Hatima ya Sugu, Msigwa Kanda ya Nyasa ni suala la muda tu

Wanachama na makada wa Chadema wakiwa katika viunga vya Kanisa Katoliki Parokia ya Bikra Maria wa Neema Mji wa Makambako mkoani Njombe wakisubiri utaratibu wa kuingia ukumbini tayari kwa uchaguzi wa ndani Kanda ya Nyasa. Picha na Saddam Sadick

Muktasari:

  • Uchaguzi huo unafanyika leo Mei 29,2024 katika Mji wa Makambako mkoani Njombe, ambapo macho na masikio ya wengi ni kusikia na kuona nani ataibuka mshindi nafasi ya Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa kati ya Msigwa na Sugu.

Njombe. Wakati uchaguzi wa ndani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa ukifanyika leo Mei 29,2024 wajumbe na makada wa chama hicho wamejitokeza kwa wingi kushiriki hatua hiyo.

Uchaguzi huo ni kuwapata viongozi wa mabaraza ikiwa ni Baraza la Wanawake (Bawacha), Wazee (Bazecha) na Vijana (Bavicha) na Mwenyekiti,  Makamu na Mweka Hazina.

Wanaogombea nafasi ya Mwenyekiti ni Mchungaji Peter Msigwa anayetetea nafasi yake na Joseph Mbilinyi 'Sugu' ambaye anawania nafasi hiyo kwa mara ya kwanza na wameonekana kuwa na upinzani mkali katika kiti hicho.

Hadi sasa wajumbe wanaendelea kuingia huku uchaguzi wa mabaraza ambao ndio utatanguliwa kufanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikra Maria wa Neema katika mji wa Makambako mkoani hapa.

Mwananchi Digital iliyoweka kambi katika viunga vya Kanisa hilo, imeshuhudia ulinzi ukiimarishwa huku wajumbe wakiingia kwa utaratibu na kuwekwa eneo maalumu karibu na ukumbi wa kupigia kura.

Akizungumzia maandalizi, Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Gwamaka Mbugi amesema wanatarajia jumla ya wajumbe 109 kutoka majimbo 31 kushiriki uchaguzi huo.

Amesema hadi sasa wagombea wote wamefika na hakuna taarifa za yeyote kukacha au kujitoa kwenye, hivyo kinachoendelea kwa sasa ni uhakiki wa mabaraza matatu kisha kuanza uchaguzi wao na baadaye kuingia kwenye Mkutano Mkuu wa kuwapata Mwenyekiti,  Makamu na Mweka Hazina.

"Kanda yetu ina mikoa mitano na minne wote imefika isipokuwa Njombe ambao uchaguzi wao ulivurugika, kwa ujumla tunatarajia uchaguzi kufanyika vyema" amesema Mbugi.

Kwa upande wao baadhi ya wajumbe wamesema pamoja na mchuano utakaokuwapo, lakini wanatarajia uchaguzi huru, haki na amani kwani hawagombani na vyama vingine ikiwamo Chama cha Mapinduzi (CCM).

Asifiwe Mwambewele amesema wanatarajia kupata mabadiliko na kwamba Kanda hiyo yenye majimbo 31 wanahitaji kuona Chadema wakishinda yote kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa.

"Tunataka atakayeshinda ajitahidi kuyafikia majimbo yote ili kupambania ushindi katika uchaguzi ujao kuanzia Serikali za Mitaa" amesema Mwambewele wa kutoka mkoani Songwe.

Naye Mulele Mulele kutoka wilayani Karambo mkoani Rukwa amesema uchaguzi utakuwa na upinzani mkali na kura ndizo zitaamua huku akieleza kuwa wanachohitaji ni kumpata kiongozi.

"Hapa hatushindani na chama pinzani, tunatarajia uchaguzi mgumu ila wa haki na amani, hitaji letu ni Ofisi ya Kanda na matarajio yetu atakayeshinda atekeleze ahadi alizoahidi wakati wa kampeni" amesema Mulele.