Hawa ndiyo Mawaziri Wakuu wa Uingereza waliojiuzulu
Muktasari:
- Mawaziri wakuu wa Uingereza wamekuwa wakijiuzulu nyadhifa hizo kwa sababu mbalimbali na sasa ni Keir Starmer ambaye ametangaza kuachia ngazi.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer ametangaza kujiuzulu wadhifa wake na uongozi wa Chama cha Labour, lakini unafahamu viongozi waliowahi kujiuzulu nchini Uingereza katika wadhifa huo?
Starmer aliyeingia madarakani Julai 2024, ametangaza kuachia nafasi hiyo leo Jumatatu, Juni 22, 2026 akisema ataendelea kuhudumu kama Waziri Mkuu wa mpito hadi pale kiongozi mpya wa chama hicho atakapochaguliwa katika wiki chache zijazo.
Uamuzi huo umetona na shinikizo kutoka kwa wanachama wa chama na wabunge wanaotaka mabadiliko ya uongozi ili kufufua matumaini katika utendaji wa serikali ambao umeonekana kuzorota.
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson. Picha na Mtandao
Uamuzi huu siyo wa kwanza kufanywa na viongozi katika nafasi ya Waziri Mkuu wa Uingereza. Mwaka 2022, aliyekuwa Waziri Mkuu Boris Johnson alijiuzulu wadhifa wake mwezi Julai baada ya msururu wa kashfa za kisiasa, ikiwemo iliyojulikana kama "Partygate" ya kukiuka sheria za kujitenga wakati wa janga la Uviko-19.
Shinikizo kubwa la mwisho liliibuka baada ya Johnson kumteua Chris Pincher kuwa Naibu Msimamizi Mkuu wa Chama cha Conservative, licha ya kufahamu kuwa alikuwa na tuhuma za utovu wa maadili ya kijinsia.
Baada ya Boris kuondoka madarakani, Chama cha Conservative kilimchagua Liz Truss kuwa kiongozi wa chama hicho, kisha akateuliwa kuwa Waziri Mkuu na Mfalme Charles III Septemba 2022.
Kabla ya Johnson kuondoka madarakani, aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo alikuwa Theresa May.
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May. Picha na Mtandao
Theresa aliyepokea kijiti cha uwaziri mkuu mwaka 2016 alijiuzulu mwaka 2019 kufuatia kukosa uungwaji mkono wa Bunge la Uingereza kuhusu makubaliano yake ya Brexit, yaliyolenga kuweka masharti ya kuondoka kwa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya.
Juni 2016, Uingereza ilipiga kura ya maoni (referendum) kuwauliza wananchi kama wanataka kubaki au kuondoka katika Umoja wa Ulaya.
Matokeo yalionyesha asilimia 51.9 walipiga kura ya kuondoka (Leave) na asilimia 48.1 walitaka kubaki (Remain). Baada ya matokeo hayo, Waziri Mkuu wa wakati huo, David Cameron, ambaye alikuwa upande wa kubaki ndani ya EU, alijiuzulu mwaka 2016.
Theresa May alipoingia madarakani, jukumu lake kubwa lilikuwa kusimamia mazungumzo ya kuondoka kwa Uingereza kutoka EU.
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron. Picha na Mtandao
Baada ya kushindwa kupata uungwaji mkono wa Bunge na kukabiliwa na upinzani ndani ya chama chake cha Conservative, Theresa May alitangaza kujiuzulu Mei 2019 na akaondoka rasmi madarakani Julai 2019.
Mfululizo wa viongozi wa Uingereza kujiuzulu ulimkumba pia aliyekuwa Waziri Mkuu Tony Blair.
Blair alijiuzulu uwaziri mkuu wa Uingereza mwaka 2007 baada ya kuongoza taifa hilo tangu 1997 na kukabidhi madaraka kwa mrithi wake, Gordon Brown.
Kuondoka kwake kulikuja baada ya shinikizo la kisiasa, hasa kuhusu vita vya Iraq na kupungua kwa uungwaji mkono ndani ya Chama cha Labour.
Historia pia inaonyesha kuwa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Margaret Thatcher, alijiuzulu Novemba 1990 baada ya kupoteza uungwaji mkono ndani ya Chama cha Conservative.
Pia, kulikuwa na upinzani mkubwa dhidi ya sera ya kodi ya jamii (Poll Tax) na changamoto ya uongozi kutoka ndani ya chama.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer aliyetangaza kujiuzulu wadhifa wake na uongozi wa Chama cha Labour. Picha na Mtandao
Waziri Mkuu akijiuzulu nini hufuata?
Kinachofuatia baada ya kiongozi wa Conservative kujiuzulu ni kuanzishwa kwa uchaguzi wa kiongozi mpya wa chama, ambapo chini ya sheria za sasa, wagombea wanahitaji kuungwa mkono na wabunge wanane wa chama hicho ili kuwania nafasi hiyo.
Baada ya wagombea wote kuidhinishwa, na iwapo watakuwa zaidi ya wawili, wabunge wa chama hicho watashiriki katika uchaguzi hadi wagombea wawili watakaposalia.
Katika raundi ya kwanza, mgombea ni sharti apate asilimia 5 ya kura ili kusalia katika kinyang'anyiro.
Katika raundi ya pili ni sharti apate asilimia 10 ya kura. Katika raundi zinazofuata, mgombea mwenye kura chache zaidi ataondolewa. Wakati wagombea wawili watakaposalia, wanachama wote wa Chama cha Conservative nchini, na si wabunge pekee, watampigia kura mshindi.
Muda wa uchaguzi huo huamuliwa na Kamati ya Wabunge wa Nyuma, na kamati hiyo inaweza kupiga kura kubadilisha sheria kabla ya uchaguzi huo kufanyika.