza,” alisema Waziri Kubayi.
Hadhi ya Afrika Kusini imeporomoka. Mamlaka za utalii zimeshatoa taarifa ya uwepo wa wimbi la ukatishaji ziara za kitalii nchini humo, kutoka kwa wageni wa mataifa mengine ya Afrika. Ukatishaji huo wa ziara, unahusu Wanigeria na raia wa nchi nyingine ambao kwa kawaida hufanya matumizi makubwa ya fedha wakiwa Afrika Kusini.
Ghana ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika, kuratibu usafiri wa kuwaondosha raia wao na kuwarejesha nyumbani. Haitoshi, Serikali ya Ghana iliweka wazi nia yao ya kuifungulia mashtaka Afrika Kusini, ili ilipe fidia kwa raia wa Ghana waliorejeshwa nyumbani, vilevile kulipia ndege ambayo ilitumika kusafirisha Waghana.
Nigeria ilichukua hatua ya kuwachukua raia wao kutoka nchini Afrika Kusini. Haitoshi, ilimwita Balozi wa Afrika Kusini nchini Nigeria, Prof Bobby Moroe, jijini Lagos kwa mazunguzo. Ghana pia waliendesha kikao na Balozi wa Afrika Kusini nchini humo, Grace Mason, jijini Accra, na kujadili tatizo la chuki za wenyeji dhidi ya wageni kutoka Afrika, nchini Afrika Kusini.
Msumbiji, baada ya raia wake watano kuuawa Afrika Kusini, kutokana na kushambuliwa na wenyeji wenye chuki, serikali ya nchi hiyo ilituma ndege na kuwasafirisha raia wao zaidi ya 700. Msumbiji walitishia kufunga mipaka kuzuia magari ya Afrika Kusini kuingia kwenye nchi yao.
Nchi mbalimbali za Afrika, zikiwamo Malawi, Zimbabwe na Kenya, zimeshatoa matamko ya kulaani vurugu za Waafrika Kusini, kuwashambulia raia wao. Nchi nyingi za Afrika pia zimeshatoa tahadhari za kiusalama kwa raia wanaoishi au waliopo matembezini Afrika Kusini.
Baadhi ya waandamanaji wanaopinga uwepo wa raia wageni nchini Afrika Kusini. Picha na Maktaba
Afrika na Waafrika
Waafrika wana mengi ya kukumbuka kihistoria yenye kupasa kuwaweka pamoja. Namna ambavyo walibaguliwa kisha kufanywa watumwa kwa mabwana wa Kizungu na Kiarabu.
Manamba waliotumikishwa kwenye mashamba ya mkonge (Silabu), watumwa waliopitishwa Kilwa kwenda Uarabuni au lango kuu la kwenda utumwani (Door of No Return), pwani ya Bahari ya Atlantic, Afrika Magharibi. Kwa uchache ni alama ya kutambua nafasi ya Mwafrika kihistoria.
Ni historia hiyo ambayo iliwafanya kina Mwalimu Julius Nyerere (Tanzania), Kwame Nkrumah (Ghana), Modibo Keita (Mali), Sekou Toure (Guinea), Haile Selasse (Ethiopia), William Tubman (Liberia), Nnamdi Azikiwe (Nigeria) na wengine, pamoja na kuzipatia uhuru nchi zao, walipambana kuikomboa Afrika yote, maana wamepitia chungu kimoja cha moto.
Historia ya kumtambua mtu mweusi kuwa si binadamu bali bidhaa. Hukumu ya kesi ya Mwafrika Dred Scott ya mwaka 1857, Marekani, ikupe mantiki. Scott na familia yake waliishi majimbo ya Illinois na Wisconsin ambako biashara ya utumwa haikuwapo. Hata hivyo, alikamatwa na kufikishwa Mahakama Kuu ambayo iliamua kuwa Scott ni mtumwa na kwamba mtumwa siyo binadamu bali ni mali (bidhaa).
James Buchanan, Rais wa 15 wa Marekani, aliunga mkono hukumu hiyo na kueleza kuwa watumwa hawatakiwi kupewa uraia kwa sababu mtumwa ni bidhaa. Akasema bidhaa haiwezi kupewa uraia.
Historia ya manyanyaso dhidi ya Mwafrika ndiyo iliwaunganisha viongozi wa Afrika kuipigania Afrika Kusini huru dhidi ya sera ya ubaguzi wa rangi iliyokuwa inatekelezwa na Serikali ya kikaburu.
Ajabu, Afrika Kusini ilipopata uhuru wa kidemokrasia Mei 10, 1994, Nelson Mandela akawa Rais wa kwanza. Desemba 1994, makundi ya vijana wa Afrika Kusini, walivamia makazi ya Waafrika wageni kwenye mji wa Alexandra, Johannesburg, kuwapiga, kuharibu nyumba zao kwa hoja kwamba waliishi kwenye nchi yao bila vibali.
Septemba 1998, Wasenegali wawili na raia wa Msumbiji, walisukumwa nje ya treni iliyokuwa ikitembea jijini Johannesburg na kupoteza maisha. Hivyo ndivyo chuki ya ubaguzi wa utaifa (xenophobia) ilivyoanza Afrika Kusini na kukomaa. Hadi sasa, mamia ya Waafrika wageni Afrika Kusini wameshauawa na wenyeji.
Suala la chuki dhidi ya wageni, tena weusi wa Afrika Kusini, dhidi ya weusi wa nchi nyingine za Afrika, limebebwa kisiasa. Inakaribia miaka 32 tangu tukio la kwanza, Desemba 1994, hali haijadhibitiwa. Chuki imepamba moto. Serikali ya Afrika Kusini inafanya siasa, na imezidiwa.
Baadhi ya waandamanaji wanaopinga uwepo wa raia wageni nchini Afrika Kusini wakizuiwa na polisi. Picha na Maktaba
Tuipate tafsiri sahihi
Vurugu za xenophobia Afrika Kusini, na matukio mengi ya kibaguzi miongoni mwa jamii za Kiafrika, zinaonesha kuwa Waafrika ni wabaguzi sana. Wamekosa fursa ya kubagua watu wa rangi nyingine, hivyo wanabaguana wao kwa wao. Waafrika wa nchi moja, hawataki Mwafrika wa nchi nyingine, afanye makazi kwenye nchi yao.
Ni hulka hiyo ya ubaguzi ndiyo ambayo ilisababisha mwanamuziki na mwanasiasa maarufu nchini Kenya, Charles Njagua Kanyi 'Jaguar', kuzungumza kwenye Bunge la Kenya, kutaka Watanzania, Waganda na Wachina, waondoke kwenye nchi hiyo, vinginevyo watapigwa na kupelekwa Uwanja wa Ndege kwa nguvu.
Serikali ya Kenya ilimchukulia Jaguar hatua za kisheria kwa kauli yake ya uchochezi na inayopandikiza chuki kwa Wakenya dhidi ya Watanzania, Waganda na Wachina. Hata hivyo, upande wa pili lazima iwekwe wazi kuwa Waafrika wanatamani na wanapigania mno fursa ya kubaguana.
Mauaji ya kimbari Rwanda, watu zaidi 1.2 milioni waliuawa kwa sababu ya ubaguzi miongoni mwa Waafrika. Jamii za Wahutu na Watutsi haziivi kabisa. Burundi imekuwa na visa vya miaka nenda rudi. Chanzo ni jamii hizohizo za Wahutu na Watutsi.
Waafrika watabaguana kwa chuki za utaifa, wakiwa ni watu wa Taifa moja, watachukiana kwa ukabila, na wanaweza kuwa kabila moja, wakashindwa kuelewana kwa sababu za ukoo. Wahutu na Watutsi ni kabila moja, wanazungumza lugha moja, ila hawaoni kama ni wamoja kwa sababu za kimaumbile.
Husikii mauaji ya jamii za watu wenye ualbino Ulaya na mataifa mengine, ila Afrika albino hawana usalama. Waafrika wanawawinda na kuwaua wenzao kwa sababu ni walemavu wa ngozi.
Mwaka 1821-1822 (Karne ya 19), Wamarekani Weusi waliokuwa watumwa Marekani, waliachiwa huru na kuelekezwa Pwani ya Afrika Magharibi ili kuunda jamii ya koloni la Marekani (American Colonization Society 'ACS'). Watumwa hao walipofika Afrika, kituo chao kikuu kikawa Liberia.
Liberia tayari ilikuwa na wakazi wake walioishi katika jamii za makabila ambayo yalihamia kuanzia Karne ya 13-16 kutokea Sudan (Songhai Empire), Mali na maeneo mengine ya Afrika. Jamii ya waliozungumza Kimende pamoja na makabila ya Dei, Kru, Bassa, Gola, Grebi, Gio na Kissi ni watu wa mwanzoni kuishi Liberia.
Waliberia waliotokea Marekani utumwani walipofika Liberia, nao wakajiona wana hadhi kubwa, wakawatawala wenyeji, wakawanyang'anya ardhi, wakawageuza watumwa kwenye mashamba na shughuli nyingine za uzalishaji mali. Wao walizungumza Kiingereza, hivyo hawakutaka kujifananisha na wenyeji waliowasiliana kwa lugha za makabila yao.
Hayo huonesha kuwa bora Wazungu na Waarabu waliwabagua Waafrika. Kwa Afrika, Waafrika hubaguana wao kwa wao. Kiongozi wa nchi moja anaweza kufurahia vita kwenye taifa lingine la Afrika ili apate fursa ya kupora mali.
Ipo video inasambaa, mbunge wa Kenya akimtetea Jaguar bungeni kuwa masilahi ya Wakenya lazima yalindwe kwa sababu Wakenya wananyimwa ajira Tanzania, raia wa nchi hiyo wanapata wakati mgumu kufanya biashara Tanzania, anakumbusha vifaranga vya kuku Kenya vilivyochomwa moto Tanzania na ng'ombe wa Kenya waliopigwa mnada Tanzania.
Lazima kukubali kuwa chuki za utaifa zinaenea sana Afrika. Viongozi watakaribisha wageni, lakini raia wananuna. Rais Uhuru Kenyatta alisema, na Rais William Ruto, alisisitiza, kwamba raia wa Afrika Mashariki wakiwa na vitambulisho vya taifa, wapo huru kuishi Kenya, kufanya shughuli za kiuchumi na hata kuoana na Wakenya, ila wabunge hawataki hilo. Waafrika wana hulka ya kubaguana.
Kwa nini chuki?
Uchambuzi wa jumla unayo majibu kuwa tatizo la chuki Afrika Kusini dhidi ya wageni kutoka mataifa mengine ya Afrika ni wivu na uvivu. Wageni wanaoingia Afrika Kusini, wanafanya kazi kwa bidii, hivyo kuwaacha mbali wenyeji ambao ni wavivu. Wageni wamekuwa wabunifu wa kuzigeuza fursa zilizopo kuwa fedha, wakati wenyeji hubaki kulalamika. Matokeo yake, kiwango cha juu cha wivu hutengeneza chuki kubwa kutoka kwa wenyeji kwenda kwa wageni, kwamba wageni wanawazuia wenyeji kupata ajira za uhakika kwenye nchi yao.
Wanasiasa Afrika Kusini wamegawanyika. Wapo wanaunga mkono xenophobia, japo kimyakimya, wengine wanapinga. Tatizo la ubaguzi limeshageuzwa mtaji kisiasa kwenye uchaguzi. Ni vigumu kupata matokeo yanayotakiwa. Muhimu kuelewa na kuzingatia ni kuwa Waafrika, watu weusi, wana asili ya kubaguana. Hata zama za ukoloni, weusi waliwauza weusi wenzao.