FYATU MFYATUZI: Tunataabishwa, tuwataabishe wanaotutaabisha

“Hakuna kitu kibaya sana humu kayani kama shida. Kila siku shida, shida mpaka siku ya mwisho.”
Kwa waliozaliwa juzi, nawaletea falsafa kongwe na madini ya profesa al Marhum Mbaraka Mwinshehe, gwiji na nguli aliyetoka duniani mapema akihitajika. Natamani lifufuke nilipe ‘hi five.’
Ningekuwa na mshiko, ningemshikisha bintiye muhitaji. Zama hizo muziki ulikuwa muziki na shule si kupayuka mitusi kama leo. Hatukutaabishana kama sasa, japo taabu zilikuwapo. Mbaraka aliona mbali. Fikiria. Unaamka asubuhi, taabu. Hujui utaanzia au kuishia wapi.
Kila unachowaza taabu. Maisha yanapogeuka jiwe unategemea nini? Siku hizi hata kukopa taabu. Ukienda hovyo kwa wezi wanaotoza riba za juu wataishia kukomba kila ulicho nacho wakuongezee taabu. Ni taabu tupu.
Kukicha baada ya kulala, ukiugulia kama hukuitwa mume suruali, unajiondokea na hasira, njaa na taabu zako hasa unashuhudia wanene na chawa wakitanua bila taabu. Unamuonea gere hata kuku anayelisha vifaranga vyake vikashiba kufurahi na kunawiri wakati vitegemezi vyako vikikondeana kwa taabu.
Wakati ukilalamika taabu, wanene wanazidi kunena kama nune kwa kodi zako bila taabu. Wakati ukitaabika na kwa kutaabishwa, wenzako wanatanua na kutanuka kwa mashangingi, mashumbwengu, mashankupe manono kiasi cha kupata hata damu ya kulisha chawa bila taabu.
Ukirejea home taabu zishakulegeza zaidi. Unashindwa hata cha usiku hata kama cha mgawo. Wanaokata umeme hawajui wataongeza idadi ya mafyatu kwa kuzalisha vitegemezi visivyo na mpangilio wakati nao hawana mipango ya kuviendeleza.
Wanategemea mafyatu wasifyatuke kufyatua na kufyatuana gizani? Sasa bila umeme watafanya nini zaidi ya kufyatua na kufyatuana?
Umeme taabu. Maji taabu. Kodi ya mwenye mbavu za dog taabu. Ngwalangwala, nauli taabu. Mwendo kasi usiokasi ukakasi. Misururu barabarani tabu. Maadili taabu. Madili taabu. Kila kitu ni taabu. Ukiachia hizo taabu, karo za vitegemezi taabu, hata nonohimo kwa Bi Mkubwa taabu.
Kila kitu taabu, mgawo wa maji na umeme taabu hata tozo taabu. Basi kaya iitwe taabu tujue. Hakuna kitu kinataabisha kama kushudia wanaotutaabisha wakitanua. Wanaboronga hapa. Wanahamishiwa pale.
Ni taabu tupu. Wakati wakitutaabisha, wao wanateuana na kupeana ulaji kuanzia vitegemezi hata vishikaji vyake. Hamkumuona Moody Mchengeta aliyeula kwa kuwa mshikaji wa kitegemezi cha maza. Unacheza na love of the mother-in-love nini?
Kuondokana na tabu hizi ni mawili au matatu. Ima ujitoe akili na kufanya vitu visivyoingia akilini kama usanii uchwara hata uchwara au utafute kitegemezi cha mdingi mmoja ukitie ndani, ili upewe ulaji wa kiukoo ulioanza kuzoeleka.
Ukishindwa haya, wewe imba mapambio ya kusifia kila kitu hata kama ni kamba au hakiingii akilini.
Kama unadhani nazuga kwa bangi na ufyatu umeula wa chuya. Kawaulize akina Jeri Silaha na yule fuataMkumbo Kitilya wakupashe hili dili rahisi. Juzi, nilimsikia chawa mmoja akimpaka mafuta bibie kwa mgongo wa chupa kuwa ana kila sifa za kuendesha kaya kwa sababu mafyatu walimchagua. Nani alimchagua kama si mwendazake kurejesha namba?
Hapakuwa na uchaguzi wala uchakachuaji wala uchafuzi, bali kifo tu. Hili ndilo huitwa zali la mentali. Hata hivyo, chawa wakishiba sana huwa taabu kuelewa hata mambo madogo kama haya.
Hata shibe inaweza kuwa taabu na ikawa na tabu pia. Kwanza, chawa hawana aibu. Pili, hawana kumbukumbu. Tatu, hawana hata akili. Ndivyo walivyoumbwa. Kwao kujua ni tabu kama ilivyo kwa wale wanaowafuga. Chawa ni wachafu naturally. Ili uwe na chawa shurti uwe mchafu kwelikweli. Chawa hawaishi sehemu safi hata kidogo.
Siku hizi kila kitu taabu. Baada ya taabu ya machawa, soon tutaona mainzi, maana palipo na chawa kuna uchafu na uchafu huvutia mainzi. Nenda mitaani ukaone uchafu. Nenda kwenye siri kali ukaone uchafu kila namna. Kila kitu taabu.
Mgawo taabu. Taarifa ya Mkaguzi wa Njulu za siri kali ndo usiseme. Ni taabu tupu. Wizi kila mahali. Kaya inaliwa mbele na nyuma kushoto na kulia. Ni taabu tupu.
Hakuna anayejali. Walaji wanakula bila taabu. Na waliwa wameridhika na taabu. Taabu zimekuwa mtindo wa maisha kwa mafyatu wanaotaabika hata bila kulalamika. Basi hii kaya iitwe taabu tujue au siyo?
Kumbe kumekucha!