Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

FYATU MFYATUA: Onyo Mafyatu wanaohoji ulaji wangu, uhalali wangu



Kuna mafyatu katika kaya yangu ya Fyatuland waliofyatuka kwelikweli hadi wanataka kunifyatua kabla sijawafyatua. Siku hizi, mafyatu wangu wana kamchezo ka kunifyatua bila aibu wala sababu. Si juzi, kajitokeza mmoja aliyetaka kunifyatua na kunivua nguo tena haradhani akiongelea mambo ya kale.

Hakujua kuwa ya kale yananuka hata kama yaliwahi kunuka baada ya mafyatu kukinukisha. Kwa vile nilikuwa na inshu nyingi kwenda zangu ughaibuni kutanua na kujinadi, nilimlia pini. Si kwamba nilimgwaya.

Never. Muache. Ngoja nipoe. Lazima nnitamfyatua ashike adabu na adabu imshike akome na kukomaa. Senzi kabisa. Akizidisha kiherehere na kiranga chake, namfyatua kwa kumtumia wasiojulikana wamshughulikie kwa vile anajulikana. Hapa lazima nimpopoe kabla ya kunipopoa. Akishupaza shingo, namslowslow polepole na anapotea milele. Anacheza nami! Inaonekana hanijui vizuri. Anadhani upole wangu ni woga asijue mie ni katili hakuna mfano.

Wakati akizoza, nilimuuliza tena kwa upole ‘mnapata wapi jeuri kuhoji wasiohojiwa au kutaka kuwafyatua wasiofyatuliwa ila kuwafyatua nyinyi mafyatu ambao kumbe mkifyatua ni hatari eeh? Nadhani hawa wanatumwa na mabeberu waje kunibeberu wasijue mie siyo mbuzi jike bali beberu lenyewe tena la kunuka na kukinukisha. Akawaulize wale wahuni waliojifyatua wakataka kunifyatua nikawafyatua wakasahaulika. Hawa mahuluku taabu wana taabu, we acha tu.

Ngoja niwape inshu nzima. Tulikuwa na uchaguzi wa ndani siku zilizopita ambapo nilishinda baada ya wanoko fulani kutaka kuniengua nikaishia kuwaengua na kujisimika na kushinda kwa kishindo na vishindo na kuwaacha solemba. Baada ya kuona walitaka eti kugombea nami, nikaitisha kikao cha chata changu cha Chata cha Mafyatu (CcM) wakanipitsha bila kutaka pale walipotaka nitoke nje eti wanichinje nikagoma nao wakagwaya na kuniptisha bila kupingwa.

Tokana na kuwafyatua mafyatu waliotaka kunifyatua, si kuna mafyatu waliojitokeza kunipaka matope. Si walihoji kuwa nilishiriki uchaguzi sijui uchakachuaji sijui uchafuzi, wala sijui. Kwanza, walitaka eti yapelekwe majina kadhaa kwenye kamati kuu inikamate! Kuona hivyo, nilichenji gia angani na kufyatua taratibu zote za chata letu. Badala ya kufuata katiba, niliamua kuifyatua na kuwafyaulia mbali hadi nikashinda ulaji kihalali na kwa kishindo japo mafyatu adui wanadia kuwa nilishinda kwa fujo, ukatili, na mambo mengine ambayo sitaki kuyarudia.

Unawezaje kushinda kwa asilimia 1000 kama kweli kuna kamchezo ulifanya? Mie napendwa na kukubalika bwana. Hata kama ndege na wadudu wangeruhusiwa kupiga kura, wangenichagua mimi chaguo na kipenzi cha Mungu Dk. Dk. Dk. Daktari, Profesa, Shehe, Askofu, Field Marshall, Jenerali, Al haj, Mtakatifu Fyatu Mfyatuzi Esq n.k.n.k.

Ilibidi nijiapishe mwenyewe tena kwenye chumba chetu cha kulala na Bi Mkubwa. Waweza kuamini? Wengi walizoza na kusema eti haya yalikuwa maajabu na matokeo ya uchakachuaji. Kwani, niliwazuia wasichakachue? Walitaka niapishwe kwenye uwanja wa mpira wanipopoea kwa mimawe nami niwaslowslow kama siyo kuwapoteza. Mie ni mtu wa Mungu na mcha Mungu hakuna duniani isipokuwa mimi.

Kawaulize wale mashehena wanaonijua. Si waliwaasa kuwa baada ya kuumbwa mwana wa Maria na Ntume, hakuna kiumbe bora mwingine aliyeumbwa isipokuwa Fyatu Mfyatuzi mjukuu wa Mfyatuko? Walidhani hawa wanaweza kuongopa?

Baada ya kuwazidi kete mafyatu uchwara nilisikia wakilalamika. Mara chata kililazimisha mgombea wake wa urahis hata kwa kuvunja na kuvuruga kanuni zake chenyewe. Eti chata letu lilipoteza njuluku na muda kutupigia makelele kwa kisingizio cha kampeni za uongo na vitisho. Wamezoza na kuzua mengi. Mara eti chata letu linadai linadumisha amani kwa kuivunja tena kwa miaka mingi tena kwa kuongoza kwa fujo.

Ebo! Bila fujo waweza kuongoza au kuongozwa? Wanadai ninawaminisha kuwa nitatenda haki wakati ni bingwa wa kudhulumu, kuteka, kupoteza, na kuua. Wanadai najiridhisha kutaka kuwaridhisha kuwa nilivyofanya ni sawa. Nalaumiwa kwa kusifiwa na kujisifu hata ninapostahili kulaumiwa na kulaaniwa! Ebo,!

Hamjaambwa raha jipe mwenyewe? Nisipojisifu, nani atanisifu? Nilizuliwa eti nawanyanyasa wapingaji wangu. Ebo! Mlitaka niwaache waninyanyase hata kupoka ulaji wangu wa dezo! Nani yuko tayari kufua nguzo zake za ndani hadharani tena mbele ya maadui zake huyo? Japo mafyatu wanasema niko uchi nikijidanganya nimevaa, nasema sibadiliki.

Hakuna umbea na urongo vimeniudhi kama kudai niligombea na kivuli changu. Walitaka nigombee na nani wakati wao ndiyo vivuli vyangu? Si wapo waliosusa sie tukajitwalia na kujilia wakabaki kulalama na kulaani wakidhani kelele za chura zinamzuia nguruwe kunywa na kunya kwenye kisima. Lo! Imkula kwao.

Kwa vile naipenda sana Fyatuland kiasi cha kuwa tayari kuua, sorry, kuuawa kwa ajili yake, sitasikia kelele za vyura. Naendela kukandamiza na kutanua na kutesa wakati mafyatu wanajifyatua na kulalamika wakati mie nazidi kuziba masikio.

Kwa hiyo, natoa onyo la mwisho. Komeni kuniandama. Nendeni mkaandamane mkione cha moto. Kula na kutesa ni kwa zamu. Ngojeeni zamu yenu. Tumeelewana? Lo! kumbe nililewa chakari hadi nikalala mtaroni!