Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Heche aipa jukumu kamati kuu Chadema, amtaja Lissu

Muktasari:

  • Awali, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika amesema kikao hicho kimepata akidi ya kutosha, ambapo kati ya wajumbe 25 wenye haki ya kupiga kura ya kubariki uamuzi, 19 walikuwa wamewasili.

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tanzania Bara, John Heche, amewataka wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho kufanya maamuzi ya busara na yenye mwelekeo thabiti, akisisitiza kuwa hatima ya chama na nchi vipo mikononi mwao.

Aidha, amegusia masuala kadhaa likiwemo hitaji la kutafakari kwa kina mustakabali wa chama, kushinikiza kuachiwa kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, pamoja na viongozi waliokamatwa mkoani Dodoma, huku akielekeza kuendelea na usajili wa wanachama wapya nchi nzima.

Heche aliyasema hayo leo Jumanne, Aprili 28, 2026, katika makao makuu ya chama hicho, Mikocheni, jijini Dar es Salaam, wakati akifungua kikao cha siku mbili cha Kamati Kuu, kikiwa ni cha kwanza baada ya chama hicho kuruhusiwa kuendelea na shughuli za kisiasa.

Wajumbe wa kikao hicho wamejifungia kujadili na kutafakari kipindi cha mpito cha siku 309 bila shughuli za kisiasa, huku Heche akisema nchi na dunia zinasubiri kwa shauku kujua uelekeo wa taifa kupitia maamuzi yatakayofikiwa.

“Nataka kusema jambo hili kwa uzito mkubwa ili mjue. Hapa mlipokaa, hatima ya nchi yetu ipo mikononi mwenu. Tambueni uzito wa majukumu mnayobeba; dunia na nchi vinasubiri kujua mwelekeo wa taifa,” amesema.

Heche amesema Chadema ni chama kikuu cha upinzani nchini na kinapaswa kuwa na msimamo thabiti usiotetereka.

Wajumbe wa kamati Kuu Chadema, wakiwa katika kiko cha kamati Kuu jijini Dar es Salaam  Aprili 28, 2026. Picha na Michael Matemanga

“Mjadili kwa utulivu mkubwa. Watanzania wanataka kujua, na hata wadau tuliokutana nao kimataifa wanataka kusikia dira yetu,” ameongeza.

Katika hotuba hiyo, Heche pia ametoa wito kwa Serikali kumwachia huru Lissu bila masharti ili arejee kuongoza chama hicho.

“Aliyepaswa kuongoza kikao hiki ni mwenyekiti wetu Tundu Lissu, ambaye yuko gerezani. Tunaitaka Serikali imwachie bila masharti,” amesema.

Amesema msimamo huo umetokana na maamuzi ya vikao vya chama, akisisitiza kuwa lolote litakalompata kiongozi wao akiwa mikononi mwa dola halitakubalika.

“Tunasema tena: Tunataka Lissu aachiwe mara moja kwa sababu hana kosa; tunaona anaonewa. Tumewekewa masharti mengi ili aachiwe, lakini hatutapiga magoti, na yeye mwenyewe amekataa,” amedai.

Lissu anashikiliwa gerezani akikabiliwa na kesi ya uhaini kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.


Maagizo kwa viongozi

Heche pia amewataka viongozi wa chama kuendelea kusajili wanachama nchi nzima, akisema shauku ya wananchi kujiunga na Chadema imeongezeka kutokana na msimamo wake.

“Tanzania, ukitaka kuonekana mtu unayejielewa na mwenye mapenzi mema kwa nchi, lazima ujinasibishe na Chadema,” amesema.

Ameongeza kuwa licha ya changamoto za kipindi cha mpito, chama kimeendelea kuimarika kutokana na uvumilivu wa viongozi wake.

“Tungesambaratika, uhai wa chama ungekuwa hatarini. Lakini tumeendelea kusimama licha ya vitisho,” amesema.

Pia amesema baadhi ya viongozi wa chama wamekamatwa mkoani Dodoma wakati wakisajili wanachama, akamtaka Kamanda wa Polisi Mkoa huo kuwaachia mara moja.

Miongoni mwa waliotajwa kushikiliwa ni ofisa wa chama Shujaa Evarist, Katibu wa Mkoa Francisco Lawrence na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Mkoa wa Dodoma, Lukia Said.

Kwa mujibu wa Katibu wa Chadema Kanda ya Kati, Ashura Masound, viongozi hao walikamatwa mchana wa Aprili 27, 2026 na hadi usiku huo hawakuwa wameonekana katika kituo cha Polisi Central.

Makamu Mwenyekiti Chadema, John Heche akizungumza katika Mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga

Alisema chama kinaitaka polisi kueleza walipo viongozi hao. Jitihada za Mwananchi kupata ufafanuzi kutoka Polisi Mkoa wa Dodoma zinaendelea.


Mnyika azungumzia kikao

Awali, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, amesema kikao hicho kina akidi ya kutosha, ambapo kati ya wajumbe 25 wenye haki ya kupiga kura, wajumbe 19 wamehudhuria.

Alifafanua kuwa kuchelewa kuanza kwa kikao kulitokana na changamoto ya umeme na hitilafu ya jenereta katika majengo ya makao makuu ya chama.

Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa chama hicho, Brenda Rupia amesema kikao hicho kina ajenda kuu nne, taarifa ya utendaji na mali za chama, hali ya siasa nchini, hali ya siasa Zanzibar, pamoja na mpango kazi na bajeti ya chama.