Doyo aibukia NLD, ateuliwa kuwa Katibu Mkuu
Muktasari:
- Doyo ametimkia NLD na kupitishwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, zikiwa zimepita siku 69 tangu aliposhindwa kwenye nafasi ya uenyekiti wa ADC Taifa katika uchaguzi uliofanyika Juni 29, 2024.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Doyo Hassan Doyo ameibukia kwenye chama cha National League for Democracy (NLD), akieleza sababu za kuhama chama hicho akiwa mmoja wa waasisi wake.
Doyo ambaye Juni 29, 2024 alishindwa kwa tofauti ya kura 51 na Shaban Itutu aliyepata kura 121 katika kinyang'anyiro cha uenyekiti wa ADC, amekiri kuhamia NLD na Jumamosi iliyopita, Septemba 7, 2024, ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Akithibitisha hilo, Mwenyekiti wa NLD Taifa, Mfaume Hamis Hassan amesema yeye ndiye aliyempendekeza Doyo kujiunga na chama hicho na Septemba 7, 2024 wakati wa uchaguzi wa Taifa wa chama, Halmashauri Kuu ilimuidhinisha kuwa Katibu Mkuu wao.
“Tulikuwa na uchaguzi wa chama Taifa ambao Mizizi ameshinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara na Mwanakombo Hamad Hassan ameshinda upande wa Zanzibar, kama mwenyekiti baada ya kushinda, nilimteua Doyo awe Katibu Mkuu wetu na akaidhinishwa na Halmashauri Kuu,” amesema.
Mfaume amesema sababu za kumchukua Doyo na kumpitisha kuwa Katibu Mkuu ni kutokana na utendaji wake, uhodari na upambanaji wake tangu akiwa ADC.
Doyo amepitishwa kwenye nafasi hiyo, ikiwa zimepita siku 69, tangu aliposhindwa nafasi ya uenyekiti wa ADC na kukata rufaa akipinga uchaguzi huo aliodai umekiuka katiba na kanuni za chama hicho na kesi yake bado inaendelea.
Hata hivyo, baada ya kuhama, amesema hana muda na kesi hiyo tena, anachokifanya sasa ni kuendelea kuipambania NLD.
Licha ya baadhi ya wadau wa siasa kudai shida ya Doyo ilikuwa ni madaraka na alipoyakosa ADC akaamua kutimkia NLD, mwenyewe amesema alikosa fursa ya kufanya siasa baada ya uchaguzi wa ADC.
“Niliandikiwa barua sitakiwi kufanya siasa yoyote hadi nipangiwe na chama, nikaona kwa hilo nitakuwa nawadhulumu Watanzania ambao wamezoea kuniona kwenye ulingo wa kisiasa, nikachukua uamuzi wa kutimkia NLD ili kuendeleza harakati za siasa,” amesema.
Amesema sasa wanajipanga kwa uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 na lengo ni kuhakikisha wanashirikiana kukikuza chama hicho cha upinzani nchini.