Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hoja saba zilivyohitimisha kesi ya ubunge wa Baba Levo 

Muktasari:

  • Kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya Mwaka 2025 iliyotokana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ilifunguliwa na wapiga kura wanne wa jimbo hilo, Johary Kabourou, Luma Akilimali, Pendo  Kombolela,  Lumu  Mwitu.



Kigoma. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, imethibitisha ushindi wa Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando maarufu Baba Levo (CCM), baada ya kutupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wake, ikisema walalamikiwa wote hawana kesi ya kujibu.

Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi, Julai 16, 2026 na Jaji Victoria Nongwa, aliyekuwa akisikiliza shauri hilo.

Kesi ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025 ilifunguliwa na wapiga kura wanne wa Jimbo la Kigoma Mjini, Johary Kabourou, Luma Akilimali, Pendo Kombolela na Lumu Mwitu, kufuatia matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Mbali na Baba Levo, walalamikiwa wengine walikuwa ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Walalamikaji walikuwa wanadai uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kutokana na madai ya ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, wakimtuhumu Baba Levo kwa vitendo vya rushwa, matumizi ya hoja za kidini na kuhusishwa na vitendo vya utekaji.

Hata hivyo, baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi 16 wa walalamikaji, Jaji Nongwa amesema ushahidi uliowasilishwa haukufikia kiwango cha kisheria cha kuwalazimisha walalamikiwa kujibu madai hayo.


Hoja saba za mahakama

Katika uamuzi wake, Jaji Nongwa amesema mahakama iliongozwa na hoja saba ambazo walalamikaji walipaswa kuzithibitisha.

Kuhusu hoja ya kwanza ya madai kwamba Msimamizi wa Uchaguzi alikiuka masharti ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, Jaji Nongwa amesema walalamikaji hawakuwasilisha vielelezo muhimu, ikiwamo fomu za malalamiko ambazo zingethibitisha ukiukwaji huo.

Aidha, amesema walalamikaji hawakuonyesha namna madai ya kutotangazwa kwa mahali na muda wa majumuisho ya kura yalivyoathiri matokeo ya uchaguzi.

"Kutokuwepo kwa ushahidi huo kunamaanisha mlalamikiwa wa kwanza halazimiki kujitetea," amesema.

Katika hoja ya pili kuhusu madai ya matumizi ya dini wakati wa kampeni, Jaji Nongwa amesema ushahidi uliowasilishwa haukuonyesha kuwa Baba Levo alitumia nyumba za ibada au hoja za dini kuwashawishi wapiga kura wamchague au wasimchague mgombea mwingine.

Amesema pia ushahidi kuhusu kiongozi wa UVCCM kudaiwa kuonyesha picha ya mgombea wa ACT-Wazalendo na mkewe, haukuonyesha kuwa kitendo hicho kilifanywa kwa maelekezo au ridhaa ya Baba Levo.

"Walalamikaji hawakuonyesha kuwa hoja hizo zilitumika kuwashawishi wapiga kura kumchagua mlalamikiwa wa pili," amesema.

Kuhusu hoja ya tatu ya madai kwamba Baba Levo alitumia lugha ya kumdhalilisha mgombea wa ACT-Wazalendo, ikiwamo kumuita ‘dalali’ na kutumia jina ‘Mwamini’ badala ya ‘Mwami’, Jaji Nongwa amesema aliyedaiwa kuathirika, ambaye ni mgombea huyo, ndiye aliyepaswa kuonyesha namna kauli hizo zilivyomuathiri.

Katika hoja ya nne kuhusu madai ya rushwa, Jaji Nongwa amesema ushahidi uliowasilishwa haukufikia kiwango cha kuwalazimisha walalamikiwa kujitetea.

Amesema madai ya maofisa wa Serikali kushirikiana na Baba Levo katika kutoa fedha hayakuonyesha uhusiano wa moja kwa moja kwamba fedha hizo zilitolewa kwa maslahi ya mgombea huyo.

Vilevile, amesema michango aliyodaiwa kutoa kwa Bakwata, kanisani na ugawaji wa mavazi ya chama hauwezi kuwa ushahidi uliotafsiriwa kuwa rushwa ya uchaguzi.

"Ingekuwa tofauti kama michango hiyo ingetolewa kwa masharti kwamba wahusika wanapaswa kumchagua mgombea huyo pekee," amesema.

Mahakama pia imetupilia mbali madai kwamba msanii Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz aligawa fedha na kutoa ahadi za maendeleo kwa niaba ya Baba Levo, ikisema mazingira ya ushahidi huo hayakuthibitisha kuwapo kwa rushwa ya uchaguzi.

Katika hoja ya tano kuhusu madai ya utekaji wa mashahidi, Jaji Nongwa amesema mashahidi wengi walitoa ushahidi wa kusikia kutoka kwa wengine, huku shahidi mmoja pekee akidai kutekwa.

Amesema hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaomuunganisha Baba Levo na madai hayo.

Mahakama pia imekataa kupokea uzito wa vielelezo vya video vilivyowasilishwa na walalamikaji, ikisema havikukidhi vigezo vya kisheria vya ushahidi wa kielektroniki.

Kwa mujibu wa Jaji Nongwa, walalamikaji hawakuonesha nani alirekodi video hizo, zilitengenezwa kwa kifaa gani, zilihifadhiwaje na zilifikaje mahakamani, hali iliyotia shaka uhalisia wake.

Katika hoja ya sita, mahakama ilisema hata kama baadhi ya madai yangethibitika, walalamikaji hawakuonyesha kwa kiwango gani yalivyoathiri matokeo ya uchaguzi.

"Mahakama inakubaliana na hoja za mawakili wa walalamikiwa kwamba walalamikiwa wote watatu hawana kesi ya kujibu," amesema.

Kutokana na hitimisho hilo, Jaji Nongwa amesema walalamikiwa hawalazimiki kujitetea.

"Mahakama inaamua kwamba walalamikiwa wote hawana kesi ya kujibu. Shauri hili linatupiliwa mbali," amesema.


Baba Levo ashukuru,

walalamikaji wakata rufaa

Baada ya uamuzi huo, Baba Levo na wafuasi wake waliokuwa mahakamani walishangilia kwa kukumbatiana na kuimba nyimbo za kusherehekea ushindi.

Akizungumza baada ya hukumu, Baba Levo amesema anamshukuru Mungu kwa kile alichokiita haki kutendeka.

Amesema ametumia fedha nyingi kufuatilia kesi hiyo na sasa anataka kuelekeza nguvu zake katika kuwatumikia wananchi wa Kigoma Mjini.

"Nimezaliwa kuwatumikia Wanakigoma. Sasa waniachie nifanye kazi na matokeo yataonekana ndani ya miaka mitano ya ubunge wangu," amesema.

Hata hivyo, Walalamikaji, kupitia wakili wao, John Seka, wamebisha hodi katika Mahakama ya Rufani kwa ajili ya kupinga uamuzi huo.

Tayari wamewasilisha katika mahakama hiyo notisi ya kusudio la kukata rufaa, hatua ambayo ni ya msingi wakati wakisubiri kumbukumbu za rufaa na kuwasilisha sababu zao za rufaa.